Mwezeshaji wa Kongamano hilo, Prof. Honest Ngowi (aliyesimama) akizungumza katika Kongamano la Mwaka la Uwezeshaji. Wengine picha ni watoa mada mbalimbali walioshiriki katika Kongamano hilo.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wito umetolewa kwa Watanzania hasa kwa wadau wanaojihusisha na uwezeshaji wananchi kiuchumi kubadili mitazamo juu ya namna sahihi ya kuwawezesha wananchi hao katika kutimiza lengo la serikali la kuwainua wananchi kiuchumi ili kuimarisha kipato na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi nchini.
Wakizungumza katika Kongamano la Mwaka la Uwezeshaji linalofanyika mkoani Dodoma wadau hao wamesema kuwa kuna ulazima wa wadau hao kujua mahitaji sahihi ya wananchi wanaohitaji huduma za uwezeshaji wa kiuchumi kwa kuwa kila kundi lina mahitaji yake.
Mwezeshaji wa Kongamano hilo, Prof. Honest Ngowi amesema kuwa ukuaji wa uchumi wa nchi yoyote unazingatia mahitaji maalumu ya kila sekta ya kiuchumi na kutolea mfano kuwa wakulima nchini hawahitaji rasilimali fedha pekee ili kuongeza tija katika kilimo chao bali wanahitaji masoko ya uhakika ya mazao yao.
“Uzoefu kutoka kwa watekelezaji wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi unaonesha kuwa rasilimali fedha si kila kitu pekee katika kuwawezesha wananchi kiuchumi bali kila kundi linahitaji mahitaji yake, mfano mkulima anahitaji soko la mazao yake ili aweze kuongeza tija kwenye kilimo chake,” alisema Prof. Ngowi.
Akichangia mjadala huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Francis Assenga alisema kuwa Benki yake ina Dira ya kuwa benki ya mfano na ya kisasa katika kuleta mapinduzi ya kilimo Tanzania kwa kuwawezesha wananchi kwa kuzingatia mahitaji maalumu kuendana changamoto za kimaeneo hili kuwezesha wananchi kiuchumi nchini ili kutekeleza kwa vitendo dhamira ya Serikali kuwafikisha wananchi wake kufikia hadhi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
“Muundo wa TADB ni tija katika kuchagiza uwezeshaji wananchi kiuchumi hasa wakulima wadogo nchini kwani Benki inafanyia kazi mnyororo mzima wa ongezeko la thamani katika kilimo kwa kutatua changamoto mbali mbali kama vile kiwango kidogo cha uzalishaji; ukosefu wa mbinu na teknologia za kisasa; matumizi madogo ya umwagiliaji,” alisema
Aliongeza: “Changamoto nyingine ni ukosefu wa mtaji na upatikanaji wa mikopo kwa wakulima; ukosefu wa masoko ya mazao; ufinyu wa bei za mazao; miundo mbinu mibovu ya usafirishaji; maghala ya kuhifadhi mazao; nishati ya umeme na miundombinu hafifu vijijini; ufinyu au kutokuwepo kwa ongezeko la thamani kwa mazao ya kilimo; mabadiliko ya hali ya hewa; na mmomonyoko wa udongo, pamoja na changamoto zinginezo,” aliongeza.
Kuanza kufanya kazi kwa Benki ya Kilimo kunaleta suluhisho la changamoto nyingi zilizokuwa zinaikabili sekta kilimo na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kama inavyowekwa bayana na dhima ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambayo inalenga kuwaongoza watanzania katika kujenga uchumi wenye nguvu kwa kuboresha mazingira ya kibiashara na kutoa fursa sawa za kiuchumi.
Kongamano la Mwaka la Uwezeshaji linafanyika katika kutekeleza Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi iliyoundwa mwaka 2004 na Sheria ya Uwezeshaji namba.16 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment