February 05, 2017

WAZIRI NAPE NNAUYE ATANGAZA RASMI KUANZA KUTUMIKA KWA SHERIA ZA HUDUMA ZA HABARI NA KANUNI ZAKE

Na Lilian Lundo, MAELEZO–Dodoma

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametanga rasmi kuanza kutumika kwa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2017.

Nape Nnauye ametoa taarifa hiyo leo katika ukumbi wa Bunge, Mjini Dodoma alipokuwa akiongea na vyombo vya habari juu ya kuanza kwa sheria hiyo na kanuni zake.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 1 cha Sheria hiyo, ili ianze kutumika rasmi, Waziri wa Habari anatakiwa kuitangaza tarehe ya kuanza kutumika, hivyo napenda kuufahamisha Umma kuwa sheria hii imeanza kutumika tangu Desemba 31, 2016,” alifafanua Nape Nnauye.

Aliendelea kwa kusema kuwa kuanza kutumika kwa sheria hii ni jambo muhimu sana kwa tasnia hiyo kwa sababu inaihamisha taaluma ya habari kutoka fani ambayo mtu yeyote anaweza kujinasibu nayo hadi kuwa taaluma kamili yenye sifa mahsusi, maadili yanayojulikana pamoja na vyombo vya kusaidia kusimamia utekelezaji wake.

Vile vile amesema kuwa, sheria hiyo inaleta mfumo madhubuti wa kulinda haki za wanahabari kukusanya, kuhariri na kusambaza habari zao kwa uhuru.

Pia sheria hiyo imeweka wajibu kwa wale watakaokiuka misingi na maadili ya taaluma hiyo, hivyo ukurasa mpya wa haki na wajibu umefunguliwa kupitia sheria hiyo. 

Aidha amesema kuwa, Wizara imechambua maoni mbalimbali kuhusiana na sheria hiyo ambapo moja ya maoni hayo ilikuwa ni kiwango cha elimu cha mtu atakayeruhusiwa kufanya kazi ya taaluma hiyo.

Ambapo wapo  waliopendekeza kiwango cha elimu kiwe cheti, wengine diploma, digrii na hata PhD na wengine walitaka awe mtu yeyote anayejua kusoma na kuandika. 

Amesema kuwa Serikali imesimama katikati ya maoni hayo, na sifa ya chini kabisa kwa kuanzia itakuwa ni Diploma ya uandishi wa Habari. Hivyo Serikali imetoa kipindi cha miaka Mitano kuanzia Januari, 01, 2017 kwa waandishi ambao hawana sifa hizo kujiendeleza na kufikia kiwango hicho cha elimu.

Hivyo basi, Idara ya Habari MAELEZO itaendelea kutoa “Press Card” bila kuwabana wanahabari kwa kuangalia vigezo hivi vya kitaaluma bali dhamana ya waajiri wao.

Sheria ya Huduma za Habari, 2016 ilisainiwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli Novemba 16, 2016 na kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali Novemba 18, 2016.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Moses Nnauye akioongea na Waandishi wa Habari kuhusu siku rasmi ya kuanza kutumika kwa Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 pamoja na Kanuni zake za 2017 katika Ukumbi wa Idara ya Habari Bungeni Mjini Dodoma 05/02/2017. Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Dkt. Hassan Abbasi. (Picha na Benedict Liwenga-WHUSM). 

No comments:

Post a Comment

Pages