Na:
Mwandishi Wetu, MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo amepokea ripoti mbili za Kamati Maalum za
Bunge za Uchunguzi wa madini ya Tanzanite na Almasi na kusisitiza kuwa yeye
yupo Ikulu kufanya kazi wala si kutafuta mchumba.
“Watanzania tumechezewa kwa miaka
50, sasa ni wakati wa kufanya kazi; lazima tuamke tukatae kuibiwa huku
tunakoimbiwa sasa kama kwamba tumerogwa” alisema Dkt. Magufuli mara baada ya
kukabidhiwa ripoti hizo.
Aliwaambia viongozi na wananchi waliokuwa wakifuatilia
tukio hilo kupitia vituo vya televisheni, redio na mitandao ya kijamii kuwa
Ikulu ni sehemu ya kupita na yuko radhi aonekane mwanasiasa mkorofi asiyependwa
lakini lazima atatekeleza jukumu lake la kutetea na kulinda rasilimali za taifa
kwa manufaa watanzania wote wa leo, kesho na mtondogoo.
Alibanisha kuwa fedha zinazoibiwa
kwa matrilioni zingetosha kubadili maisha ya watanzania wengi kwa kuwapatia
huduma za jamii na hata kulipana mishahara mikubwa hivyo akiwa Rais hawezi
kukubali hilo liendelee.
“Tuangalie maisha yetu yalivyo
kila mmoja amuangalie jirani yake anavyoishi maisha ya shida huku rasilimali
zote zikiibiwa na watu wakituacha katika umasikini”alieleza Rais Magufuli na
kuongeza kuwa wanyonyaji hao hawana huruma kabisa na watanzania.
Akionesha kuchukizwa na matokeo ya
ripoti hizo, Rais Mafuguli alisema kama baadhi iliyoelezwa kuwa udhaifu huo
unatokana na mfumo basi huo mfumo lazima ufumuliwe.
“Unaposaini mikataba ya aina hii
na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu inahusika basi kama ni mfumo tuufue ili tufikie
mahala maslahi yetu ya nchi yapewe kipaumbele” alisisistiza Rais Magufuli na
kuongeza kuwa “Tukienda kwa utaratibu huu, tutakuwa watumwa milele”
Katika hotuba yake hiyo, Rais
alisema mambo mengine ni aibu kuyasema na kusisitiza kuwa yeye hataki baada ya
kumaliza muda wake kuwa miongoni mwa wale wanaotajwa kuwa “Nae alikuwepo hapa“
Alisema yeye binafsi angependa
kuona watanzania wanakuwa matajiri kutokana na rasilimali zao si kuwanufaisha watu
wa nje na makuwadi wao wa ndani ambao aliwaeleza kuwa watu waliokosa uzalendo.
Alizipongeza ripoti hizo kuwa
zimekidhi matarajio yake na kwamba zimempunguzia kazi ya kutafuta wataalamu
wengine kuchunguza jambo hilo na kulipongeza Bunge kwa kutimiza wajibu wake huo
vyema.
Katika mnasaba huo alimuagiza Waziri
Mkuu kuwaita wataalamu wa sheria washirikiane na Bunge kukaa pamoja na kufanya
marekebisho ya sheria.
“Tusiulizwe kwa nini tunabadili
sheria hivi sasa kwani jibu ni wazi kuwa huu ndio wakati unaofaa kufanya hivyo”
alisisitiza Rais Magufuli.
Katika mkutano huo alivipongeza
vyombo vya habari kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhabarisha wananchi na akatoa
wito kwa vyombo hivyo kuendelea kuelimisha wananchi wajitambue na kuwa
wazalendo.
No comments:
Post a Comment