WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka
Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro kuwakamata, Bw. Bahman wa kampuni ya
NAS na Wakala wa Kampuni ya Wallmark Bw. Samwel kwa kutaka kutoa bandarini
magari makubwa aina ya semi tela 44 bila ya kulipa kodi kwa kutumia jina la
Waziri Mkuu.
Pia Waziri Mkuu ameitaka
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kufanya kazi kwa mujibu wa sheria
na kutowasikiliza wafanyabiashara wanaotaka kukwepa kodi kwa madai ya kupewa
vibali vya msamaha wa kodi kutoka kwa viongozi wa juu Serikalini.
“Mtu asije hapa aseme
amepewa kibali na Rais Dkt. John Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu
Hassan au Waziri Mkuu cha kutaka kutoa mzigo wake bila ya kufuata taratibu.
Akija mtu na taarifa hizo akamatwe mara moja na achukuliwe hatua kwa mujibu wa
sheria.”
Ametoa agizo hilo leo
(Jumatano, Novemba 29, 2017) alipofanya ziara ya ghafla bandarini baada ya kupata
taarifa za mfanyabiashara huyo aliyetaka kuutapeli uongozi wa TPA kutaka kutoa
magari hayo yaliyoingizwa nchini mwaka 2015 kutoka nchini Uturuki.
Hatua hiyo imekuja baada ya
Bw. Bahman wa kampuni ya NAS kutaka kupata msamaha wa kodi kwa kuidanganya TPA kwa madai kwamba
wamewasiliana na Waziri Mkuu na wasipotekeleza jambo hilo watapata matatizo.
Amesema Serikali inasisitiza
watu kufuata sheria na taratibu za nchi ikiwa ni pamoja na kulipakodi ipasavyo na inataka watendaji wake wafanye
kazi bila ya kubugudhiwa, hivyo amewataka wafanyabiashara kufuata sharia za
nchi na kwamba Serikali haina ugomvi nao.
Waziri Mkuu amefafanua kuwa mfanyabiashara
huyo alitaka kuyatoa magari hayo bila ya kukamilisha malipo ya ununuzi kutoka
kwenye kampuni Serin ya nchini Uturuki.
“Magari haya aliyalipia
asilimia 30 tu kwa makubaliano ya kumaliza asilimia 70 iliyobaki baada ya
kufika Tanzania na atakapokamilisha ndipo angepewa nyaraka ambayo inaonyesha
jina la mwenye mzigo, aina ya mzigo na thamani
(bill of lading) inasaidia
mteja kufanyiwa tathmini ya gharama za kulipia ushuru, lakin huyu bwana
hajafanya hivyo”
Waziri Mkuu amesema kitendo
cha kuyasajili magari hayo bila ya kuwa na nyaraka hizo ni kinyume cha sheria
na pia kinaweza kusababisha kampuni iliyouza magari hayo ya Serin kutolipwa
malipo yaliyobaki.
Amesema jambo hilo
halikubaliki kwa sababu linaweza kudhohofisha mahusiano mazuri iliyopo kati ya
Tanzania na Uturuki kwani tayari kampuni hiyo imeshawasilisha malalamiko hayo
katika ofisi za Ubalozi wa Uturuki nchini Tanzania.
“Uturuki wanawaamini sana wafanyabiashara
wa Tanzania sasa huu ujanjaunja uliotumika katika Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) na kuyasajili magari haya bila ya kuwa na bill of lading halisi unajenga sura mbaya kwa wafanyabiashara
wengine waaminifu na watiifu wa sheria nawaagiza TRA kuchukua hatua kwa
wahusika, hatuwezi kupoteza mahusiano na nchi kwa sababu ya utapeli wa
mfanyabiashara mmoja.”
Pia Waziri Mkuu ametoa wito
kwa Mawakala wa Forodha kuhakikisha wanakuwa makini katika kazi zao na Serikali
haitawavumilia wababaishaji kwani inasisitiza wafanyabiashara kulipa kodi kwa
mujibu wa sheria na si vinginevyo.
Awali, Mkurugenzi wa Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit
Kakoko alimueleza Waziri Mkuu kuwa pamoja na vitisho vya mfanyabiashara huyo kuwa
wasipotekeleza matakwa yake watapata matatizo, lakini waliendelea kusimamia sheria
na taratibu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATANO, NOVEMBA 29, 2017.
No comments:
Post a Comment