HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 14, 2017

SMZ YAPONGEZWA KWA KULETA MAENDELEO

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akibadilishana mawazo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania, Generali Davis Mwamunyange Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. 
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania, Generali Davis Mwamunyange akipokea zawadi ya Mlango kutoka kwa Balozi Seif  kama ishara ya utumishi wake uliotukuka kwa jinsi alivyolitumikia Jeshi la Wananchi kwa  nidhamu takriban miaka 45. Picha na – OMPR – ZNZ

ZANZIBAR

Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeelezea faraja yake kutokana na juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika  kuwaletea Maendeleo Wananchi wake bila ya bila ya kuingizwa cheche za kibaguzi.

Faraja ya Jeshi hilo imekuja kufuatia ushuhuda wa Taasisi za Kimataifa  zinavyothibitisha  maendeleo makubwa yaliyofikiwa na  wananchi wa Zanzibar na kubadilisha ustawi  na  uchumi wao ndani ya kipindi cha zaidi ya miaka 50 iliyopita.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Majeshi ya ulinzi na usalama Tanzania  General Davis Mwamunyange wakati akiwasilisha salamu za pongezi za Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokana na kufanikisha vyema sherehe za Maadhimisho ya kutimia miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

General Mwamunyange alisema ongezeko la miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiambatana na Miundombinu imara inayowekwa katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba imewawezesha wananchi mbali mbali kuwa na uhakika wa kuendesha maisha yao ya kila siku.

Alisema Visiwa vya Zanzibar hivi sasa vimebadilika kiuchumi pamoja na kibiashara kiasi cha kuzioa harakati za kibiashara na kimaisha kuongezeka zaidi zinazotoa fursa kwa wawekezaji wa nje ya Zanzibar kuanzisha miradi yao inayosaidia kuongeza pia fursa za ajira hasa kwa kundi la Vijana.

Akizungumzia migogoro ya Ardhi inayojichomoza kati ya Wananchi  na Kambi za Jeshi hilo ziliopo jirani na maeneo yao Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi   Tanzania  alisema Uongozi wa Jeshi hilo utaandaa utaratibu maalum wa kuyaachia  baadhi ya maeneo ya ardhi ambayo hayana umuhimu kwa shughuli za kiulinzi ili yatumiwe na Wananchi kwa shughuli zao za Kimaisha.

General  Devis  Mwamunyange alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba  mahitaji ya ardhi kwa sasa hapa Nchini yamekuwa makubwa kutokana na ongezeko kubwa la Idadi ya Watu pamoja na kubadilika kwa harakati za Kiuchumi.

Aliwashukuru Wananchi wa maeneo yaliyoibuka migogoro hiyo kuendelea kuwa wastahamailivu na kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi iliyochukuwa ya kusaidia kutafuta suluhu  ya migogoro hiyo jambo ambalo limesaidia kuleta hali ya utulivu na amani katika maeneo hayo.

Akitoa shukrani zake kwa kazi kubwa ya ulinzi  inayoendelea kufanywa na Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema nidhamu na Heshima iliyojengeka ndani ya vikosi hivyo vimeiwezesha Tanzania kuwa na heshima Kimataifa.

Balozi Seif alisema Umoja wa Mataifa (UN) umekuwa ukikimbilia Tanzania kutaka nguvu za ulinzi isaidie kwenye maeneo ya Mataifa yenye migogoro ya kisiasa na kiusalama baada ya kubaini nidhamu kubwa iliyopo ndani ya Jeshi la Tanzania.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  alisema Vikosi vya Ulinzi Tanzania vimekuwa na uwezo, nguvu, uzoefu na nidhamu  kubwa ya kusimamia ulinzi wa Taifa na haya yamepatikana kutokana na mafunzo wanayopewa na Wataalamu pamoja na Viongozi wao.

Balozi Seif alitumia mkutano huo kuwasilisha salamu za pole kwa Uongozi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania kufutia kifo cha Kamanda wa Brigedia ya Nyuki Zanzibar Brigedia Generali Cyrill Ivor Mhaiki.

No comments:

Post a Comment

Pages