WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Mataifa ya Afrika yanatakiwa yaandae
maarifa, vitendea kazi na rasilimali watu watakaoweza kusimamia na
kuendeleza ipasavyo sekta ya madini na kuleta tija kwa Taifa husika na
wananchi kwa ujumla.
Amesema
taarifa za kijiolojia zinaonesha kuwa Afrika ni Bara lenye utajiri
mkubwa wa rasilimali madini huku sehemu kubwa ya madini hayo yakiwa bado
hayajaanza au yako kwenye hatua mbalimbali za uendelezaji.
Ametoa
kauli hiyo leo (Alhamisi, Septemba 14, 2017) alipofungua mkutano wa 37
wa Baraza la Uongozi wa Kituo cha Madini na Jiosayansi cha Afrika (AMGC)
uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kituo hicho mkoani Dar es
Salaam.
Waziri
Mkuu amesema rasilimali za madini ilizopo Barani Afrika inaweza kuwa ni
chanzo kikubwa cha kusukuma maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika
nchi nyingi iwapo itasimamiwa vizuri.
Ametolea
mfano Tanzania ambayo licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa madini ya
dhahabu, almasi, chuma, madini ya vito kama tanzanite lakini mchango wa
sekta ya madini ni asilimia 4.8 ya pato ghafi la Taifa.
“Changamoto
kuu kwa sasa ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa na sekta ya madini
inayotoa mchango stahiki katika nchi husika pamoja na kusimamia sekta
hii kwa kuwafanya wananchi wetu hususan katika maeneo yenye rasilimali
wakanufaika na kuona fahari badala ya kuacha mashimo, umasikini na
mateso kwa wananchi.”
Amesema
lengo la kuanzishwa kwa kituo hicho ambacho leo kimetimiza miaka 40 ni
kuhakikisha sekta ya madini inawajibika kuleta maendeleo ya kijamii na
uchumi pia ikijali masuala ya mazingira, hivyo ni vema kikatumika kama
ilivyokusudiwa.
Waziri
Mkuu amesema kituo hicho kikitumika vema kwa mujibu wa kusudia la
uanzishwaji wake kinaweza kuleta tija kubwa kwenye sekta ya uchumbaji wa
madini, uongezaji wa thamani na usimamizi wa sekta.
Amesema
kituo hicho ni moja kati ya taasisi chache duniani yenye teknolojia za
kisasa ambazo zinaweza kusaidia kufanya uchambuzi wa miamba na madini
yaliyimo. “Pia ni sehemu ambayo unaweza kupata huduma za ushauri na
kusaidia teknolojia utakayoweza kutumia ili kufanya uzalishaji wa madini
mbalimbali.”
Hivyo
amewakumbusha wajumbe na wanachama wa AMGC kuwa kituo hicho
hawajakitumia ipasavyo ni vema kikatumika ili kupata tija kwenye
uendelezaji na usimamizi wa madini, ambapo ameiagiza Bodi iandae mpango
utakaoziwezesha nchi wasnachama kukitumia.
Kwa upande wake,
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amesema kwa
sasa kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ya kwanza ni kwa
wanachama kutolipa ada kwa wakati.
Dkt.
Kalemani ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Kituo cha AMGC
amesema changamoto ya pili ni wanachama wa kituo hicho kutokitafutia
wateja na masoko. Pia miundombinu mingi ya kutuo ni chakavu.
Akizungumzia
changamoto hizo Waziri Mkuu ameziagiza nchi zote zinazodaiwa ada
ikiwemo Tanzania zilipe ada stahiki kwa wakati na kuweka mkakati wa
kukitangaza kituo hicho ili kukiwezesha kupata wateja kwa ajili ya
kutumia huduma zitolewazo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, SEPTEMBA 14, 2017.
No comments:
Post a Comment