NA MBARUKU YUSUPH, TANGA
WATU 12 wamepoteza maisha baada ya jahazi walilokuwa
wakisafiria kuzama huku wengine 27 wakijeruhiwa.
Jahazi hilo linalofanya safari zake kati ya Pemba na Tanga
lilizama katika kisiwa cha Jambe kilichopo bahari ya Hindi nje kidogo ya jiji
la Tanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba
alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa ilitokea saa 12:30.
Wakulyamba alisema jahazi hilo lilikuwa linaendeshwa na nahodha
Badru Sa.idi, ambaye pia alifariki lilikuwa na namba za usajili MV Z5512
maarufu kama Sayari
Alisema juhudi za kuopoa miili inaendelea.
Aidha alisema mpaka sasa chanzo cha ajali hiyo hakijajulikana
na Jeshi la Polisi linachunguza ili kubaini huku taarifa za awali zikisema kuwa
chombo hicho kilipigwa wimbi eneo la nyuma na kupoteza muelekeo.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Bombo, Dk.
Goodluck Mbwilo alithibitisha kupokea miili 12 pamoja na majeruhi 25.
Aidha alisema kuwa kati ya maiti hizo sita ni watu wazima na
sita ni watoto wadogo ambao bado hawajatambuliwa na imehifadhiwa hospitalini
hapo.
Baadhi ya majeruhi walisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni
upepo mkali.
Juma Maduhu Mkazi wa Bariadi alisema kuwa chombo hicho kiliondoka
saa 4:00 usiku na baada ya mwendo wa masaa mawili nahodha alilazimika
kusimamisha safari kutoka na kuwepo na upepo mkali baharini.
Alisema kuwa walipofika katika kisiwa cha Jambe jahazi hilo
lilianza kujaa maji ndani na kuanza kutoa ambapo yaliwashinda nguvu na
kusababisha chombo hicho kupasuka na kuzama.
Mbunge wa Tanga (CUF), Mussa Mbaruku, ametoa msaada wa sanda
kwa maiti 12 na kuwataka wafiwa kuwa na moyo wa subra katika kipindi hiki cha
msiba.
Mbunge huyo aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa boti lililoletwa
kwaajili ya Bagamoyo kwenda Dar es Salaam kuhamishiwa Tanga.
No comments:
Post a Comment