September 12, 2017

WAZIRI MKUU AKUTANA NA MKURUGENZI WA KAMPUNI YA NAMERA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (R)amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Namera Group of Industries Bw. Hamza Rafiq Pardesi (c) ambaye ameahidi kununua pamba yote itakayozalishwa nchini kuanzia msimu ujao.(L) Ni Meneja wa Namera Bwana Muhammad Waseem. Waziri Mkuu amekutana nao leo Septemba 12/ 2017 Ofisini kwake Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

 *Aahidi kununua pamba yote itakayozalishwa nchini

 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Namera Group of Industries Bw. Hamza Rafiq Pardesi ambaye ameahidi kununua pamba yote itakayozalishwa nchini kuanzia msimu ujao.

Amekutana na Bw. Pardesi leo (Jumanne, Septemba 12, 2017)  kwenye makazi ya Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar es Salaam na amesema kwamba tayari Serikali imeanza kuwahamasiha wakulima kuongeza uzalishaji kwa kuwa kuna soko la uhakika.

Waziri Mkuu amempongeza Bw. Pardesi kwa kuiunga mkono Serikali katika mpango wake wa kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda. Kampuni ya Namera Group of Industries inamiliki kiwanda cha nguo cha NIDA na cha Namera vya jijini Dar es Salaam.Kampuni inatarajia kufungua kiwanda kingine cha nguo wilayani Kahama.

Pia Waziri Mkuu amesema katika kuhakikisha zao la pamba linapewa kipaumbe alikutana na wakuu wa mikoa yote inayolima pamba Ijumaa, Septemba 8, 2017 na aliwaagiza wasimamie zao hilo kwa karibu ili kuinua uzalishaji wake na kuwaongezea kipato wananchi hususan wakulima wa zao la pamba.

Amesema Serikali imeamua kufufua mazao makuu matano ya biashara ambayo ni pamba, chai, kahawa, korosho na tumbaku ili kuwawezesha wakulima kupata tija na kuondokana na umasikini wa kipato, hivyo kukuza uchumi wa Taifa.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeamua kusimamia kilimo cha pamba kuanzia maandalizi ya shamba, kupanda, matumizi ya pembejeo na dawa, kuvuna na kutafuta masoko, hivyo ahadi yao ya kununua pamba yote ni faraja kwa wakulima.
“Nimefurahishwa na uamuzi wenu wa kutaka kununua pamba yote itakayozalishwa nchini kuanzia msimu ujao kwani kwetu sisi ni faraja kwa sababu wakulima walipunguza uzalishaji baada ya kukosa soko la uhakika.”
Kwa upande wake Bw. Pardesi amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba kampuni yao inauwezo wa kununua pamba yote inayozalishwa nchini na kuichakata katika viwanda vyao na kutengeneza nguo zitakazouzwa nchini kwa bei nafuu.
Amesema kwa sasa wameajiri mafundi katika viwanda vyao ambao watakuwa wa nashona nguo na kuziuza nchini kwa gharama nafuu ili kuwawezesha wananchi wa hali ya chini kumudu kununua na kuondokana matumizi ya nguo za mitumba.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu sisi Namera tuko tayari kununua pamba yote inayozalishwa nchini kwani viwanda vyetu vinafanya kazi ya kuchambua pamba, kutengeneza nyuzi na majora kisha tunashona nguo na kuziuza. Hapa Kazi Tu maana bila ya kufanya kazi huwezi kuheshimika.”
Hata hivyo Mkurugenzi huyo amesema kitendo cha kununua pamba inayolimwa nchini na kuchakata katika viwanda vyao kwa lengo la kutengeneza nguo za aina mbalimbali wataiwezesha Serikali kuokoa fedha nyingi za kigeni zilizokuwa zinatumika kuagiza nguo nje ya nchi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMANNE, SEPTEMBA 12, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages