1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa Hoja kwamba kutokana na taarifa zilizowasilishwa
leo katika Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Katiba na Sheria, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua
Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya
Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2016/2017 na Mwelekeo wa
Kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018. Aidha, ninaliomba Bunge lako Tukufu
likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri
Mkuu na Taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
2.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Bunge
lako Tukufu limeondokewa na Wabunge wenzetu, Mheshimiwa Hafidh Ally Tahir
aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Dimani - CCM na Mheshimiwa Dkt. Elly Marko Macha,
aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum - CHADEMA. Pia, Taifa lilimpoteza Mheshimiwa
Samwel John Sitta aliyekuwa Spika Mstaafu wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Aidha, nchi yetu imekumbwa na majanga na maafa
yaliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali. Ninaomba Mwenyezi Mungu
awajalie nafuu ya haraka wale wote waliopata majeraha, na kuwapumzisha kwa
amani wale waliopoteza maisha, Amina!
Ninatoa pole kwa familia za wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki. Pia
ninatoa pole kwa Mheshimiwa Aida Khenani aliyepata ajali ya kugongwa na
pikipiki wakati akitoka Bungeni. Tunamuombea apone haraka na aweze kurejea
Bungeni ili kuendelea na majukumu yake.
PONGEZI NA SHUKRANI
3.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii
kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Makamu wa Rais na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar kwa kutimiza mwaka mmoja wa
uongozi wao. Sisi tunaowasaidia tunajivunia uongozi wao mahiri, uzalendo
uliotukuka na dhamira njema waliyonayo kwa Watanzania.
4. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Bunge lako Tukufu limepokea na kuwaapisha
Wabunge wapya watano, ambao ni Mheshimiwa Abdallah Majura Bulembo (Mb.),
Mheshimiwa Anne Killango Malecela (Mb.), Mheshimiwa Juma Ali Juma (Mb.),
Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb.) na Mheshimiwa
Salma Rashidi Kikwete (Mb.). Ninawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wapya kwa
heshima waliyoipata ya kujumuika nasi kwenye Bunge hili. Kama ilivyo ada,
tutatoa ushirikiano unaotarajiwa kwa Waheshimiwa Wabunge hawa ili watekeleze
majukumu yao kwa ufanisi na tija. Kipekee, ninampongeza Mheshimiwa Prof.
Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba
na Sheria.
Pia ninatumia nafasi hii
kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote walioteuliwa kuingia kwenye Bunge la
Afrika Mashariki, Makatibu Wakuu wapya walioteuliwa na Mheshimiwa Rais yaani
Profesa Kitila Alexander Mkumbo, Dk. Leonard Akwilapo, Maimuna Tarishi na Dk.
Ave Maria Semakafu. Nawapongeza sana wote walioteuliwa kushika nyadhifa hizo.
5.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii
kuwashukuru Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kazi kubwa ya kupitia
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali
zinazojitegemea na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Ninawashukuru kipekee sana Wajumbe
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria inayoongozwa na Mheshimiwa
Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile,
Mbunge wa Kigamboni na Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mheshimiwa Hawa
Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini kwa kutoa mchango mkubwa wakati
wa maandalizi ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri
Mkuu. Pia, niwapongeze Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za
Bunge kwa kuongoza kwa umahiri mkubwa Kamati zao wakati wa kupitia makadirio ya
sekta zote. Maoni na ushauri wao umesaidia sana kuboresha Makadirio ya Bajeti
ya Serikali kwa mafungu yote.
6. Mheshimiwa Spika, niruhusu pia niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu
Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Makatibu Wakuu, Wakuu
wa Mikoa na Wilaya, Wakuu wa Idara, Mashirika na Taasisi zote za Serikali kwa
ushirikiano wanaoendelea kunipa katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, ninawashukuru
Wafanyakazi wote wa Serikali na Taasisi zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu
Kiongozi, kwa kukamilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/2018.
7. Mheshimiwa Spika, kipekee, ninamshukuru Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama (Mb.), Mbunge wa Peramiho, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu);
Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde (Mb.), Mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana) kwa ushirikiano wao mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya
Ofisi ya Waziri Mkuu. Aidha, ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Abdallah Possi aliyekuwa
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa aliyofanya wakati
akiitumikia nafasi hiyo. Ninamtakia kazi njema kwenye jukumu lake jipya la kuiwakilisha Tanzania nchini
Ujerumani. Vilevile, ninawashukuru wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu,
chini ya Uongozi wa Makatibu Wakuu, Dkt. Hamisi H. Mwinyimvua; Bwana Eric F.
Shitindi na aliyekuwa Katibu Mkuu Bwana Uledi A. Mussa kwa ushauri wao wa
kitaalam kwangu na kwa Waheshimiwa Mawaziri.
8.
Mheshimiwa Spika, ninazishukuru pia nchi marafiki,
Taasisi na Mifuko ya Fedha Duniani, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Madhehebu ya
Dini na Mashirika yasiyo ya Kiserikali kwa kuunga mkono jitihada za Serikali
katika kujenga uchumi wa nchi yetu.
Misaada na mikopo iliyopatikana kwa wakati imechangia kutekeleza miradi
ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
9.
Mheshimiwa Spika, ninapenda kutumia fursa hii
kuwashukuru kwa dhati wananchi wa Jimbo la Ruangwa kwa kuendelea kuniunga mkono
na kuielewa vizuri dhamana ya Kitaifa niliyonayo ya kusimamia utendaji wa
Serikali katika sekta zote na kuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Mwisho ninaishukuru familia yangu
hususan mwenza wangu mpendwa, Mary na watoto wetu kwa upendo, dua na kuendelea
kunitia moyo ili nitekeleze kwa ufanisi zaidi majukumu yangu ya Kitaifa. Asanteni
sana!
MWELEKEO WA BAJETI
10.
Mheshimiwa Spika, ni mwaka mmoja sasa
tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani. Katika kipindi hicho, yapo mambo mengi yaliyofanyika kwa mafanikio
makubwa ambayo yataanishwa kwa kina katika bajeti za Sekta pindi Mawaziri
husika watakapoziwasilisha. Baadhi ya mafanikio hayo ni utekelezaji wa ahadi ya
Serikali ya Elimu Bila Malipo; kuongezeka kwa uzalishaji na kasi ya usambazaji
wa umeme vijijini; kuimarika uwajibikaji na nidhamu katika Utumishi wa Umma; kuongeza
ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa matumizi ya fedha za Umma; kuboresha huduma
za kiuchumi na za kijamii; na kutekeleza Awamu ya Kwanza ya Mpango wa Serikali
Kuhamia Dodoma. Nitumie fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge, Viongozi wa
Serikali, Watumishi wa Umma na Watanzania wote kwa ujumla kwa kuendelea kuiunga
mkono Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake, kwani bila ushirikiano wao,
tusingeweza kupata mafanikio hayo.
11.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Ofisi ya Waziri
Mkuu imeendelea kuandaliwa kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha
Mapinduzi ya mwaka 2015; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano; ahadi za
Mheshimiwa Rais alizotoa wakati wa Kampeni, pamoja na maelekezo yake wakati
anazindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba,
2015. Bajeti hii itaendelea kuimarisha mafanikio yaliyopatikana katika mwaka
uliopita na kushughulikia utatuzi wa vikwazo vya kukuza uchumi kwa haraka na
baadhi ya changamoto zilizojitokeza. Aidha, Serikali itajikita zaidi katika
maeneo yatakayochangia kuimarisha uchumi wa viwanda na kuboresha huduma za
jamii. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla, kuendelea
kushirikiana na Serikali katika kufikia azma hiyo ili dhamira yetu
ya kuboresha maisha ya Watanzania iweze kutimia. Ni vyema tukakumbuka kwamba
tuna mwaka mmoja tu wa utekelezaji wa yale tuliyopanga kufanya ndani ya kipindi
cha miaka mitano. Tutatumia bajeti ya mwaka ujao wa fedha kukabili changamoto
zilizojitokeza. Ahadi ya Serikali ni kuendelea kuwatumikia wananchi kwa
uadilifu na bila ubaguzi wowote, huku tukitanguliza mbele maslahi ya Taifa.
SERIKALI KUHAMIA DODOMA
12. Mheshimiwa Spika, tarehe 23 Julai 2016, Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihutubia Mkutano Mkuu Maalum
wa Chama Cha Mapinduzi, alitangaza uamuzi wa kuhamishia rasmi Shughuli za
Serikali Kuu Dodoma. Kufuatia uamuzi huo, mipango ya kuhamia Dodoma kwa awamu
ilianza baada ya mahitaji halisi yatakayoiwezesha Serikali kuhamia Dodoma
kubainishwa, ikiwa ni pamoja na ofisi na nyumba za makazi kwa viongozi na watumishi
wa umma. Awamu ya kwanza ilipangwa kuhama ifikapo mwisho wa mwezi Februari,
2017.
13.
Mheshimiwa
Spika, ninafurahi kuliarifu
Bunge lako Tukufu kwamba tayari watumishi 2,069 wakiwemo Mawaziri, Naibu
Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, baadhi ya Wakuu wa Idara na
Vitengo na watumishi wengine wamekwishahamia Dodoma kama ilivyopangwa.
Vilevile, Wizara zote zimepata majengo ya Ofisi yatakayotumika katika kipindi
cha mpito.
14.
Mheshimiwa
Spika, ili Mji wa Dodoma uweze
kuendelezwa kwa mpangilio mzuri, Serikali inaupitia upya Mpango Kabambe wa Mji
wa Dodoma. Mapitio hayo yatasaidia sana kuepuka makosa yaliyofanyika katika
miji mingi hususan ujenzi holela unaochangia katika uchafuzi wa mazingira na
kuharibu mandhari ya miji. Ni wazi kwamba, ujenzi wa Mji wa Dodoma hautafanywa
na Serikali pekee, bali tutaendelea kuhamasisha Sekta binafsi na wadau wengine
kuwekeza Dodoma. Ninalipongeza sana Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa
kujenga nyumba 300 za makazi hapa Dodoma ambazo watumishi wanaweza kununua au
kupangishwa. Ninatoa wito kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma kuongeza kasi ya
upimaji wa viwanja, kuboresha miundombinu na kudhibiti ujenzi holela kwa kushirikiana
kwa karibu na Manispaa ya Dodoma na Taasisi nyingine za Serikali.
SIASA
15. Mheshimiwa Spika, mwaka mmoja baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, hali
ya kisiasa nchini imeendelea kuwa shwari na ya kuridhisha. Aidha, Chaguzi Ndogo
zilifanyika tarehe 22 Januari, 2017 katika Jimbo la Dimani - Zanzibar na
Udiwani katika kata 20 Tanzania Bara kwa kushirikisha wagombea kutoka vyama 15
vya siasa. Ninavipongeza vyama vyote vilivyoshiriki katika chaguzi hizo, na
kipekee nakipongeza Chama cha Mapinduzi kwa ushindi wa Jimbo la Dimani na viti
19 vya udiwani katika chaguzi hizo.
16. Mheshimiwa Spika, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, mashauri 53
ya kupinga ushindi wa Ubunge na mashauri 194 ya kupinga ushindi wa Udiwani
yalifunguliwa. Mashauri hayo yamekwishasikilizwa na hukumu kutolewa, isipokuwa
shauri moja la kupinga matokeo ya Ubunge katika Jimbo la Mbagala. Nizipongeze Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kazi kubwa waliyofanya
ya kuhakikisha kesi hizo zinaendeshwa kwa kasi na kwa weledi na hivyo kuwezesha
wananchi kuendelea kupata uwakilishi.
17. Mheshimiwa Spika, ili kuendelea kuboresha demokrasia hapa nchini,
hatuna budi kujenga jamii inayoheshimu na
kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi pamoja na kuwa na uvumilivu wa
kisiasa. Ninatoa rai kwa wadau wa siasa kote nchini kujenga utamaduni wa
masikilizano na kuendesha siasa za maendeleo badala ya siasa za malumbano; siasa
za kuunganisha watu wetu badala ya kuwagawa; na siasa za uwajibikaji badala ya
siasa za mazoea. Serikali itaendelea kulinda na kuheshimu misingi ya siasa zinazolenga
kuleta ustawi wa wananchi na zinazotanguliza maslahi ya nchi na wananchi.
MUUNGANO
18. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kudumisha muungano wetu ambao
ni tunu na mfano wa kuigwa barani Afrika na dunia nzima. Wananchi wanaendelea
kunufaika na matunda ya Muungano wetu ambao ni imara na dhabiti. Serikali zote
mbili zinafanya mashauriano kupitia Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kushughulikia masuala ya Muungano
chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, viongozi na watendaji wa sekta nyingine zisizo
za Muungano wamekuwa wakikutana mara kwa mara ili kubadilishana uzoefu na
kubaini maeneo ya ushirikiano kwa ustawi wa wananchi wa pande zote mbili. Jumla
ya vikao 13 vya sekta ambazo siyo za Muungano vilifanyika kati ya Julai 2016 na
Machi 2017.
19.
Mheshimiwa
Spika, ninapenda kutumia fursa
hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa kuendesha kwa ufanisi mkubwa kikao kilichofanyika
tarehe 13 Januari, 2017 ambapo taarifa kuhusu hoja zilizopatiwa ufumbuzi, maagizo
na maelekezo ya kufuatilia utekelezaji wa changamoto zilizobaki ilitolewa.
Serikali itaendelea kuulinda na kuuenzi Muungano wetu kwa manufaa ya wananchi
wa pande zote mbili.
HALI YA UCHUMI
20.
Mheshimiwa
Spika, mwenendo wa viashiria
vya ukuaji wa uchumi wa nchi yetu kwa mwaka 2016/2017 vinaonesha kuwa uchumi
wetu unakua na kuimarika. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa
ya Takwimu, ukuaji halisi wa Pato la Taifa ulifikia asilimia 7.0 mwaka 2016. Sekta zilizochangia kwa kiwango kikubwa
kwenye ukuaji huo ni uchimbaji madini na mawe;
usafirishaji na uhifadhi wa mizigo; habari na mawasiliano; pamoja na
shughuli za fedha na bima. Mfumuko wa Bei uliendelea kubakia katika wigo wa
tarakimu moja na kasi ya upandaji bei ilipungua kutoka wastani wa asimilia 5.6 mwaka 2015 hadi asilimia
5.2 mwaka 2016. Kwa upande mwingine,
tathmini ya hali ya Taasisi za Fedha inaonesha kuwa Benki zetu ziko salama na
zina mitaji na ukwasi wa kutosha. Aidha, taarifa za Mashirika mbalimbali ya
Kimataifa zinaonesha kwamba katika mwaka 2016 uchumi wa Taifa letu ulikua
vizuri na hivyo kutufanya kuwa miongoni mwa nchi sita (6) za Bara la Afrika,
Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa zaidi.
21.
Mheshimiwa
Spika, Serikali ya Awamu ya
Tano imeweka juhudi kubwa katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Kutokana na
juhudi hizo, makusanyo ya ndani kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
yaliongezeka kutoka wastani wa Shilingi
Bilioni 850 kwa mwezi katika mwaka 2015/2016 hadi Shilingi Trilioni 1.2 kwa mwezi katika mwaka 2016/2017. Pamoja na
kuongeza ukusanyaji wa mapato, juhudi kubwa zimefanyika kudhibiti matumizi ya
rasilimali za umma ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya rushwa, ubadhirifu, wizi
na upotevu wa fedha za umma. Mwenendo huo umeiwezesha Serikali kuanza utekelezaji
wa miradi mikubwa kwa fedha za ndani na pia utoaji huduma kwa wananchi. Serikali
itaendelea kupanua wigo wa vyanzo vya mapato ya ndani na kuongeza kasi ya
ukusanyaji mapato ili kila anayestahili kulipa kodi aweze kuilipa.
22.
Mheshimiwa
Spika, kuimarika kwa viashiria vya
uchumi wa nchi yetu katika kipindi cha mwaka mmoja tangu Serikali ya Awamu ya
Tano iingie madarakani ni dalili njema katika kujenga uchumi imara na tulivu
utakaotusaidia kuelekea katika Uchumi wa Viwanda na kufikia nchi ya kipato cha
kati ifikapo mwaka 2025. Serikali itaongeza juhudi katika kuchochea ukuaji wa sekta
za kipaumbele zenye fursa kubwa ya kukuza uchumi kwa haraka na kuondoa umaskini
kama vile Kilimo na Viwanda. Pia, itahakikisha kwamba sekta wezeshi kama vile
Nishati, Habari na Mawasiliano, Fedha na ujenzi wa miundombinu muhimu ya barabara,
bandari, reli, vivuko na viwanja vya ndege zinaimarishwa. Vilevile, Serikali
itaendelea kuhimiza utekelezaji thabiti wa miradi ya maendeleo na kuweka
mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji.
Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi
23. Mheshimiwa Spika, Serikali
imeendelea kuwezesha Wananchi kupitia Mipango na Programu mbalimbali kwa
kuelekeza nguvu zaidi kwa makundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Serikali imeweka mazingira bora kwa vikundi vya kiuchumi na vijana kujiunga na
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, SACCOS na VICOBA. Aidha, Serikali imeanzisha
majukwaa ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi katika mikoa yote na kufanya
mapitio ya Mwongozo wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake wa mwaka 2007. Mapitio
hayo yana lengo la kuboresha uendeshaji na usimamizi wa Mfuko huo ili kuwezesha
wanawake wengi zaidi kukopesheka.
24.
Mheshimiwa
Spika, tunatambua kwamba asilimia 56 ya nguvu kazi ya
Taifa ni vijana. Hivyo, Serikali inatekeleza Programu ya Kukuza Ujuzi na Stadi
za Kazi ili kuwawezesha vijana kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda
pamoja na kuinua ari ya vijana kupenda kufanya kazi. Katika mwaka 2016/2017,
Serikali inatoa mafunzo kwa vijana 9,120
katika fani mbalimbali zikiwemo stadi za kushona nguo, kutengeneza bidhaa za
ngozi, mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana kwa mfumo usio rasmi na
mafunzo ya kukuza ujuzi na stadi za kujiajiri katika fani mbalimbali. Jumla ya
vijana 1,469 wamehitimu mafunzo hayo na kupata ajira. Vijana 7,651 waliobaki
wanaendelea kupata mafunzo kupitia viwanda vya TOOKU GARMENTS, MAZAVA FABRICS,
Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), VETA na Don Bosco. Katika mwaka
2017/2018, Serikali itatoa mafunzo ya kukuza ujuzi wa kujiajiri na stadi za
kazi kwa vijana 15,350 katika fani mbalimbali.
