HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 23, 2017

VIONGOZI WA AFRIKA WAKUBALIANA KUFUNGUA FURSA ZA KIBIASHARA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema viongozi wa mataifa ya Afrika wamekubaliana kufungua fursa za kiuchumi baina ya nchi hizo pamoja na kuweka utaratibu wa kutumia hati moja ya kusafiria.

Alitoa kauli hiyo jana (Jumatano, Machi 22, 2017) wakati akingumzia makubaliano yaliyofikiwa katika uzinduzi wa Jukwaa la Uchumi Barani Afrika (AEP) uliofanyika nchini Mauritius Machi 20 hadi 21, 2017. Waziri Mkuu alimuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli.

Waziri Mkuu alisema viongozi hao wamekubaliana kwamba mataifa ya Afrika yawe na hati moja ya kusafiria, ambayo itawawezesha wananchi kuingia nchi yoyote ndani ya bara hilo bila ya vikwazo kwa lengo la kurahisisha muingiliano wa watu na bidhaa.

Alisema jambo jingine walilokubaliana ni kuimarisha Jumuiya zao ikiwemo ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na kuzishawishi nchi nyingine ambazo hazijajiunga kujiunga jumuia hizo.

Alisema viongozi hao walijadili namna watakavyoweza kuinua uchumi na kuweka mikakati ya kuimarisha viwanda, ambapo Tanzania ipo katika nafasi nzuri kwa kuwa tayari inatekeleza mpango wa kukuza uchumi wake kwa kupitia sekta ya viwanda.

Viwanda ndiyo mkombozi wa changamoto mbalimbali barani Afrika ikiwemo ya ajira, hivyo Serikali ya awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuongeza ajira na kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake,” alisema.

Jukwaa hilo lilizinduliwa Machi 20, 2017 na Waziri Mkuu wa Swazland Bw. Barnabas Sibusiso Dlamini kwa niaba ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) na Rais wa Chad, Idriss Deby. Pia Bw. Dlamini alimuwakilisha Mfalme Muwsati wa III.

Bw. Dlamini alisema nchi za Afrika zinatakiwa kuboresha mitaa yake na kujikita katika kutoa elimu ya masuala ya sayansi na viwanda ili kuwajengea wanafunzi uelewa wa masuala hayo angu wakiwa na umri mdogo.

Alisema iwapo wanafunzi wataanza kujifunza masuala ya viwanda kuanzia shule watakuwa na uelewa wa kutosha wa masuala hayo jambo ambalo litawarahisishia kupata ajira katika viwanda mbalimbali, hivyo kuondokana na tatizo la ajira linalozibakili nchi nyingi za Afrika.

Uzinduzi wa jukwaa hilo ulikuwa na ajenda nne ambazo zilihusu sekta ya viwanda, kukuza biashara miongoni mwa nchi za Afrika, kukuza ujuzi katika taaluma mbalimbali na kurahisisha muingiliano wa watu na bidhaa baina ya mataifa hayo.

Jukwaa hilo lilifanyika kwa siku mbili lilihudhuriwa na viongozi wakuu wa nchi za Afrika, wanazuoni, wafanyabiashara pamoja na watu kutoka kwenye asasi mbalimbali za kiraia barani Afrika.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, MACHI 23, 22017.

No comments:

Post a Comment

Pages