WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea ripoti mbili za kamati
ya Maalumu ya Bunge ya kuchunguza biashara ya madini ya almasi na tanzanite na
kuahidi kuiwasilisha kwa Rais Dkt. John Magufuli kesho asubuhi.
Pia amesema Serikali haina mchezo katika usimamizi wa
rasilimali za Taifa, hivyo amewataka viongozi
na watendaji wote waliokabidhiwa dhamana ya kusimamia sekta ya madini
hakikisha wanatimiza vyema wajibu wao.
Waziri Mkuu amepokea ripoti hizo leo (Jumatano, Septemba
6, 2017) kutoka kwa Spika wa Bunge, Bw. Job Ndugai ambaye alikabidhiwa ripoti
hizo na Wenyeviti wa kamati Bw. Mussa
Zungu (Almasi) na Bw. Dotto Biteko (Tanzanite).
“Kesho saa 4.30 asubihi nitaziwasilisha ripoti hizi kwa Mheshimiwa
Rais Dkt. Magufuli. Hakuna ucheleweshaji katika jambo hili na Mheshimiwa Spika
(Job Ndugai) kesho twende tukakabidhi wote.”
Waziri Mkuu amesema kamati
hizo zimefanya kazi nzuri na kwamba Serikali inaimani na ripoti hizo na ushauri uliotolewa utawezesha
Taifa kunufaika na rasilimali zake, hivyo mapendekezo na hoja zote
zilizoibuliwa zitafanyiwa kazi katika kipindi kifupi.
Amesema taarifa hiyo zimewasilishwa
katika kipindi muafaka na zimeonyesha
dhamira ya dhati ya Bunge, kuunga
mkono juhudi za Rais Dkt. Magufuli
na Serikali yote kwa ujumla katika kulinda rasilimali za Taifa.
“Watanzania ni mashahidi kwamba Mwenyezi Mungu ameijalia
Tanzania utajiri wa rasilimali za kila aina.
Tunayo ardhi yenye rutuba, madini ya aina mbalimbali na mengine
hayapatikani katika nchi nyingine isipokuwa Tanzania tu kama vile Tanzanite.”
Amesema ni lazima
rasilimali hizo zisimamiwe na kutunzwa vizuri ili ziwezeshe kuboresha hali na
maisha ya Watanzania wote na kila mwananchi ana jukumu la kuunga mkono jitihada
za Serikali katika kuleta mageuzi katika Sekta ya madini nchini.
Waziri
Mkuu amesema suala la kusimamia rasirimali za nchi ni la Watanzania wote kama
ilivyoainishwa kwenye ibara ya 27 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania, ambapo aliinukuu Ibara hiyo kama ifuatavyo:
“27
(1) kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na
Wananchi na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.
“(2)
Watu wote watatakiwa na Sheria kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya nchi na pamoja
vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu na kuendesha uchumi wa Taifa na
kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya
baadaye ya taifa lao.”
Kamati
hizo zilipewa jukumu la kutathmini mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na
udhibiti wa madini ya Tanzanite na Almasi Nchini, ambazo zimeishauri Serikali
kuhusiana na mfumo bora wa uendeshaji na udhibiti wa biashara ya Tanzanite na
Almasi nchini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S.L.P 980,
40480-DODOMA
JUMATANO, SEPTEMBA 6, 2017.
No comments:
Post a Comment