25.
Mheshimiwa
Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana,
imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.5 kwa vikundi vya vijana 297
katika Halmashauri mbalimbali nchini. Aidha, Mamlaka za Serikali za Mitaa
kupitia mapato yake ya ndani zimetoa Shilingi bilioni 4.6 ikiwa ni mikopo yenye
masharti nafuu kwa vikundi vya vijana 2,356. Hatua hizi zimekwenda sanjari na
utengaji wa maeneo maalum yenye jumla ya ekari 85,603 kwa ajili ya shughuli za
vijana za kilimo, biashara ndogo ndogo, burudani na michezo. Katika mwaka
2017/2018, Serikali itaendelea kusimamia Halmashauri zote nchini kutenga
asilimia tano (5) ya mapato yao kwa ajili ya vijana na asilimia tano (5) kwa
wanawake.
Ajira na Mahusiano Mahali pa Kazi
26. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuratibu utekelezaji
wa juhudi za kukuza ajira nchini kama inavyoelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi
ya CCM ya mwaka 2015. Hadi kufikia Machi 2017, jumla ya ajira 418,501
zimezalishwa nchini. Kati ya ajira hizo, ajira 239,017 sawa na asilimia 57
zimezalishwa katika sekta binafsi wakati ajira 179,484 sawa na asilimia 43
zimezalishwa kutokana na shughuli za sekta ya umma ikiwemo miradi ya maendeleo.
27.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imefanya utafiti
na kubaini kuwa asilimia 58 ya migogoro ya kikazi inatokana na kutozingatiwa
kwa taratibu za kuachisha kazi. Sekta zinazoongoza kwa migogoro ya kazi ni
usafirishaji, ujenzi, ulinzi binafsi, elimu, huduma za hoteli na viwanda.
Katika kupunguza migogoro mahali pa kazi, Serikali imefanya kaguzi na kusimamia
uundwaji wa Mabaraza ya Wafanyakazi. Aidha, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi imeendelea kutimiza
wajibu wake wa kusuluhisha migogoro ambapo katika kipindi cha Julai 2016 hadi
Februari 2017, Tume imesajili jumla ya migogoro 8,832 kati ya hiyo migogoro
3,319 sawa na asilimia 37.6 ya migogoro yote iliyosajiliwa imesuluhishwa. Kati
ya migogoro hiyo iliyosuluhishwa, migogoro 1,957 ilifikia suluhu (mediation) na
migogoro 1,362 haikufikia suluhu. Aidha, migogoro 5,513 inaendelea kusuluhishwa
katika hatua mbalimbali.
Ninatoa wito kwa waajiri na waajiriwa wote nchini,
kuzingatia Sheria za Kazi na kuimarisha uhusiano mzuri kwenye maeneo ya kazi,
ili muda mwingi zaidi utumike kwenye uzalishaji mali badala ya kutatua
migogoro. Vilevile, ni muhimu sana kuimarisha kaguzi za kazi na
kuendelea kusaini mikataba ya kuunda na kusajili mabaraza ya wafanyakazi ili
kuimarisha zaidi mahusiano mahali pa kazi.
MAENDELEO YA KISEKTA
Sekta za Uzalishaji
Viwanda
28.
Mheshimiwa Spika, ili kujenga uchumi wa viwanda, Serikali
inahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.
Viwanda vinavyopewa kipaumbele ni vile vinavyotumia malighafi zinazopatikana hapa
nchini, vinavyotoa ajira kwa watu wengi na vinavyozalisha bidhaa zenye soko
hapa nchini na nje ya nchi. Katika kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu
kwenye uchumi wa viwanda, Serikali inahamasisha zaidi sekta binafsi ya hapa
nchini pamoja na mashirika ya umma kujenga viwanda. Jitihada hizo zimewezesha
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya NSSF, PPF, LAPF, GEPF, PSPF na NHIF kuanza kufufua,
kuendeleza na kujenga viwanda vipya vipatavyo 27 katika maeneo mbalimbali
nchini. Natoa pongezi kwa Bodi na Menejimenti ya Mifuko hiyo, kwa kuunga mkono
jitihada za Serikali katika ujenzi wa viwanda nchini. Aidha, ninaendelea kuyasisitiza
mashirika ya umma kuhakikisha kwamba mipango yao inaendana na utekelezaji wa
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa ambao dhima yake ni kujenga uchumi wa
viwanda.
Maliasili na Utalii
29. Mheshimiwa Spika, sekta ya utalii ni moja kati ya sekta muhimu sana katika
uchumi wa nchi yetu. Kote ulimwenguni, mafanikio ya sekta ya utalii kwa kiasi
kikubwa hutegemea miundombinu thabiti ya utalii, huduma bora na ulinzi na
usalama. Ili kuendelea kunufaika na sekta hiyo, Serikali inaboresha miundombinu
ya utalii, kupanua wigo wa vivutio vipya vya utalii na kuimarisha huduma ya
usafiri wa anga. Vilevile, Serikali inafanya juhudi kubwa za kudhibiti ujangili
na biashara haramu ya wanyamapori ambapo watuhumiwa 897 walitiwa mbaroni na kati yao watuhumiwa 282 wamefikishwa Mahakamani.
30. Mheshimiwa Spika, idadi ya watalii imeongezeka kutoka 1,137,182 mwaka 2015 hadi watalii 1,284,279 mwaka 2016 sawa na ongezeko la asilimia 12 na
kuliingizia Taifa Dola za Marekani bilioni 2. Juhudi zilizoanza za kuliimarisha
shirika letu la ndege zinalenga pia kutoa mchango mkubwa kwenye sekta ya utalii
kwa kusafirisha watalii wa ndani na kutoka nje ya nchi. Shabaha yetu ni
kuongeza idadi ya watalii wanaokuja kutembelea nchi yetu na pia mapato
yatokanayo na sekta hiyo. Nitumie fursa hii kuisihi sekta binafsi kuwekeza
zaidi kwenye miundombinu muhimu ya sekta hii zikiwemo hoteli, kuboresha huduma
na kubuni mbinu mpya za kuvutia watalii.
Kilimo
31.
Mheshimiwa
Spika, uzalishaji wa mazao ya
chakula kwa msimu wa mwaka 2015/2016 ikijumuisha mazao ya nafaka na yasiyo ya
nafaka ulifikia tani 16,172,841 ikilinganishwa
na mahitaji ya kitaifa ya tani
13,159,326. Hivyo, katika kipindi hicho nchi ilikuwa na ziada ya tani 3,013,515 za chakula. Katika msimu
wa kilimo wa mwaka 2016/2017, hali ya upatikanaji wa mvua katika Mikoa
inayopata mvua za vuli haikuwa ya kuridhisha na hivyo kusababisha ukame na
upungufu wa mavuno katika baadhi ya maeneo. Tathmini ya awali imebainisha
kwamba Halmashauri 55 zimeathirika na ukame.
32.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na hali hiyo,
Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kununua mazao ya chakula kutoka
katika maeneo yenye ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba. Aidha, wafanyabiashara waliokuwa wamehifadhi nafaka
katika maghala, walitakiwa kuzisambaza katika masoko ya ndani. Vilevile, Wakuu
wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya walielekezwa kuwahamasisha na kuwaelekeza wakulima
kupanda mbegu bora za mazao ya kilimo yanayostahimili ukame na yanayokomaa kwa
muda mfupi kwa kipindi hiki cha mvua za masika. Ili kutoa msukumo katika kazi
hiyo, kiasi cha tani 1,969 za mbegu
bora za mazao yanayostahimili ukame zilinunuliwa na Serikali na kusambazwa
katika Halmashauri zilizobainika kuathirika na ukame. Pia, wakulima wanaendelea
kuhamasishwa kuzitumia vizuri mvua zinazonyesha katika msimu huu wa masika kwa
kupanda mazao hayo yanayostahimili ukame na kukomaa mapema.
33.
Mheshimiwa
Spika, kwa kutambua umuhimu wa
sekta ya kilimo katika uchumi wetu, Serikali imeweka dhamira ya kuongeza
uzalishaji, tija na kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara. Katika mwaka
2016/2017, Serikali ilifanikisha kupatikana kwa tani 277,935 za mbolea na tani
23,333 za mbegu bora. Aidha, hadi Februari 2017, Serikali ilitoa tani 30,773 za mbolea ya ruzuku ya
kukuzia na kupandia kupitia vituo vya mauzo ya mbolea vya Kampuni ya Mbolea
Tanzania (TFC).
34. Mheshimiwa Spika, moja ya ahadi ya Serikali kwa wakulima wetu ni kupunguza kodi, tozo na
ada mbalimbali zinazochangia kupunguza faida kwa mkulima. Katika mwaka
2016/2017, Serikali ilifuta baadhi ya tozo za mazao ambazo ni kero kwa wakulima
katika mazao ya pamba, chai na kahawa. Tozo zilizofutwa kwenye zao la pamba ni mchango wa Mwenge wa Shilingi
450,000 unaotolewa na kila kiwanda cha kuchambua Pamba na ada ya vikao vya
Halmashauri za Wilaya ambayo ni shilingi 250,000. Kwa zao la chai, kodi ya moto
na uokoaji imeondolewa na katika zao la kahawa, ada ya leseni ya kusindika
kahawa ya Dola za Marekani 250 nayo pia imefutwa.
35. Mheshimiwa
Spika, Serikali pia imeboresha
Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani kwa kuanzisha utaratibu wa wazi wa ununuzi
wa mazao kupitia minada. Mathalani, katika msimu wa 2016/2017 kwenye zao la
korosho, utaratibu huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa bei ya korosho
kwa kilo kutoka shilingi 1,200 hadi shilingi 3,800, bei ambayo haijawahi
kufikiwa katika historia ya zao la korosho nchini. Aidha, Mfumo wa Stakabadhi
za Mazao Ghalani na utaratibu wa minada umeongeza ushindani na kuvutia
wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi hususan nchi ya Vietnam na nchi
nyingine kuja wenyewe kununua korosho badala ya kutegemea soko la India pekee.
Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea na uchambuzi wa kina wa kodi, tozo
na ada zilizobaki katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la
kuziondoa au kuzipunguza ili kumwezesha mkulima, mvuvi na mfagaji anufaike
zaidi na jasho lake na kuongeza mapato ya Halmashauri zetu. Kwa sasa,
tunashughulikia zao la tumbaku kwa kupitia tozo zake na pia kubaini ubadhirifu
unaoendelea kwenye ushirika huo.
Mifugo
36.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeongeza uzalishaji wa mitamba na uhimilishaji wa mifugo ili kuhamasisha ufugaji
wa kisasa na wenye tija. Mitamba 546 imezalishwa kutoka mashamba ya Serikali na
mitamba 88 kutoka NARCO na kusambazwa kwa wafugaji wadogo. Aidha, Kituo cha
Taifa cha Uhimilishaji – NAIC Usa River, Arusha kimeimarishwa na kuongeza
uzalishaji wa mbegu bora za ng’ombe hadi kufikia dozi 10,494 ikilinganishwa na dozi
8,000 zilizozalishwa na kusambazwa katika mwaka 2015/2016. Pia, ng’ombe
waliohimilishwa wameongezeka kutoka 221,390
mwaka 2015/2016 hadi ng’ombe 457,557
mwaka 2016/2017.
37.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2017/2018, Serikali
itaendelea kuimarisha kituo chetu cha kuzalisha mitamba cha Kitulo wilayani
Makete ili kukiongezea uwezo wake. Aidha, Serikali inatoa nafasi kwa mashamba
binafsi kuzalisha mitamba zaidi kama mashamba ya ASAS kule Iringa ili wafugaji
wadogo wanufaike. Serikali pia
itaendelea na zoezi la kutenga, kupima na kumilikisha wafugaji maeneo ya
ufugaji na kujenga miundombinu ya mifugo kwa kuongeza idadi ya malambo na
mabwawa katika mikoa. Hatua hizo zitasaidia kupunguza uzururaji wa mifugo na
migogoro baina ya wafugaji na wakulima na hifadhi za misitu.
Madini
38. Mheshimiwa Spika, Sekta ya madini ni muhimu kwa uchumi wetu. Serikali imetenga maeneo
zaidi kwa ajili ya wachimbaji wadogo, kuweka utaratibu mzuri zaidi wa kutoa
ruzuku pamoja na kuimarisha shughuli za ugani. Katika kipindi cha mwezi Julai 2016 hadi Februari 2017, Serikali
imetenga maeneo 11 yenye ukubwa wa hekta 38,567 kwa ajili ya wachimbaji madini wadogo. Maeneo hayo ni
Msasa na Matabe mkoani Geita, Biharamulo na Kyerwa mkoani Kagera, Itigi mkoani
Singida, D-Reef, Ibindi na Kapanda Mkoani Katavi, Ngapa mkoani Ruvuma, Kitowelo
na Namungo mkoani Lindi pamoja na Nzega mkoani Tabora.
39.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali itaimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Serikali
yatokanayo na rasilimali za madini na kuimarisha
ukaguzi wa shughuli za uzalishaji na biashara ya madini kwa migodi mikubwa, ya
kati na midogo. Aidha, Serikali itaendeleza wachimbaji wadogo na wa kati wa madini pamoja na kuhamasisha
shughuli za uongezaji thamani wa madini hayo.
Huduma za Kiuchumi
Ardhi
40.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa 2016/2017, Serikali
iliahidi kuanza ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi. Ninapenda
kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kazi ya ujenzi wa mfumo huo awamu ya kwanza
ilizinduliwa rasmi Agosti, 2016 na Mkandarasi tayari ameanza kazi. Sambamba na
zoezi hilo, Serikali inakamilisha ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Taarifa za
Ardhi. Kukamilika kwa mradi huo kutaboresha utendaji kazi, kuharakisha huduma
za utoaji hati miliki, kuongeza mapato ya Serikali na kuboresha utunzaji wa
kumbukumbu za ardhi ambapo nyaraka zote za ardhi zitakuwa katika mfumo
unganishi wa kielektroniki.
41.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia iliidhinisha
ramani za upimaji zenye jumla ya viwanja 78,771 na mashamba 239. Aidha, Serikali
imekamilisha upigaji wa picha za anga za Jiji la Dar es Salaam na inaendelea
kutatua migogoro ya matumizi ya
ardhi baina ya wakulima, wafugaji na
hifadhi katika maeneo mbalimbali nchini.
42. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kujenga Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za
Ardhi na kuboresha usimamizi wa sekta ya ardhi kwa kufanya mapitio ya Sera na
Sheria za Ardhi na kutoa elimu kwa
wananchi kuhusu sera, sheria, kanuni na miongozo ya ardhi ili kudhibiti
viashiria vya migogoro ya matumizi ya ardhi nchini. Ninatoa wito kwa
Halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba zinashughulikia migogoro ya ardhi mapema
na kuweka mazingira wezeshi ya upimaji wa ardhi katika Halmashauri zao.
Umeme
43.
Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua thabiti za kuongeza
uzalishaji, kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na kuongeza kasi ya
usambazaji umeme. Katika mwaka 2016, umeme uliozalishwa na kuingizwa katika Gridi
ya Taifa uliongezeka na kufikia Gigawatt
hours (GWh) 7,092 ikilinganishwa
na Gigawatt hours (GWh) 6,227 zilizozalishwa
mwaka 2015 sawa na ongezeko la asilimia
13.9. Vilevile, Serikali imepanua na
kuboresha njia za usafirishaji umeme kwa kukamilisha ujenzi wa njia ya umeme wa
msongo wa kilovolti 400 na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme kutoka Iringa –
Dodoma – Singida – Shinyanga.
44.
Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea kutekeleza miradi ya
kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Katika kipindi cha mwaka 2016/2017, Wakala ulikamilisha ujenzi wa vituo sita (6) vya kuongeza nguvu ya umeme kutoka msongo wa kilovolti 11 hadi kilovolti 33 katika miji ya Kigoma, Kasulu, Kibondo,
Ngara, Mbinga na Tunduru; ujenzi wa njia za kusambaza umeme zenye urefu wa kilometa 17,740 za msongo wa kilovolti 33; ujenzi wa vituo vidogo
vya kupoza na kusambaza umeme 4,100;
na ujenzi wa njia ndogo ya usambazaji umeme wenye urefu wa kilometa 10,970.
45.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali itaongeza uzalishaji,
kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme
nchini. Aidha, Serikali itaendelea na utekelezaji wa Mradi mkubwa wa Ujenzi wa
Bomba la Mafuta kutoka Kabaale (Uganda) hadi Tanga (Tanzania). Serikali pia,
itawezesha uwekaji wa mtandao wa usambazaji wa gesi asilia kwenye viwanda na
matumizi ya majumbani pamoja na uendelezaji wa mradi wa kusindika gesi asilia (Liquefied Natural Gas - LNG) mkoani
Lindi.
Barabara
46. Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi Julai
2016 hadi Februari 2017, Serikali imejenga na kukarabati jumla ya kilometa 430 za barabara
kuu sawa na asilimia
62 ya lengo la kilometa
692. Aidha, ujenzi wa
barabara za juu kwenye makutano ya TAZARA unaendelea vizuri
pamoja na maandalizi ya kuitisha zabuni za ujenzi wa Daraja Jipya la Selander
na ujenzi wa Barabara ya Dar es Salaam – Chalinze kwa kiwango cha Expressway. Vilevile, ujenzi wa barabara
za juu (Interchange) kwenye makutano
ya Barabara ya Ubungo ulizinduliwa rasmi tarehe 20 Machi, 2017. Hizi ni hatua
muhimu za kukabiliana na changamoto ya muda mrefu ya msongamano wa magari katika
Jiji la Dar es Salaam ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015.
Vivuko na Usafiri Majini
47.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha
2016/2017, Serikali ilipanga kujenga kivuko kipya cha Pangani (MV Pangani) na
kukarabati kile cha Magogoni – Kigamboni. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu
kwamba hadi kufikia Februari, 2017 ujenzi na ukarabati wa vivuko hivyo ulikuwa
umekamilika. Aidha, ununuzi wa boti ndogo za abiria kwa ajili ya vivuko vya
Kilambo – Namoto (Mtwara), Mkongo – Utete (Pwani), Pangani – Bweni (Tanga) na
Msemo – Msangamkuu (Mtwara) utakamilika katika mwaka huu wa fedha. Kwa upande
wa huduma za usafiri kwenye maziwa, Serikali inaendelea na ujenzi wa meli moja
katika Ziwa Victoria, meli mbili katika Ziwa Nyasa zitakazofanya safari kati ya
Kyela na Mbambabay pamoja na ukarabati wa meli za MV Victoria na Butiama (Ziwa
Victoria) na MV Liemba (Ziwa Tanganyika).
Bandari
48.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Uboreshaji wa Bandari
nchini kwa kufanya upanuzi na kuimarisha miundombinu ya Bandari za Dar es
Salaam, Tanga na Mtwara. Mifumo ya Ulinzi katika bandari hizo imeimarishwa
na mashine za kisasa za kukagua mizigo zimefungwa. Kutokana na jitihada hizo,
tumeanza kuona mwelekeo mzuri wa kuimarika ufanisi wa kiutendaji hususan katika
Bandari ya Dar es Salaam. Tutaendelea kufanya maboresho zaidi ili Bandari ya
Dar es Salaam iwe chaguo namba moja katika usafirishaji wa mizigo ndani na nje
ya nchi yetu.
Reli
49.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali iliendelea
kutekeleza miradi ya uboreshaji wa miundombinu ya Reli ya Kati ili kuongeza
uwezo wa reli hiyo kutoa huduma za uchukuzi nchini na nchi jirani zinazotumia
bandari zetu. Awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli mpya ya kati kutoka Dar es
Salaam hadi Mwanza kwa kiwango cha standard
gauge imeanza kutekelezwa kwa kusaini mkataba wa ujenzi wa kipande cha reli
ya Dar es Salaam - Morogoro (kilometa
205). Taratibu za kuwapata makandarasi wa ujenzi wa reli kutoka Morogoro –
Makutupora (kilometa 336),
Makutupora- Tabora (kilometa 294),
Tabora- Isaka (kilometa 133) na Isaka- Mwanza (kilometa 254) zinaendelea.
Usafiri wa anga
50. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2016/2017, Serikali imetekeleza kwa dhati azma ya kuimarisha Kampuni ya
Ndege Tanzania (ATCL). Katika kipindi hicho, ndege mbili (2) aina ya Dash 8 –
Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja zilinunuliwa na kuanza kutoa
huduma mwezi Oktoba, 2016. Aidha, mwishoni mwa mwaka 2016, Serikali iliingia
mkataba wa ununuzi wa ndege nyingine nne (4). Kati ya hizo, ndege moja ya aina
ya Dash 8 - Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 76 inatarajiwa kuwasili mwezi
Julai, 2017. Ndege nyingine mbili (2) aina ya CS300 zenye uwezo wa kubeba
abiria 127 kila moja zinatarajiwa kuwasili mwezi Juni, 2018 na ndege kubwa moja
ya masafa marefu aina ya Boeing 787 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262
inatarajiwa kuwasili mwezi Julai, 2018.
51. Mheshimiwa
Spika, kukamilika kwa ununuzi
wa ndege hizi kutaisaidia ATCL kuongeza safari za ndani na nje ya nchi na hivyo
kuchangia katika jitihada za kuongeza watalii wanaokuja nchini kutembelea
vivutio vyetu na kuimarisha usafiri wa anga hapa nchini. Aidha, ATCL imeanzisha
safari za kuja Dodoma na hivyo kuongeza uhakika wa usafiri wakati huu ambapo
Serikali inahamia Dodoma. Wigo wa upanuzi kwa viwanja vyote nchini unaendelea
na sasa hivi tunakamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege.
Mawasiliano
52. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, baadhi ya kazi zilizofanyika
kwenye sekta ya mawasiliano ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa
wa Mawasiliano; kutekeleza Mradi
wa Anuani za Makazi na Postikadi; na kuanzisha huduma ya kituo cha Jamii Centre kitakachorahisisha utoaji
wa huduma muhimu katika kituo kimoja. Huduma hizo ni kulipa pensheni, ankara na
huduma za kibenki. Aidha, Sekta ya Mawasiliano inatekeleza Programu ya
Miundombinu ya Kikanda ambayo inahusisha Mradi wa Shule Mtandao (e-school),
Mradi wa Video Conference ambao unahusisha ununuzi, usimikaji na
ufungaji wa vifaa vya TEHAMA katika Mikoa 26 na Taasisi za Serikali.
53.
Mheshimiwa
Spika, Serikali pia inatekeleza
mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Mawasiliano Vijijini kwa kushirikiana na
Kampuni ya Viettel ya Vietnam.
Mradi huu unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu
2015-2017. Viettel wamekwishafikisha
miundombinu ya mtandao wa intaneti kwenye shule 417, Ofisi za
Halmashauri za Wilaya 123, Hospitali za Wilaya 74, Vituo vya Polisi vya Wilaya
131 na Ofisi za Posta 68.
54. Mheshimiwa Spika, Serikali
imekamilisha ujenzi wa kituo cha kuhifadhi taarifa na mifumo ya Serikali (Government Data Centre). Lengo ni
kuongeza na kuimarisha usalama wa mifumo na taarifa unaoenda sambamba na
uhakika wa upatikanaji wa taarifa za Serikali katika kutekeleza majukumu yake
ya kila siku. Pamoja na ujenzi wa vituo hivyo, matumizi ya TEHAMA yameongezeka na
hivyo kuziwezesha taasisi za Serikali kutoa mchango mkubwa kwenye uboreshaji na
utoaji wa huduma, kuongeza mapato na kuokoa gharama mbalimbali.
Sekta ya Huduma za Jamii
Elimu
55. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kujenga uwezo wa walimu wa
shule za msingi kwa kuwapa mafunzo hasa katika ufundishaji wa stadi za Kusoma,
Kuandika na Kuhesabu (KKK). Jumla ya walimu 22,995 wa shule za msingi na walimu
519 wanaofundisha elimu maalum kwa wanafunzi wasioona na wenye ulemavu wa kusikia
wamepewa mafunzo hayo. Lengo ni kuhakikisha kila mwanafunzi anayemaliza darasa
la saba anajua kusoma na kuandika.
56.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2016/2017,
Serikali iliendelea na mpango wa kutoa Elimumsingi bila malipo. Tangu
utekelezaji wa mpango huo uanze, Serikali imekuwa ikipeleka wastani wa Shilingi bilioni 18.77 kila mwezi,
ambapo shule za msingi 16,088 na shule za sekondari 3,602 zimenufaika na mpango
huo. Mpango huo umeleta manufaa kwa Watanzania wengi wa kipato cha chini na cha
kati na umeongeza uandikishaji wa wanafunzi kwenye shule za Msingi na
Sekondari. Kufuatia ongezeko hilo, tulijikuta tukilazimika kupambana na upungufu
wa madawati, jambo ambalo liliifanya Serikali ianzishe kampeni maalum ya kumtoa
sakafuni mtoto wa Kitanzania. Hivi sasa madawati sio tatizo tena kwenye shule
nyingi nchini. Nitumie fursa hii kutoa pongezi kwa Watanzania wote
walioshirikiana na Serikali katika kutatua changamoto ya upungufu wa madawati. Natoa pongezi kwa taasisi binafsi, watu
binafsi na Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao yote.
57. Mheshimiwa
Spika, uchumi wa viwanda kwa kiasi kikubwa unahitaji rasilimaliwatu
yenye weledi hasa katika masomo ya hisabati na sayansi. Kama zilivyo nchi
nyingine Barani Afrika, Tanzania inakabiliwa na changamoto ya wanafunzi kutopenda
kusoma masomo ya hisabati na sayansi na hivyo kuchangia katika ufaulu duni
kwenye masomo hayo. Ni dhahiri kuwa watoto wetu wasipoweka bidii katika masomo
ya hisabati na sayansi viwanda vyetu vitalazimika kutegemea wataalamu kutoka
nje ya nchi jambo litakalowafanya Watanzania kuwa watazamaji.
58. Mheshimiwa
Spika, ili kukabiliana na
changamoto hiyo, Serikali imefanya juhudi za kuhamasisha wanafunzi kupenda
masomo ya sayansi katika ngazi zote za shule. Aidha, Serikali inaendelea na
Mpango wa Ujenzi wa Maabara katika shule za sekondari na vyuo vikuu pamoja na
ununuzi wa vifaa. Katika mwaka 2016/2017, Serikali imenunua vifaa vya maabara
kwa ajili ya shule 1,625 za
sekondari zilizokamilisha ujenzi wa maabara na
usambazaji wa vifaa umeanza mwezi Machi, 2017 katika Mkoa wa Dar es Salaam na
kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Aprili, 2017 kwa nchi
nzima. Aidha, Serikali inatoa mafunzo
kwa walimu 5,920 wanaosoma
Stashahada maalum ya Sayansi, Hisabati na TEHAMA.
59. Mheshimiwa Spika, Serikali inakusudia kuimarisha ufundishaji wa masomo
ya TEHAMA kwa shule za Sekondari. Serikali inaendelea na mpango wake wa kujenga
maabara za kompyuta ili wanafunzi wawe na uelewa wa TEHAMA. Utekelezaji wake
utafanyika hatua kwa hatua.
60.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imetoa vibali
vya ajira kwa walimu wa Hisabati na Sayansi 4,129. Natoa wito kwa wazazi wenzangu
kuhamasisha watoto wetu kupenda masomo ya Hisabati na Sayansi. Naagiza Wizara
ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na TAMISEMI na wadau wengine waandae
Mkakati Maalum wa kuhamasisha na kuwavutia wanafunzi kusoma masomo ya Hisabati
na Sayansi. Mkakati huo pia uwezeshe upatikanaji wa walimu watakaofundisha
masomo ya Hisabati na Sayansi katika shule za msingi na sekondari kwa kipindi
kifupi bila kuathiri ubora wa ufundishaji.
61.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imeendelea na
ukarabati na ujenzi wa miundombinu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha
Sayansi na Teknolojia Mbeya, Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa na Taasisi ya
Teknolojia Dar es Salaam. Ujenzi wa majengo 20 ya mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi
3,840 umekamilika. Vilevile, Serikali inaimarisha miundombinu katika vyuo vya
ufundi vya Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam, Chuo cha Sayansi na
Teknolojia cha Mbeya na Chuo cha Ufundi Arusha kwa lengo la kuimarisha mafunzo
ya Ufundi na Sayansi nchini. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaimarisha Vyuo
vya Elimu ya Juu ili kuwezesha upatikanaji wa wataalam mahiri katika nyanja
mbalimbali hususan Sayansi na Teknolojia.
Maji
62. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu
wa kusogeza huduma za maji karibu zaidi na wananchi ili wasitumie muda mwingi
kutafuta maji badala yake wajikite katika shughuli za uzalishaji mali. Ili
kutimiza azma hiyo, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maji mijini na
vijijini ikiwemo miradi ya vijiji 10 chini ya Programu ya
Maendeleo ya Sekta ya Maji. Kati ya mwezi Julai na
Desemba 2016, miradi 90 ya maji vijijini ilikamilika na kufanya idadi ya miradi iliyokamilika kufikia 1,301 kati ya miradi 1,810
iliyolengwa. Miradi 509 iliyobaki
ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na yote inatarajiwa kukamilika kabla
ya mwezi Juni, 2017.
63.
Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji vijijini katika Halmashauri zote nchini ukiwemo
mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe unaolenga kuhudumia wananchi zaidi ya 456,000 katika vijiji 38 kwenye miji ya Same, Mwanga na Korogwe Vijijini. Ili
utoaji wa huduma ya maji uwe endelevu, wananchi waendelee kuelimishwa kuhusu
umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji, uvunaji wa maji ya mvua na matumizi bora ya
maji. Nitumie fursa hii kuwakumbusha watendaji katika Halmashauri zote
kusimamia kikamilifu sheria inayokataza shughuli za kibinadamu katika vyanzo
vya maji.
Afya
64.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imeendelea kuhamasisha
wananchi kujikinga dhidi ya magonjwa ikiwemo kuhimiza lishe bora. Aidha, Serikali
inaboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini kwa kujenga vituo vya kutolea
huduma za afya na tiba pamoja na kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba. Bajeti
ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016 hadi Shilingi bilioni 251 mwaka
2016/2017. Vilevile, Serikali imeanzisha utaratibu wa kununua dawa na vifaa
tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji kwa lengo la kupunguza gharama.
Serikali pia imeanzisha maduka ya dawa yanayouza bidhaa zake kwa bei nafuu kwa
wananchi katika hospitali za mikoa ambapo hadi sasa maduka manane (8)
yameanzishwa, na ujenzi wa maduka mengine katika mikoa iliyobakia unaendelea.
65.
Mheshimiwa
Spika, Serikali pia inaimarisha
huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto nchini kwa kutekeleza Mpango Mkakati wa
Kupunguza Vifo Vitokanavyo na Uzazi na Vifo vya Watoto wa mwaka 2016-2020.
Lengo ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020, asilimia 50 ya vituo vya Afya
nchini vinakuwa na uwezo wa kutoa huduma za dharura kwa matatizo ya uzazi
ikiwemo upasuaji na huduma za watoto wachanga.
Hadi sasa, vituo vya afya 159 vinatoa huduma za upasuaji ambapo vituo
106 ni vya Serikali.
Vilevile, Serikali imeimarisha utoaji wa huduma za
kinga na hivyo kuchangia kutokomezwa kwa ugonjwa wa Polio hapa nchini na
hatimaye nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi zilizopatiwa hati ya kutokomeza
ugonjwa huo. Katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kuimarisha huduma za
afya nchini kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Afya ya
Msingi na kuimarisha huduma za kinga ili kupunguza vifo vya watoto na akina
mama pamoja na makundi mengine. Naomba nitoe wito
kwa wote Watanzania wajiunge kwa wingi na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili
Serikali iweze kuwachangia kupitia mfumo huo.
BUNGE
66.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa. Katika mwaka 2016/2017,
Ofisi ya Bunge iliratibu na kusimamia
shughuli za Mikutano mitatu ya Bunge ambapo maswali 1,054 ya kawaida, nyongeza na ya papo kwa papo kwa Waziri
Mkuu yaliulizwa. Miswada kumi (10)
ya Sheria ilijadiliwa na kupitishwa na Bunge. Aidha, Bunge liliratibu na
kusimamia shughuli za Mikutano ya Kamati za Kudumu za Bunge, kutoa huduma za Hansard,
utafiti, utawala na kutoa mafunzo kwa Waheshimiwa Wabunge na Watumishi wa
Ofisi ya Bunge. Ofisi ya Bunge pia ilisimamia kazi ya ukarabati wa jengo la
Bunge pamoja na kuratibu ujenzi wa Ofisi za Waheshimiwa Wabunge. Katika mwaka 2017/2018,
Serikali itaendelea kuliwezesha Bunge kutekeleza majukumu yake ya Kikatiba kama
kawaida.
MAHAKAMA
67. Mheshimiwa Spika, utendaji wa mhimili
wa Mahakama nchini umezidi kuimarika. Katika mwaka 2016/2017, Mahakama imesikiliza
na kukamilisha mashauri 279,331 kati
ya 335,962 katika ngazi zote za
Mahakama sawa na asilimia 83.1 ya
mashauri yote. Pamoja na kazi kubwa ya kusikiliza mashauri, Mahakama imesogeza
huduma zake karibu na wananchi kwa kukamilisha ukarabati na ujenzi wa majengo
ya Mahakama Kuu katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam. Pia, kazi za ukarabati
wa Mahakama Kuu katika Mkoa wa Mbeya inaendelea na ujenzi wa Mahakama ya Wilaya
na Mahakama ya Mwanzo Kibaha Mkoa wa Pwani umekamilika na kuzinduliwa.
Mheshimiwa Spika, ni matarajio yangu
kwamba, katika mwaka 2017/2018, Mahakama itaendelea kutekeleza majukumu yake
kwa ufanisi zaidi ili kupunguza mlundikano wa mashauri yaliyopo mahakamani.
Hata hivyo, ili Mahakama ifanye kazi zake vizuri, shughuli za upelelezi wa kesi
na uendeshaji wa mashtaka zinatakiwa pia kuimarishwa zaidi. Serikali itafanya
kila liwezekanalo kuimarisha taasisi zote zinazohusika katika mlolongo wa
utoaji haki ili wananchi wapate haki zao kwa wakati.
MASUALA MTAMBUKA
Mfumo wa Ufuatiliaji wa
Shughuli za Serikali
68.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017,
Serikali iliahidi kuanzisha Mfumo wa Wazi wa Kielektroniki wa kufuatilia
uwajibikaji na utendaji Serikalini. Mfumo huo utasaidia kuongeza ufanisi katika
uratibu wa shughuli za Serikali kwa kuwawezesha Viongozi kutoa maelekezo na
kufuatilia utekelezaji wake. Aidha, Mfumo huo utasaidia ufuatiliaji wa
utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ahadi na Maagizo ya Mheshimiwa
Rais na Mpango wa Taifa wa Maendeleo. Napenda kulialifu Bunge lako Tukufu
kwamba, Mfumo huo umekamilika, kuzinduliwa rasmi na mafunzo kutolewa kwa
wataalamu katika Wizara zote. Mfumo huo pamoja na mambo mengine utaongeza kasi
ya utoaji taarifa za utekelezaji wa kazi za Serikali kwa wakati na pia kuongeza
uwajibikaji kwa watumishi wa Umma. Wizara na Taasisi zote za Serikali zinatakiwa
kuutumia Mfumo huo kikamilifu ili kurahisisha ufuatiliaji wa utekelezaji wa
kazi za Serikali na kusaidia viongozi kutatua vikwazo pale vinapojitokeza.
Vita dhidi ya Rushwa
69.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapambana na rushwa kwa nguvu zake zote na haina mzaha wala uvumilivu na vitendo vya rushwa. Hatua zilizochukuliwa kupambana na
rushwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani Novemba, 2015
zimetambulika hata na Mashirika ya Kimataifa yanayojishughulisha na tafiti kuhusu
masuala ya rushwa Duniani. Taarifa ya Shirika la Transparency
International kwenye utafiti wake kuhusu mtazamo wa rushwa mwaka 2016 imeonesha kuwa
viwango vya rushwa vinaendelea kupungua hapa nchini.
70. Mheshimiwa Spika, katika Mwaka 2016/2017, Serikali kupitia
TAKUKURU imefanya uchunguzi wa majalada 306 ya tuhuma za rushwa na kupata kibali cha
Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini kuendelea na mashtaka kwa majalada 104. Katika
kipindi hicho, TAKUKURU iliendesha kesi 674 zikiwemo kesi mpya 182, ambapo
katika kesi 97 watuhumiwa walipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo au kulipa
faini. Kesi 407 zinaendelea kusikilizwa mahakamani. Kutokana na operesheni
zilizofanywa na TAKUKURU, kiasi cha Shilingi
bilioni 9.75 ziliokolewa. Katika Mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea na
mapambano yake dhidi ya rushwa hususan katika eneo la ukusanyaji mapato ya
Serikali, kudhibiti matumizi ya fedha za umma, malipo hewa, matumizi mabaya ya
fedha za ushirika na kuimarisha ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi ya maendeleo.
Vita dhidi ya UKIMWI
71.
Mheshimiwa Spika, mapambano dhidi
ya UKIMWI yamekuwa yakitegemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa rasilimali
fedha kutoka kwa Wadau wa Maendeleo. Ninapenda kulijulisha Bunge lako Tukufu
kuwa, Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI ulioanzishwa na Serikali miaka miwili
iliyopita, ulizinduliwa tarehe 01 Desemba, 2016 ambapo kupitia harambee iliyofanyika
kwa ajili ya kuchangia Mfuko huo, shilingi milioni 347 zilipatikana kama ahadi.
Vilevile, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 5.6 kwa ajili ya Mfuko wa
UKIMWI.
72.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inaendelea kutoa huduma kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) ambapo
hadi Desemba, 2016 WAVIU 839,574 sawa na asilimia 63 ya WAVIU wote, walikuwa
wamepatiwa dawa. Juhudi zinaendelea kufanyika ili kuwahamasisha WAVIU
kujitokeza na kuingia kwenye Mpango wa Tiba ya Kufubaza Athari za UKIMWI. Aidha,
Serikali imekamilisha uandaaji wa miongozo
minne ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI ikijumuisha Mpango Kazi wa Kinga, Mkakati wa
Kondomu, Mkakati wa Uwekezaji na Mpango kazi wa jinsia.
73.
Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka 2017/2018,
itaimarisha uratibu wa afua za UKIMWI kwa wadau wote wa sekta ya umma na
binafsi na kupitia mifumo ya uratibu iliyoanzishwa. Serikali kwa kushirikiana
na wadau pia itazijengea uwezo Kamati zilizo katika ngazi ya jamii hususan vijiji
na kata ili kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa ya kupunguza na kumaliza
UKIMWI ifikapo mwaka 2030 kwa kutumia mfumo ulio katika jamii. Vilevile,
Serikali itakamilisha utafiti wa nne wa kubainisha viwango vya maambukizo ya
UKIMWI nchini na kuboresha ushiriki wa sekta binafsi ili kuleta ufanisi katika
kuchangia mwitikio wa Taifa dhidi ya UKIMWI.
Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu
74. Mheshimiwa Spika, katika
2016/2017, Serikali imeendelea kutoa huduma pamoja na kuongeza upatikanaji wa
haki na fursa kwa watu wenye ulemavu. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali imewaagiza
Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa Kamati za Watu wenye Ulemavu zinaanzishwa
katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Mitaa na Vijiji. Aidha, Serikali imeanzisha kampeni
za kupinga unyanyapaa na vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino
katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Geita, Simiyu, Kagera, Tabora, Kigoma, Mara,
Mbeya, Katavi na Rukwa na kampeni hiyo itaendelea nchi nzima.
75.
Mheshimiwa Spika,
Serikali pia inahakikisha kwamba watumiaji wa
lugha ya alama wanapata haki ya kupata habari na vituo vyote vya televisheni
vimeelekezwa kutumia wakalimani wa lugha ya alama. Napenda kuvikumbusha Vituo
vya Televisheni kuweka wakalimani wa lugha katika vituo vyao. Katika mwaka
2017/2018, Serikali itaendelea kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni
pamoja na kutoa vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye ulemavu shuleni na vifaa vya
kufundishia.
Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya
76. Mheshimiwa spika, dawa za kulevya zinaathiri maisha ya vijana wetu wengi na hivyo kuzima
ndoto za maisha yao na kupunguza nguvu kazi ya Taifa. Ili kupambana na janga
hilo, katika mwaka 2016/2017, Bunge lako Tukufu lilifanya marekebisho ya Sheria
ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015. Marekebisho hayo
yameipa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nguvu ya kukamata,
kupeleleza na kushitaki watuhumiwa wanaohusika na biashara ya dawa za kulevya.
Aidha, hivi karibuni Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya uteuzi
wa Watendaji Wakuu watakaosimamia Mamlaka hiyo.
77. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Januari, 2017
watuhumiwa 11,303 walikamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na uzalishaji,
usambazaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya katika sehemu mbalimbali
nchini. Kati ya watuhumiwa hao, watu 9,811,
walikutwa na kesi za kujibu ambapo 9,174 wametiwa hatiani, 238 hawakukutwa na
hatia na wengine 478 upelelezi wa kesi zao unaendelea. Pia alisema tangu Tume
mpya iundwe Februari mwaka huu, jumla ya watuhumiwa 79 wametiwa mbaroni na
uchunguzi wa kesi zao unaendelea. Ni imani yangu kuwa, Mamlaka
ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya itaendeleza kwa kasi zaidi juhudi za kupambana
na uingizaji, uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini.
Watanzania wana imani kubwa na Mamlaka hii na ninaomba wote tuipe ushirikiano wakati
wote kwani vita hii ni kubwa na ni ya Kitaifa! Aidha, nawasihi wazazi wenzangu,
tuwe karibu na vijana wetu na kufuatilia nyendo zao ili wasiingie kwenye mtego huu
wa dawa za kulevya.
Uratibu wa Maafa
78.
Mheshimiwa Spika, Serikali wakati wote inahakikisha kuwa nchi ipo katika hali ya utayari
wa kukabiliana na maafa na pia kutoa misaada ya kibinadamu ikiwemo huduma za
matibabu, ushauri wa kisaikolojia, na vifaa
pale maafa yanapotokea. Serikali
imejenga vituo vipya 20 vya upimaji wa hali ya hewa katika Halmashauri 11 za Tarime,
Nyamagana, Muleba, Longido, Geita, Maswa, Kigoma, Sikonge, Kongwa, Serengeti,
na Kahama. Kuwepo kwa vituo hivyo kutaongeza ufanisi
katika upatikanaji wa taarifa za tahadhari hasa kwa majanga ya mafuriko na
ukame.
79.
Mheshimiwa Spika, kufuatia tetemeko la ardhi
lililotokea katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa mwezi Septemba 2016, Serikali kwa
kushirikiana na wadau imechukua hatua za kushughulikia athari zilizotokana na
tetemeko hilo. Huduma za afya na tiba na za kibinadamu za chakula na malazi zilitolewa
kwa walioathirika. Vilevile, Serikali ilirejesha hali ya miundombinu
iliyobomoka, yakiwemo majengo ya Serikali na Taasisi za Umma 686, Kituo cha
wazee Kilima pamoja na kutoa maturubai 6,237, mahema 367, mabati 7,300 na mifuko
ya saruji 1,825 kwa walioathirika. Serikali inaendelea na ujenzi wa Shule za
Ihungo, Nyakato na Omumwani pamoja na ukarabati wa Kituo cha afya Kabyaile
Ishozi. Ninapenda kuwashukuru sana wananchi wote na wadau waliotoa michango yao
kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi.
HABARI NA MICHEZO
Habari
80.
Mheshimiwa
Spika, Bunge lako Tukufu lilipitisha Sheria ya Huduma za
Habari Na. 12 ya mwaka 2016 ambayo ni muhimu katika kuimarisha usimamizi na uwajibikaji
katika Sekta ya Habari nchini. Kanuni za Sheria hiyo zimeandaliwa na tayari
zimeanza kutumika. Natoa wito kwa wadau wa sekta ya habari kuzingatia sheria na
kanuni hizo ili kuimarisha weledi katika tasnia ya habari. Aidha, nashauri
wadau wa habari kujikita zaidi katika kuandika na kutangaza habari za masuala
ya maendeleo na uchumi ili kuwasaidia wananchi kutekeleza azma ya Serikali ya
Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na kuboresha huduma za kijamii.
Maendeleo ya
Michezo
81.
Mheshimiwa Spika,
tumeanza kuona dalili nzuri za kuimarika kwa shughuli za michezo hapa
nchini. Mathalan, timu ya Mpira wa Miguu ya Serengeti
Boys imefuzu kushiriki Mashindano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika
kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 yatakayofanyika Gabon, Mei 2017. Napenda
nimshukuru sana Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan ambaye amewaaga na
kuwakabidhi bendera ya Taifa tayari kwenda kushiriki vita hiyo. Nawaomba
Watanzania wote tuungane pamoja kuiombea na kuiunga mkono timu yetu kwa
michango ya hali na mali ili kuiwezesha kushiriki kikamilifu. Kwa
upande wa riadha, Mtanzania mwenzetu Alphonce Simbu alipata medali katika mbio
za marathon huko Mumbai nchini India. Aidha, mwezi Septemba 2016, Timu ya Taifa
ya Mpira wa Miguu ya Wanawake Tanzania (Twiga Stars) iliweka historia ya kuwa
timu ya kwanza kutwaa taji la CECAFA. Ninatoa pongezi kwa wale wote
walioliletea Taifa sifa kupitia michezo. Naziombea dua ili ziweze kushiriki
michuano ya kimataifa.
82.
Mheshimiwa Spika, michezo ni sekta muhimu
katika kuongeza ajira, kuimarisha afya, kukuza uchumi, kuimarisha umoja wa
Kitaifa na kuitangaza nchi Kimataifa. Nchi nyingi zilizofanikiwa kimichezo
ziliwekeza zaidi kujenga vipaji vya vijana katika michezo. Natoa wito kwa TFF ihakikishe
kuwa vijana wa Timu ya Serengeti Boys wanawekewa Mpango Endelevu wa Kukuza
Vipaji Vyao na kutunzwa vyema ili waweze kuiwakilisha nchi yetu katika
mashindano mengine ya kimataifa. Aidha, vyama vingine vya michezo vitoe msukumo
mkubwa kwenye kuwekeza zaidi kwa vijana wa shule za msingi na sekondari kwani
hao ndio watakuwa wawakilishi wetu katika miaka ijayo. Na mwaka huu, michezo ya
shule za msingi na sekondari itarejea na kufanyika mkoani Mwanza kama
ilivyotangazwa mwaka jana. Nazisihi wizara husika za TAMISEMI na Wizara ya
Elimu zianze maandalizi mapema na kuandaa mpango huo na kutoa taarifa timu hizo
ziweze kujiandaa na kushindana ili tupate wachezaji imara wa kushiriki michuano
hiyo.
ULINZI NA
USALAMA
83. Mheshimiwa Spika, hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari kutokana na kazi kubwa na
nzuri inayofanywa na vikosi vyetu vya ulinzi na usalama katika kulinda mipaka ya
nchi yetu. Serikali imeendelea kuimarisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa
kulipatia zana na vifaa vya kivita na kukamilisha mradi mkubwa wa ujenzi wa
nyumba 6,064 za makazi ya askari ulioanza mwaka 2013/2014. Kwa upande mwingine,
Serikali kupitia Jeshi la Magereza inakamilisha ujenzi wa nyumba zilizojengwa
kwa njia ya ubunifu katika baadhi ya Magereza ikiwemo ujenzi unaoendelea katika
Gereza la Ukonga wa ghorofa 12 zenye uwezo wa kuishi askari na familia 320.
84. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha usalama wa raia na
mali zao kwa kufanya operesheni za
kuzuia uhalifu nchini, kufanya upelelezi wa kesi kwa kasi ili kupunguza
mlundikano wa kesi zilizopo mahakamani,
na kusimamia sheria za barabarani ili kupunguza ajali zinazoleta madhara
kwa wananchi. Aidha, Serikali itaendelea kutoa mafunzo kwa askari na maafisa wa
jeshi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kupambana na vitendo vya
rushwa na kupambana na biashara ya dawa za kulevya.
MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
85.
Mheshimiwa Spika, kudumisha uhusiano mzuri
na mataifa mengine duniani pamoja na mashirika ya kimataifa ni moja kati ya
Misingi ya Sera yetu ya Mambo ya Nje. Tumeendelea kuimarisha ujirani mwema
baina yetu na nchi jirani, nchi marafiki pamoja na mashirika ya kikanda na
kimataifa, jitihada ambazo zimetuwezesha kuvutia mitaji mikubwa ya uwekezaji,
utalii pamoja na kupanua fursa za kibiashara. Katika mwaka 2016/2017, Serikali
imefungua Balozi mpya sita (6) katika nchi za
Algeria, Israel, Korea Kusini, Sudan, Qatar na Uturuki. Balozi hizo zina kazi
kubwa ya kuendeleza juhudi za kuitangaza Tanzania kama nchi yenye vivutio vingi
vya utalii na rasilimali zinazoweza kutumika kuvuta uwekezaji kutoka mataifa
hayo ikizingatiwa utulivu na amani iliyopo. Serikali itaendelea kulinda na
kutetea maslahi ya Tanzania nje ya nchi na kuweka mikakati ya kunufaika na
nafasi ya nchi yetu kihistoria. Hivyo, ninatoa
wito kwa mabalozi wetu wote waendelee kuitangaza nchi yetu kama eneo mwafaka
lenye fursa nyingi za utalii, uwekezaji na biashara.
HITIMISHO
86. Mheshimiwa Spika, ili kujenga uchumi wa viwanda tunahitaji nidhamu ya
kazi, ubunifu, elimu na matumizi makubwa ya sayansi na teknolojia. Vilevile,
tunahitaji kuimarisha sekta binafsi, miundombinu ya huduma za kiuchumi na jamii
na kuondoa urasimu usio wa lazima. Nafarijika kwamba misingi tunayoendelea kujenga
katika kutekeleza azma hiyo imeanza kuzaa matunda kama nilivyoeleza awali. Ili
kufanya mafanikio hayo yawe endelevu, naomba nihitimishe hotuba yangu kwa
kusisitiza mambo makuu yafuatayo:-
(i)
Mosi, ustawi
wa nchi yetu na mafanikio ya mipango yetu ya maendeleo vinategemea amani na
utulivu. Hivyo, kila mmoja wetu aweke nadhiri ya kuendelea kuilinda na kuienzi amani
ya nchi yetu ili mipango yetu iweze kufanikiwa. Tunalo jukumu la kuhimiza amani
ili tufanye kazi zetu kwenye mazingira ya amani na utulivu.
(ii)
Pili, jukumu
la kujenga uchumi wa nchi yetu ni wajibu wa kila mwananchi. Njia pekee ya
kuijenga nchi yetu ni kufanya kazi kwa bidii, kulipa kodi kwa hiari na kufichua
wakwepa kodi wote na wala rushwa.
(iii)
Tatu, ujenzi
wa uchumi wa viwanda unahitaji wananchi wenye afya njema na maarifa ya kufanya
kazi na ubunifu. Tujenge utamaduni wa
kupima afya zetu na kufanya mazoezi ya viungo ili kuepuka magonjwa yasiyo ya
kuambukiza ambayo yanapoteza nguvu kazi kubwa ya Taifa;
(iv)
Nne, rasilimali
tulizonazo ipo siku zitaisha. Hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuzitumia kwa
uangalifu ili zitufae sisi na vizazi vijavyo.
Tuepuke matumizi mabaya ya rasilimali zetu kama vile maji, madini na
misitu ili zinufaishe kizazi hiki na vizazi vijavyo;
(v)
Tano, tuongeze
nidhamu na uwajibikaji katika kila jambo la maendeleo tunalolifanya na
kuzingatia matumizi ya muda. Tamaduni na mila zinazohamasisha uvivu na uzembe
ni lazima tuzipige vita kwa nguvu zetu zote; na
(vi)
Mwisho, dawa
za kulevya ni janga kubwa linaloitafuna kwa kasi nguvukazi ya nchi yetu.
Tunahitaji ushiriki wa kila mmoja katika vita hii kwa kufichua mtandao wa
wahusika wa dawa za kulevya. Ahadi yetu ni kuwapa
ushirikiano na kuchukua hatua kali dhidi ya wote waliohusika.
MAKADIRIO YA MAPATO
NA MATUMIZI YA FEDHA
ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2017/2018
87.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2017/2018,
Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake inaliomba Bunge lako Tukufu
liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni
Mia Moja Sabini na Moja; Milioni Mia Sita Sitini na Nne, na Hamsini na Tano
Elfu (Sh.171,664,055,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Sabini na
Nne, Milioni Mia Sita Arobaini na Tatu, na Mia Tatu Thelathini na Tisa Elfu
(Sh.74,643,339,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Tisini na Saba, Milioni
Ishirini, na Mia Saba na Kumi na Sita Elfu (Sh.97,020,716,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
Vilevile, ninaliomba Bunge lako Tukufu
liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni
Mia Moja Ishirini na Moja, Milioni Mia sita Hamsini na Mbili na Mia Mbili
Sitini na Mbili Elfu (Sh.121,652,262,000) kwa ajili ya Mfuko wa
Bunge. Kati ya fedha hizo, Shilingi
Bilioni Mia Moja Kumi na Nne, Milioni Mia Nne Hamsini na Mbili, na Mia Mbili
Sitini na Mbili Elfu (Sh.114,452,262,000) ni kwa ajili ya Matumizi ya
Kawaida na Shilingi Bilioni Saba na
Milioni Mia Mbili (Sh.7,200,000,000) ni kwa ajili ya Matumizi
ya Maendeleo.
88.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment