HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 30, 2017

HALMASHAURI ZIFANYE KAZI KWA WELEDI-MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa akihutubia leo wakati wa kufungua Baraza la Ushauri (RCC) Mkoa wa Dodoma ambapo lilishirikisha Wizara, Idara na Wadau mbalimbali wanaoratibu ujio wa Serikali kuhamia Makao makuu Dodoma Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Chuo cha mipango ya Maendeleo Vijijini Dodoma ( Picha na PMO)

*Azitaka zisiwe pango la wezi, wazembe

WAZIRI MKUU Kassm Majaliwa amesema wakati umefika wa kuwa na watumishi wenye weledi wa kutosha kwenye Halmashauri zote nchini na pia hazitakiwi kuwa pango la wezi, wazembe au jalala la kutupa wabadhilifu walioshindikana kwingineko.

Aidha, Waziri Mkuu amesemma Serikali za Mitaa na Halmashauri zote nchini zinatakiwa zianze kujitathmini na kujipanga vizuri zaidi kuona ni kwa namna gani zitakuwa chachu ya maendeleo ya viwanda vinavyotarajiwa.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Januari 30, 2017) wakati akifungua Kikao cha Baraza la Mashauriano (RCC) mkoani Dodoma. Amesema kikao ni chombo muhimu na endapo kitatumika vizuri kitaweza kusaidia kusukuma maendeleo ya Mkoa na kupunguza migogoro kwenye Halmashauri.

Amesema Serikali itaendelea kuongeza kiwango cha ruzuku kwa Halmashauri zote nchini kwa kadiri uwezo utakavyoruhusu na kusisitiza kwamba fedha hizo lazima zisimamiwe vizuri na zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo inayowagusa wananchi.

“Endapo itabainika kwamba kuna baadhi ya Sheria zinazokwamisha utendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, hatutasita kuzifanyia mapitio na hatimaye kuzibadili ili ziendane na azma yetu ya kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema.

Amesema Serikali ina maslahi makubwa kwa Serikali za Mitaa, sio tu kwa kuwa ni Serikali kamili katika ngazi hiyo, bali pia kutokana na ukweli kwamba kero nyingi za wananchi ziko katika ngazi hiyo.

Waziri Mkuu amesema vyanzo vingi vya mapato ya Serikali vinapatikana kwenye Halmashauri huku changamoto kubwa ikiwa ni kulegalega kwa  Halmashauri nyingi katika ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi jambo linalozorotesha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hivyo Waziri Mkuu ametoa rai kwa Halmashauri hizo kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi na kutatua kero zao kikamilifu na kwa wakati pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato.

Pia zihakikishe malipo yote yanafanyika kwa njia za kielektoniki na zihamasishe vijana na akina mama wajiunge kwenye vikundi vya uzalishaji mali na kuwapatia stadi za kazi na mikopo yenye masharti nafuu ili waweze kuwa chanzo cha mapato hapo baadaye.

Amesema watendaji wa Halmashauri wanatakiwa  kujiepusha na vitendo vya rushwa na ubadhilifu wa mali za umma na uzembe kazini na watakaobainika kufanya vitendo hivyo  wachukuliwe hatua kali za kisheria na kinidhamu.

“Someni taarifa ya CAG (Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali) na kutoa majibu ya kina ya namna mtakavyodhibiti mianya ya rushwa na ubadhilifu kama ilivyoainishwa kwenye ripoti hizo,” amesema.

Hata hivyo amesema kila Halmashauri iandae mpango wa utekelezaji wa Ilani ya CCM kwenye maeneo makubwa ya kipaumbele kama vile ujenzi wa miundombinu ya shule,  maboresho kwenye sekta ya afya (ujenzi wa hospitali, zahanati na vituo vya afya).

“Endeleeni kuwa na mahusiano mazuri miongoni mwenu, mfanye kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.  Kila mmoja kwa nafasi aliyonayo atimize wajibu wake na kuzingatia mipaka ya nafasi yake. Punguzeni migogoro, matusi, dharau, bezo na vitisho. Mshirikiane na jamii ione mpo wamoja,” amesema.
  
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATATU, JANUARI 30, 2017 

No comments:

Post a Comment

Pages