HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 10, 2017

RAIS DKT. MAGUFULI AHUTUBIA KATIKA SHEREHE ZA MWAKA MPYA KWA MABALOZI (NEW DIPLOMATIC SHERRY PARTY) IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli akihutubia Mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini katika Sherehe za Mwaka mpya kwa Mabalozi(New Diplomatic Sherry Party) Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais John Magufuli akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Augustine Mahiga katika picha ya pamoja na Mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa nchini baada ya kuwahutubia katika Sherehe za Mwaka mpya kwa Mabalozi (New Diplomatic Sherry Party) Ikulu jijini Dar es Salaam. (Picha na Ikulu).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amezialika nchi mbalimbali na wadau mbalimbali wa maendeleo kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kujenga uchumi wa viwanda utakaoiwezesha Tanzania kuingia katika nchi ya kipato cha kati.

Mhe. Rais Magufuli ametoa rai hiyo leo, wakati akihutubia sherehe ya kuaga mwaka mpya kwa Mabalozi na Wawakilishi wa mashirika ya kimataifa (New Year Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Dkt. Magufuli amesema ifikapo mwaka 2020 Tanzania imedhamiria uchumi wake ukue kwa wastani wa asilimia 10, sekta ya Viwanda iajiri asilimia 40 ya watanzania na pato la mtu kwa mwaka likue hadi kufikia wastani wa Dola 3,000 za kimarekani (sawa na Shilingi na takribani shilingi Milioni 6 na Laki 6 kwa mwaka)

Pamoja na kuwepo kwa malengo hayo, Mhe. Rais Magufuli amewaomba Mabalozi wote wanaoziwakilisha nchi mbalimbali hapa nchini na Wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya kimataifa kuwaleta wawekezaji hususani katika sekta ya viwanda kwa kuwa fursa zipo.

Pia amewaomba wawahamasishe wadau watakaokuwa tayari kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi ikiwemo ujenzi wa reli ya kati yenye urefu wa Kilometa 1,200 kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza na Kigoma na kuunganisha hadi nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda, na kwamba tayari Serikali itaanza kujenga Kilometa 300 za kuanzia Dar es Salaam mwaka huu.

Kuhusu mwaka uliopita, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali imeanza kutekeleza awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo (2016-2021) uliopangwa kugharimu Shilingi Trilioni 107 ambapo kati ya fedha hizo Shilingi Trilioni 59 zitatolewa na Serikali ya Tanzania na kiasi kinachobaki kitatolewa na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Mhe. Dkt. Magufuli amebainisha kuwa katika kutekeleza mpango huo, Serikali imechukua hatua ya kuongeza bajeti ya maendeleo kutoka asilimia 26 hadi kufikia asilimia 40 katika mwaka huu.

Pamoja na kuwashukuru kwa ushirikiano walioendelea kuuonesha katika mwaka uliopita Mhe. Rais Magufuli amewaahidi Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na nchi zao na Taasisi zao katika masuala mbalimbali hasa uchumi.

Akizungumza kwa niaba ya Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Kiongozi wa wanadiplomasia hao Mhe. Edzai Chimoyo ambaye ni Balozi wa Zimbabwe hapa nchini, amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Magufuli katika kupambana na rushwa, kujenga nidhamu kwa watumishi wa umma na kuimarisha uchumi na ameahidi kuwa yeye na wenzake wapo tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Awamu ya Tano.

Pia amepongeza juhudi kubwa zilizofanywa kufufua Shirika la Ndege (ATCL) kwa kununua ndege mpya ambazo licha ya kurahisisha usafiri zitasaidia kukuza sekta ya utalii hapa nchini.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

10 Februari, 2017

No comments:

Post a Comment

Pages