HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 14, 2017

SIKU 72 ZA MANJI MAHABUSU

Mfanyabiashara Yusuf Manji, akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo baada ya kufutiwa shtaka la uhujumu uchumi lililokuwa linamkabili. (Picha na Said Powa).
 Manji akitoa mahakamani.
 Manji akitoa mahakamani leo.
Na Mwandishi Wetu

MFANYABIASHARA Yusuf Manji leo ameachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu pamoja na wenzake watatu waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.



Manji aliyesota rumande takribani siku 72, ameachiwa huru pamoja na  washtakiwa wengine ambao ni Meneja Rasilimali watu wa Kampuni ya Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda, Mtunza Stoo, Abdallah Sangey na Thobias Fwere.

Wakili wa serikali mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alimueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa wameomba hati ya kumtoa gerezani (remove order) na kwamba Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) kwa niaba ya Jamhuri wanaiharifu mahakama kwamba hakusudii kuendelea kuwashtaki Manji na wenzake katika shauri hiyo.

Shauri hilo limeondolewa chini ya kifungu cha 91(1) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Baada ya kueleza hayo wakili wa Manji, Hajra Mungula alieleza kuwa sheria inaruhusu DPP kufanya hivyo.

Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Shaidi alisema kesi hiyo imefutwa na kuanzia sasa washtakiwa hao wapo huru.

"Nendeni nyumbani hamkamatwi, hakuna kesi mpo huru," alisema Hakimu Shaidi wakati Manji na wenzake wakiwa hawaamini kama wameachiwa huru.

Katika kesi hiyo, Manji na wenzake watatu walikuwa wakikabiliwa na mashtaka saba chini ya sheria ya uhujumu uchumi na usalama wa Taifa kwa kukutwa na vitambaa vinavyotengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vyenye thamani ya zaidi ya Sh 200 milioni na mihuri.

Baada ya kuachiwa huru Manji bado alionekana hana furaha huku akionekana mnyonge na machozi yakimlenga wakati akitoka mahakamani akielekea kupanda gari.

Manji aliondoka mahakamani hapo na gari ndogo ya rangi ya bluu aina ya Alteza yenye namba za usajili T 383 DFN.

Kesi hiyo iliyokuwa ikimkabili Manji ya uhujumu uchumi wengi hawakutegemea kilichofanyika kutokana na makosa hayo kutokua na dhamana.

Kwa sasa Manji anakabiliwa na shtaka moja la kutumia dawa za kulevya katika mahakama hiyo ambapo katika kesi hiyo yupo nje kwa dhamana.

No comments:

Post a Comment

Pages