Benjamin Sawe, Maelezo Dar es Salaam
Mkuu wa wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma Bw. Deogratius Ndejembi amepiga marufuku matumizi ya nafaka kutengenezea pombe za kienyeji ili kujikinga na baa la njaa.
Bw. Ndejembi amesema kumekuwa na tabia ya wananchi kufanya sherehe zisizokuwa na tija ikiwemo zile za jando na ngoma za asili kwa kutumia nafaka
Akizungumza na Idara ya Habari Bw. Ndejembi amesema hivi sasa wilayani Kongwa kipo chakula cha kutosha majumbani, sokoni na kwenye Maghala yanayotumika kuhifadhi chakula.
Amesema chakula kilichopo kikitumika vizuri kitawatosheleza wananchi mpaka pale watakapovuna mazao mengine katika msimu wa mavuno ujao.
“Kongwa chakula kipo cha kutosha, wanaosema hakuna chakula ni wafanyabiashara wanaotaka kuzua hofu ili wapandishe bei ya mazao na wanasiasa waliokosa ajenda” Alisema Ndejembi.
Mkuu huyo wa wilaya amesema hakuna sababu ya kuficha kama itatokea kuna upungufu wa chakula lakini kwa sasa hakuna upungufu wowote wa chakula wilayani Kongwa.
Bw. Ndejembi amefanya ziara ya kutembelea maghala ya chakula yaliyopo Kibaigwa wilayani Kongwa ambako pia kuna soko la mahindi la kimataifa na kujiridhisha na chakula kilichopo.
“Mahindi yapo ya kutosha na kama unavyojua hili ni soko la Kimataifa inamaana kungekuwa na upungufu ungeanzia hapa” Alisema Ndejembi.
No comments:
Post a Comment