HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 06, 2017

SERIKALI YAFUTA TOZO ZA MAZAO YA CHAI, PAMBA NA KAHAWA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imefuta baadhi ya tozo katika mazao ya pamba, chai na kahawa ambazo ni kero kwa wakulima ikiwemo ya sh. 450,000 iliyokuwa inatolewa na kila kiwanda cha kuchambua pamba kwa ajili ya kuchangia mbio za Mwenge.

Amesema tozo nyingine iliyofutwa kwa zao la pamba ni ada ya vikao vya Halmashauri za Wilaya ambayo ni sh. 250,000, ambapo katika zao la chai kodi ya moto na uokoaji imeondolewa na kwenye zao la kahawa, ada ya leseni ya kusindika kahawa ya Dola za Marekani 250 imefutwa.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Aprili 6, 2017) katika hotuba yake ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2017/2018 Bungeni mjini Dodoma.

Amesema kufutwa kwa tozo hizo ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali kwa wakulima nchini ili kuwapunguza kodi, tozo na ada mbalimbali zinazochangia kuwapunguzia faida.

“Serikali pia imeboresha mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuanzisha utaratibu wa wazi wa ununuzi wa mazao kupitia minada na katika msimu wa mwaka 2016/2017 kwenye zao la korosho, utaratibu huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa bei ya korosho kwa kilo kutoka sh  1,200 hadi sh 3,800, bei ambayo haijawahi kufikiwa katika historia ya zao la korosho nchini,” amesema.

Amesema mfumo huo wa stakabadhi ghalani na utaratibu wa minada umeongeza ushindani na kuvutia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi hususan nchi ya Vietnam na nchi nyingine kuja wenyewe kununua korosho badala ya kutegemea soko la India pekee.

Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea na uchambuzi wa kina wa kodi, tozo na ada zilizobaki katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la kuziondoa au kuzipunguza ili kumwezesha mkulima kunufaika zaidi na jasho lake na kuongeza mapato ya Halmashauri.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema Bunge lilipitisha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016, ambayo ni muhimu katika kuimarisha usimamizi na uwajibikaji katika Sekta ya Habari nchini, ambapo Kanuni za Sheria hiyo  zimeandaliwa na tayari zimeanza kutumika.

“Natoa wito kwa wadau wa sekta ya habari kuzingatia sheria na kanuni hizo ili kuimarisha weledi katika tasnia ya habari. Aidha, nashauri wadau wa habari kujikita zaidi katika kuandika na kutangaza habari za masuala ya maendeleo na uchumi ili kuwasaidia wananchi kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na kuboresha huduma za kijamii,” amesema.

Pia Waziri Mkuu amevikumbusha vituo vya televisheni kuweka wakalimani wa lugha katika vituo vyao. Amesema katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kutoa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye ulemavu shuleni na vifaa vya kufundishia.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kwamba Serikali imeendelea kutoa huduma pamoja na kuongeza upatikanaji wa haki na fursa kwa watu wenye ulemavu na katika kutimiza azma hiyo, amewaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa Kamati za Watu wenye Ulemavu zinaanzishwa katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Mitaa na Vijiji.

Pia Serikali imeanzisha kampeni za kupinga unyanyapaa na vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Geita, Simiyu, Kagera, Tabora, Kigoma, Mara, Mbeya, Katavi na Rukwa na kampeni hiyo itaendelea nchi nzima.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S.L.P 980, DODOMA
ALHAMISI, APRILI 6, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages