WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewaagiza wakuu wa mikoa 10 inayolima pamba nchini wasimamie zao hilo kwa
karibu ili kuinua uzalishaji wake na kuwaongezea kipato wananchi.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni (Ijumaa, Septemba 8, 2017) wakati akizungumza na
wakuu hao wa mikoa kwenye kikao alichokitiisha mjini Dodoma kujadili mbinu za
kufufua zao hilo.
Wakuu wa mikoa walioitwa
kwenye kikao hicho ni kutoka mikoa ya Shinyanga, Singida, Kagera, Tabora,
Morogoro, Mara, Mwanza, Simiyu, Katavi na Geita.
“Serikali imeamua kufufua
mazao makuu matano ya biashara ambayo ni pamba, chai, kahawa, korosho na
tumbaku na leo nimetaka nianze na ninyi wakuu wa mikoa ili mwende mkawasimamie
watu wenu tunapokaribia kuanza msimu mpya,” alisema.
Waziri Mkuu alisema
Serikali imeamua kusimamia kilimo cha pamba kuanzia maandalizi ya shamba,
kupanda, matumizi ya pembejeo na dawa, kuvuna na kutafuta masoko na akawataka
wasimamie katika maeneo yao ili kilimo cha zao hilo kiweze kubadilika.
“Kuna maafisa kilimo kwa
kila Halmashauri iliyoko kwenye mikoa yenu. Maafisa kilimo hawa lazima wahusike
kikamilifu. Moja ya majukumu yake kwa cheo chake, kazi kubwa aliyonayo ni
kusimamia zao la pamba. Kama hajafanya kazi hiyo, usiridhike kuwa na afisa
kilimo wa aina hiyo,” alisema.
“Ni lazima kila mmoja awe
na mpango kazi, ausimamie na atoe matokeo ya kuwa zao hili limefanikiwa katika
eneo lake. Tunataka zao hili lichukue nafasi yake ya namba moja. Heshima ya “Dhahabu
Nyeupe” lazima irudi lakini pia ni vema mkumbuke kuwa zao la pamba ni uchumi,
zao la pamba ni siasa katika mikoa yenu,” alisisitiza.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Kilimo,
Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba; Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –
TAMISEMI; Bw. Suleiman Jafo, Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara
ya Kilimo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Tito Haule na Mkurugenzi Msaidizi
wa Uhamasishaji Mazao, Bw. Beatus Malema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 DODOMA,
JUMAMOSI, SEPTEMBA 9, 2017.
No comments:
Post a Comment