NA JANETH JOVIN
UTAFITI kuhusu hali ya misimamo mikali uliyofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) umebaini kuwa hapa nchini kunaviashiria na chembehembe za misimamo mikali na kama haitadhibitiwa mapema kunauwezekano wa kupoteza amani iliyopo sasa.
Utafiti huo ambao umefanywa mwaka huu katika mikoa mitatu ya Tanzania bara ambayo ni Tanga, Mtwara na Pwani umebaini kuwa sababu kubwa ya uwepo wa misimamo hiyo ni manung’uniko waliyokuwa nayo wananchi kuhusu kukosa huduma za kijamii na ukosefu wa ajira.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Kaimu Mkurugenzi Mtendji wa LHRC, Anna Henga, alisema utafiti huo pia umebaini sababu nyingine zinazopelekea uwepo wa misimamo hiyo hapa nchini ni uelewa duni wa wananchi kuhusu haki za kiraia na kibinadamu kwa ujumla.
Alisema ingawa hali ya misimamo hiyo kwa hapa nchini haijafikia viwango vya nchi nyingine ni bora kujikinga na kuzuia isiweze kusambaa na kusababisha kupotea kwa amani tuliyonayo na kuongeza kuwa kama tutashindwa kudhibiti hali hiyo miongoni mwa athari zitakazotokea ni vifo, kuharibika kwa miundombinu na wakati mwingine huweza kupelekea kuporomoka kwa uchumi wa nchi kwani wawekezaji hawawezi kuwekeza katika taifa lisilokuwa na amani.
“Kwa kutumia matokeo ya utafiti huu, LHRC tunaona kuwa ni vyema kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na wananchi katika kukomesha vitendo hivi vya misimamo mikali inayopelekea kuwa na vurugu kali ambazo huleta mtikisiko katika jamii, ili kuweza kupambana na vurugu zitokanazo na misimamo hiyo wananchi wanapaswa kujenga uaminifu kwa vyombo vya usalama kwa kushirikiana navyo katika kupambana na vitendo hivyo,”alisema.
Aidha alisema vyombo vya usimamizi wa sheria kama Jeshi la Polisi vinapaswa kudumisha dhana ya kushirikisha jamii badala ya kutumia mguvu kupita kiasi katika kukabiliana na uhalifu.
No comments:
Post a Comment