HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 14, 2017

Watanzania Watakiwa Kuchangamkia Ajira Ujenzi wa Reli ya Kisasa

Na: Frank Shija–MAELEZO


WATANZANIA watakiwa kuchangamkia fursa za Ajira zitokanazo na utekelezaji wa Ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) Line kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro.

Wito huo umetolewa na Afisa Uhusiano wa Shirika Hodhi la Miundombinu ya Reli (RAHCO) Bi. Catherine Mushi wakati wa ziara ya kutembelea ujenzi wa Kambi ya Wafanyakazi wa Kampuni ya Yapi Merkezi inayotekeleza ujenzi wa mradi huo iliyo Shaurimoyo, Kariakoo Jijini Dar es Salaam leo.

“Nitoe rai kwa watanzania wajitokeze kwa wingi kuomba nafasi za ajira zitokanazo na ujenzi wa Reli hii, mkataba baina yetu na Mkandarasi uko wazi, wazawa wana asilimia 20% ya nafasi zote za ajira, pelekeni maombi yenu katika ofisi za Mkandarasi zilizopo Upanga mtaa wa Lugalo ili mnufaike na rasilimali zenu,” alisema Bi. Catherine.

Wakati huohuo Bi.Catherine amewatahadharisha wananchi kuepuka kutapeliwa na watu wanaopita mitaani wakiwalaghai kuwa wao ni mawakala wa ajira waliotumwa na RAHCO kwa ajiri ya kutoa ajira kwa watanzania wanaohitaji kufanyakazi katika ujenzi wa mradi wa Reli hiyo badala yake amewataka wananchi kupelekea maombi yao kwenye Ofisi za Mkandarasi Kampuni ya Yapi Merkezi zilizopo Mtaa wa Lugalo Upanga Jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia mradi huo amesema kuwa ujenzi umeanza kwa hatua mbalimbali za Kiinjinia ambazo ni pamoja na kupendekeza njia ambapo Reli itapita, ujenzi wa Kambi zitakazotumiwa na mafundi pamoja na wafanyakazi wakati wa ujenzi wa mradi huo.

Bi. Catherine amezitaja Kambi hizo kuwa ni pamoja na Shaurimoyo, iliyopo Ilala, Dar es Salaam, Soga Kibaha mkoani Pwani pamoja na Ngerengere mkoani Morogoro.Ambapo Kambi ya Soga ndiyo itakuwa kubwa itakayokuwa na kiwanda kwa ajili ya kutengeneza Mataruma ya Reli yanayotumia Simenti.

Amesema kuwa Kambi hizo zitatumiwa na wafanyakazi waandamizi wa Kampuni ya Yapi Maerkezi ambapo watakuwa wanalala hapo kwa ajili ya kurahisisha shughuli zao ikiwemo urahisi wa kuhamisha mitambo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kadri ya mahitaji.

Kwa mujibu wa Afisa Uhusiano huyo takribani watanzania 150 wameajiriwa katika hatua ya awali ya ujenzi wa Kambi ya Shaurimoyo ambayo inakadiriwa kutumiwa na wafanyakazi zaidi ya 100 itakapokamilika.

Ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) Line kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro yenye urefu wa Kilomita 300 ulizinduliwa rasmi tarehe 12 Aprili, 2017 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Jamhuri ya Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambapo, ujenzi huo unafanywa na Kampuni ya Yapi Merlkezi kutoka Uturuki kwa kushirikiana na Kampuni ya Motaengli Afrika na kugharimu takribani sh.2.7.

Ujenzi huu ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge). Mradi wote utajengwa kwa awamu nne ambapo una jumla ya urefu wa kilomita1,219 utakaoanzia Dar es Salaam hadi Mwanza. Mradi huo unatakadiriwa kuibua takribani ajira milioni moja hadi kukamilika kwake.

No comments:

Post a Comment

Pages