September 13, 2017

TRA YAONGEZA UFANISI WA UKUSANYAJI KODI YA MAJENGO

Serikali imeeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2016/17 Mamlaka ya Mapato Nchini, (TRA) imekusanya Kodi ya Majengo kwa ufanisi zaidi ikilinganishwa na kipindi ambacho kodi hiyo ilikuwa ikikusanywa na Halmashauri.

Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri waFedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Cecilia Paresso(CHADEMA), aliyetaka kujua baada ya TRA kupewa jukumu la kukusanya kodi za majengo basala ya Halshauri za Miji, Manispaa na Majiji, ufanisi wake umefikiwa kiasi gani ikilinganishwa na mapato yaliyokuwa yakikusanywa na Halmashauri zenyewe. 

Katika swali hilo Mhe. Paresso alisema kuwa kodi hiyo ilikuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Halmashauri hizo yaliyokuwa yakitumika katika kutekeleza majukumu ya kutoa huduma kwa wananchi.
 
“Baada ya TRA kupewa jukumu la kukusanya kodi ya majengo majukumu ya Halmashauri hizo hayajapungua, je Serikali imejipanga vipi kufidia vyanzo hivyo?,” alihoji.
 
Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji alisema ufanisi wa TRA katika kukusanya kodi ya majengo umeongezeka kwa asilimia 20.6 kutoka Sh. bilioni 28.28 mwaka 2015/16 hadi Sh. Bil 34.09 mwaka 2016/17.

Dkt. Kijaji alifafanua kuwa Serikali inatambua kuwa kodi ya majengo imekua ikichangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Halmashauri husika katika kutekeleza mipango ya utoaji huduma za jamii na imeweka utaratibu wa kibajeti ambao unaziwezesha Halmashauri hizo kupata fedha za makusanyo ya kodi ya majengi iliyokusanywa na TRA ili kuziwezesha kutimiza majukumu yao.
 
“Utaratibu uliopo ni kwamba, Halmashauri zinatakiwa kuomba fedha hizo kutoka Serikali Kuu kwa kuzingatia makisio ya bajeti zao, kwa mantiki hiyo Halmashauri zinashauriwa kuzingatia utaratibu huo ili ziweze kupata fedha hizo,”alisema Dkt. Kijaji.
 
Alisisitiza kuwa hatua ya Serikali kuhamisha jukumu hilo la kukusanya kodi TRA halikulenga kuzinyang’anya Halmashauri vyanzo vya mapato bali ni kuimarisha ukusanyaji wake kwani takwimu zilizoainishwa hapo juu zinadhihirisha kuwa TRA imefanya vyema katika kukusanya mapato hayo ikilinganishwa na Halmashauri.

Imetolewa na:

Benny Mwaipaja

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Fedha na Mipango

No comments:

Post a Comment

Pages