September 03, 2017

‘SERIKALI INATOA SH. BILIONI 22 KILA MWEZI KUBORESHA ELIMU’

SERIKALI imesema hivi sasa inatoa sh. bilioni 22.2 kila mwezi ili kuboresha elimu ya msingi na sekondari hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa jana (Jumamosi, Septemba 2, 2017) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bw. George Simbachawene wakati akizungumza na wahitimu 166 wa darasa la saba wa shule ya msingi ya Martin Luther, kwenye sherehe za mahafali ya 10 zilizofanyika shuleni hapo katika Manispaa ya Dodoma.

Waziri Simbachawene ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema Serikali itaendelea kuboresha elimu ya sekondari kwa kuajiri walimu wengi zaidi wa masomo ya sayansi.

“Wazazi wa wanafunzi wanaohitimu tunawakaribisha kwenye shule za sekondari kwa sababu zote zina walimu wa kutosha, madawati na vifaa vya kufundishia. Kila mwezi tunatenga sh. bilioni 22.2 kuendesha shule za msingi na za sekondari hadi kidato cha nne,” alisema.

Alisema hivi sasa, baadhi ya shule zinakabiliwa na changamoto ndogo ya upungufu wa walimu wa sayansi lakini nayo itatuliwa hivi karibuni kwa sababu vibali vya ajira vimeanza kutolewa.

“Tunaendelea kuziboresha na tumeshuhudia miaka ya karibuni wanafunzi bora kitaifa wakitoka katika shule za Serikali ambazo wengi wamezoea kuziita ni shule za kata. Hakuna shule za kata. Zote ni zimejengwa na Serikali,” alisisitiza.

“Ukienda vyuo vikuu, wanafunzi na ufaulu wa juu wengi wao ni wale waliotoka kwenye shule za Serikali,” aliongeza.

Aliwataka wanafunzi wanaojiandaa kufanya mitihani yao Septemba 6 na 7, wasiwe na hofu kwani kufanya hivyo ni chanzo cha kuwafanya wachanganye mambo na kisha kufeli.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shule hiyo, Bw. Rabbiely Mmanga aliwaasa wazazi na kuwaomba wasiwaingize watoto kwenye migogoro kwani matendo hayo yanawajisi watoto na kuwaathiri kisaikolojia hata wawapo shuleni.

“Ninawaomba sana wazazi, tofauti zenu ziishie chumbani na zisifike masikioni mwa watoto kwa sababu zinawasumbua kisaikolojia na kuwaharibia concentration yao kimasomo. Tumewahoji baadhi na wamesema wanaumia kwa kukumbuka adha ambayo mama anaipata kutoka kwa baba, au baba anaipata kutoka kwa mama,” alisema.

Katika mahafali hayo, wanafunzi mbalimbali walipewa vyeti kwa kufanya vizuri kwenye masomo mbalimbali huku Ismail Milambo na Nise-Magreth Malila wakiibuka kidedea kwenye masomo yote (best academic performers). Tuzo za nidhamu bora (discipline) zilichukuliwa na Michael Nyalusi na Sayuni Kampuni.

Wanafunzi wengine waliopata tuzo na masomo yao kwenye mabano ni Ismail Milambo (Hisabati), William Terry William (Kiingereza), Majaliwa K. Majaliwa (Sayansi), Nise Malira (Kiswahili), Clinton Dotto (Social Studies) na Justin Kilimali (Kompyuta).

Wengine walipewa tuzo kwenye vipengele vya michezo, uchoraji na sanaa, usafi, uongozi shuleni, uimbaji na uongozi wa ibada.

Katika risala yao, wanafunzi wanaohitimu walisema  wanaamini misingi ya elimu walioipata kwenye shule ya Martin luther haitapotea bure na wakaahidi kufanya mitihani yao kwa umakini ili watoke na ufaulu wa hali ya juu.

Wanafunzi wa darasa la saba kote nchini, wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya kitaifa Septemba 6 na 7, mwaka huu.
   
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA.            
JUMAPILI, SEPTEMBA 3, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages