HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 09, 2017

WAKUU WA MIKOA 10 WAAGIZWA KUSIMAMIA PAMBA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa 10 inayolima pamba nchini wasimamie zao hilo kwa karibu ili kuinua uzalishaji wake na kuwaongezea kipato wananchi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni (Ijumaa, Septemba 8, 2017) wakati akizungumza na wakuu hao wa mikoa kwenye kikao alichokitiisha mjini Dodoma kujadili mbinu za kufufua zao hilo.

Wakuu wa mikoa walioitwa kwenye kikao hicho ni kutoka mikoa ya Shinyanga, Singida, Kagera, Tabora, Morogoro, Mara, Mwanza, Simiyu, Katavi na Geita.

“Serikali imeamua kufufua mazao makuu matano ya biashara ambayo ni pamba, chai, kahawa, korosho na tumbaku na leo nimetaka nianze na ninyi wakuu wa mikoa ili mwende mkawasimamie watu wenu tunapokaribia kuanza msimu mpya,” alisema.

Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kusimamia kilimo cha pamba kuanzia maandalizi ya shamba, kupanda, matumizi ya pembejeo na dawa, kuvuna na kutafuta masoko na akawataka wasimamie katika maeneo yao ili kilimo cha zao hilo kiweze kubadilika.

“Kuna maafisa kilimo kwa kila Halmashauri iliyoko kwenye mikoa yenu. Maafisa kilimo hawa lazima wahusike kikamilifu. Moja ya majukumu yake kwa cheo chake, kazi kubwa aliyonayo ni kusimamia zao la pamba. Kama hajafanya kazi hiyo, usiridhike kuwa na afisa kilimo wa aina hiyo,” alisema.

“Ni lazima kila mmoja awe na mpango kazi, ausimamie na atoe matokeo ya kuwa zao hili limefanikiwa katika eneo lake. Tunataka zao hili lichukue nafasi yake ya namba moja. Heshima ya “Dhahabu Nyeupe” lazima irudi lakini pia ni vema mkumbuke kuwa zao la pamba ni uchumi, zao la pamba ni siasa katika mikoa yenu,” alisisitiza.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba; Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI; Bw. Suleiman Jafo, Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Tito Haule na Mkurugenzi Msaidizi wa Uhamasishaji Mazao, Bw. Beatus Malema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 DODOMA, 
JUMAMOSI, SEPTEMBA 9, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages