WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepiga marufuku tabia ya baadhi ya viongozi
katika maeneo mbalimbali nchini
kuwakamata na kuwaweka ndani watumishi wakiwemo wauguzi bila ya kufuata
taratibu.
Pia amewataka wauguzi nchini kufanya kazi kwa weledi, uaminifu pamoja na
kufuata maadili ya taaluma yao kwa kuwa maisha ya wagonjwa yako chini yao.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Oktoba 04,
2017) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa 45 wa Chama cha Wauguzi
Tanzania, mkoani Lindi.
“Naagiza viongozi wote kufuata na
kuzingatia sheria. Kama kuna makosa ya kitaaluma, Mabaraza husika yashughulikie
jambo hilo na ni marufuku kuwaweka ndani watumishi kwa tuhuma za kitaaluma.”
Amesema kwamba katika sekta ya afya bila
wauguzi ambao ni kundi kubwa kati ya Wanataaluma wa Afya, Serikali haitaweza kutekeleza
ipasavyo mikakati mbalimbali iliyopangwa kwa ajili ya kuboresha sekta hiyo.
Katia hatua nyingine Waziri Mkuu amewaasa wauguzi wote nchini kuhakikisha wanazingatia kiapo
cha maadili ya kazi yao na kwamba Serikali haitamvumilia yeyote atakae bainika kwenda
kinyume.
“Nanyi Wauguzi mnao wajibu wa kutoa
huduma kwa wananchi kwa kuzingatia kiapo na miiko ya taaluma yenu. Tunazo
taarifa kuhusu baadhi ya Wauguzi kutoa lugha chafu kwa wagonjwa, kuomba rushwa
na wengine kujihusisha na vitendo vya wizi wa dawa.”
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha afya za
Watanzania wote zinaimarika ili kuendana na kasi ya utendaji kazi wa Serikali ya
kuinua uchumi na kufikia wa kiwango cha kati, hivyo ni lazima watoe huduma bora
kwa wananchi.
Pia amewaomba waunge mkono kwa nguvu zote jitihada
za Serikali katika kuhakikisha miundombinu na vifaa vyote havihujumiwi na watu
wachache ili viwe msaada mkubwa hususani kwa akina mama wajawazito ili wajifungue
salama.
Akizungumzia kuhusu upungufu wa wauguzi nchini,
Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo
Wauguzi na Wakunga na kuwapanga katika maeneo yenye upungufu zaidi.
Awali, Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Khamis Kigwangalla alisema baadhi
ya viongozi katika maeneo mbalimbali wamekuwa wakiwakamata na kuwachukulia
hatua watumishi wa Sekta ya Afya bila ya kufuata taratibu, jambo ambalo si
sahihi.
Mkutano huo umehudhuriwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Kigwangalla, Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania Bw. Paul Magesa, Mbunge wa
Lindi Mjini Bw. Hassan Kaunje, Mbunge wa
Kuteuliwa Mama Salma Kikwete(MB) Viti
maalum.
Wengine ni Mkurugenzi
wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Bw. Gustav Moyo, Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania
Bw. Stewart Mbelwa.
Wengine ni Mbunge wa Viti Maalumu, Hamida
Abdallah, Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya Uuguzi Bw. Ndementria Vermund, Rais
wa Chama cha Madaktari Tanzania Dkt. Obadia Nyongole na wawakilishi wa wauguzi kutoka mikoa
yote nchini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, OKTOBA 04, 2017.
No comments:
Post a Comment