WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania ipo
salama na imara na kwamba mtu yeyote atakayejaribu kutaka kuvuruga amani
atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Septemba 13, 2017)
alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Iran nchini Tanzania, Bw. Mousa
Farhang jijini Dar es Salaam.
“Hatua kali
zitachukuliwa kwa yeyote kutoka popote atakayejaribu kuvuruga amani yetu.
Nawaomba wananchi muwe makini na muendelee kuidumisha amani yetu.”
Amesema kwa sasa Serikali ipo katika mapambano dhidi
ya vitendo vya ufisadi, rushwa, biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na
wahujumu uchumi.
Waziri Mkuu amesema licha
ya Tanzania kuwa ni nchi ya amani na yenye utulivu wa kisiasa, wameendelea
kuwahamasisha wananchi wake kudumisha mshikamano.
Amesema mbali ya kuimarisha
amani nchini, pia Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji jambo ambalo
litawawezesha watakaokuja kuwekeza nchini kupata tija.
Hivyo ametumia fursa
hiyo kuwakaribisha
wawekezaji kutoka nchini Iran ili waje kuwekeza kwenye viwanda mbalimbali
vikiwemo vya kuchakata mazao ya kilimo.
Pia amewakaribisha raia wa Iran kutembelea vivutio
mbalimbali vya utalii vilivyoko nchini Tanzania kama mlima wa Kilimanjaro,
fukwe, mali kale na mbuga za wanyama.
Kwa
upande wake, Balozi Farhang ameipongeza Serikali kwa kuwa na dhamira ya dhati
ya kuimarisha uchumi na kupambana na dawa za kulevya na ufisadi.
Balozi huyo amesema Serikali ya Irani ipo tayari
kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi
pamoja na vitendo vingine vya kihalifu.
Balozi Farhang ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali
ya Tanzania ifungue Ofisi ya Ubalozi nchini Iran ili kuimarisha uhusiano huo,
ambapo Waziri Mkuu amekubali.
Pia Bw. Farhang amesema aliwahi kutembelea mbuga za
wanyama za Serengeti na Ngorongoro na kusema kwamba ni maeneo mazuri ambayo
hajawahi kuyaona tangu azaliwe.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO,
SEPTEMBA 13, 2017.
No comments:
Post a Comment