WAZIRI wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema utapiamlo ni janga la Kitaifa na kwamba theluthi moja ya vifo nchini inasababishwa na tatizo hilo.
Ametoa kauli hiyo juzi jioni (Jumatano, Septemba 6, 2017)
wakati akitoa nasaha kwenye mkutano wa nne wa
mwaka wa wadau wa lishe wa kutathmini afua za lishe nchini kwenye ukumbi wa
Hazina mjini Dodoma.
“Haipendezi kuona katika
kila watoto 100, watoto 34 wana udumavu wa akili na katika kila watoto 100,
watoto 59 wenye umri kati ya miezi sita na miaka mitano wana upungufu mkubwa wa
damu,” alisema. Alisema Serikali inatumia asilimia mbili ya pato la Taifa sawa
na dola za Marekani milioni 518 kununua dawa za vitamin A na folic acid (vidonge
vya kuongeza damu).
Alisema kuna haja ya kubuni
mbinu za kilimo ambazo zitainua kiwango cha upatikanaji wa lishe nchini
(nutrition smart agriculture) kama njia ya kudumu ya kukabili tatizo la
utapiamlo na udumavu.
Amesema kwa vile Serikali
imetenga sh. bilioni 11 ili kukabiliana na utapiamlo, wizara yake itahakikisha
inatafuta fedha zilizotengwa na hata ikibidi kutafuta fedha na misaada ya kitaalamu
kutoka nje ya nchi ili kuhakikisha suala hilo linatekelezwa.
Kwa upande wake, Naibu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bw. Selemani Jaffo aliziagiza Halmashauri
zote nchini zitoe taarifa za kila mwezi za matumizi ya fedha za afua ya lishe
kwenye Kamati zake za Fedha. “Hizi fedha si za kufanya masikhara, Serikali iko committed katika suala hili,” alisema.
“Zamani katika bajeti za
Halmashauri tulikuwa tukitenga sh. 500 kwa kila mtoto, lakini katika bajeti ya
mwaka 2017/2018 tumetenga sh. 1,000 kwa kila mtoto, ambazo ni sawa na sh.
bilioni 11 kwa mwaka,” alisema wakati alipopewa fursa ya kutoa nasaha zake.
“Wiki iliyopita, Makamu wa
Rais alituagiza tuandike performance
contracts kwa Wakuu wote wa Mikoa nchini ili tuweze kufuatilia utekelezaji
wao katika suala zima za kuboresha upatikanaji wa lishe nchini. Kazi hiyo
tumeshaianza na tarehe 22 Septemba, 2017 itakuwa ni siku ya mwisho ya
kukamilisha zoezi hilo,” alisema.
Bw. Jaffo aliwataka waganga
wakuu wa mikoa na wilaya waifanye ajenda ya afya ya lishe kuwa kipaumbele chao.
Wakati huohuo, Naibu Waziri Jaffo amesema
kuwa maafisa lishe 660 wataajiriwa nchini kote hivi karibuni. Amesema waliopo
hivi sasa ni wataalamu 121 tu ambao kati yao 17 wako mikoani na 104 wako kwenye
Halmashauri mbalimbali.
Naye Mkurugenzi wa USAID hapa nchini,
Bw. Andrew Karas aliipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kuchukua umiliki na usimamizi
wa masuala ya lishe ikiwa ni hatua muhimu ya uratibu wa suala hilo baina ya
wahisani, wadau na Serikali.
Alisema ushirikishwaji wa
wadau ni suala muhimu na ambalo haliepukiki lakini akaonya kuwa kuna haja ya
kuangalia namna ya kuongeza uwezo wadau kwa vitendo ili kuwawezesha kutekeleza
majukumu yao ipasavyo.
“Lengo leni ni letu, na
kipaumbele chenu ni chetu. Tukisaidiana tutaweza kufanikisha suala la kuongeza
lishe na kupunguza atahari za utapiamlo hapa nchini,” alisema Bw. Karas kwa
Kiswahili fasaha na kuamsha shangwe katika ukumbi huo.
Bw. Karas ambaye
alizungumza kwa Kiswahili kwa zaidi ya dakika tano, alikuwa akitoa salamu
kutoka mtandao wa wahisani wa wenye lengo la kufuta utapiamlo kwa kuboresha
lishe nchini (Scaling Up Nutrition -SUN) ambao unajumuisha mashirika ya
Children Investment Fund, DfID, Umoja wa Ulaya (EU), Global Affairs Canada, Irish
Aid na USAID.
Naye Mwakilishi Mkazi wa UNICEF, Bibi
Maniza Zaman, akitoa salamu kwa niaba ya mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyo
chini ya mtandao wa SUN, alisema kufutwa kwa utapiamlo na kuimarishwa kwa
uapikanaji wa lishe bora nchini kunaenda sambamba na utekelezaji wa malengo 17
endelevu ya maendeleo.
“Kipengele kimojawapo kikidumaa, kinakwamisha
utendaji kazi wa kingine,” alisema na kuongeza: “Mpango uliozinduliwa unahitaji
kuwa na fedha za uhakika ili uweze kutekelezeka. Inatia moyo kuona Halmashauri
na Sekretarieti za Mikoa zimetenga bajeti kwa ajili ya mpago huu.”
Naye Mkurugenzi
Mtendaji wa Mtandao wa Masuala ya Lishe Tanzania (Partnership for Nutrition in
Tanzania - PANITA), Bw. Tumaini Mikindo aliiomba Serikali iziwekee uzio maalum
wa kibajeti (ring-fence) fedha za masuala ya lishe ili kuzilinda zisitumike
kinyume na matumizi yaliyopangwa.
“Tunaomba
fedha za kasama ya lishe ziwe ring-fenced ili ziweze kutumika kama
zilivyopangwa. Watendaji watakaofanya vizuri wapongezwe na wale watakaoharibu
wachukuliwa hatua za kinidhamu kwa sababu wanataka kuua Taifa letu,” alisema
wakati akitoa salamu kwa niaba ya mashirika yasiyokuwa ya Serikali zaidi ya 300
yaliyo chini ya mtandao wa SUN.
Alisema
mtandao wao umeenea nchi nzima na akiomba Serikali ilisimamie suala la
kupambana na utapiamlo na kuboresha lishe kwa wananchi wake kama ambavyo
ilisimamia suala la uhaba wa madawati nchini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 DODOMA,
IJUMAA, SEPTEMBA 8, 2017.
No comments:
Post a Comment