KAMATI
ya Bodi ya Ligi Kuu ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao
chake cha Novemba 22, 2017 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya
Ligi kwa msimu wa 2017/2018 inayoendelea hivi sasa.
Klabu ya Tanzania
Prisons imepewa Onyo Kali kwa kuwakilishwa kwenye benchi na ofisa
tofauti na yule aliyeudhuria kikao cha maandalizi (pre match meeting)
cha mchezo kati yake na Kagera Sugar uliofanyika Novemba 4, 2017 kwenye
Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Katika
kikao hicho, Prisons iliwakilishwa na Meneja wake Erasto J. Ntabah
lakini kwenye benchi alikaa Hassan Mtege. Adhabu ya Onyo Kali kwa klabu
hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu
Taratibu za Mchezo.
Pia
Erasto J. Ntabah amesimamishwa hadi suala lake la kutoka jukwaani na
kwenda kumfokea Mwamuzi wa Akiba litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu
ya TFF. Amesimamishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu kuhusu
Usimamizi wa Ligi.
Mchezaji
Benjamin Asukile wa Tanzania Prisons amefungiwa mechi tatu na kupigwa
faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu
na Mwamuzi kwa kosa la kumpiga kiwiko kwenye paji la uso mchezaji wa
Kagera Sugar.
Kocha
wa Azam FC, Aristica Cioaba amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya
sh. 500,000 (laki tano) kwa kuwafuata waamuzi na kuwalalamikia kwa
kurusha mikono akionyesha kutoridhika na maamuzi yao. Alifanya hivyo
kwenye mechi namba 69 ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Ruvu Shooting
iliyofanyika Novemba 4, 2017 kwenye Uwanja wa Azam Complex na adhabu
hiyo imezingatia Kanuni ya 40(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha.
Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza, Klabu
ya Mvuvumwa imepigwa faini ya sh. 100,000 (laki moja) kwa timu yake
kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mechi dhidi ya African Lyon ikiwa na
maofisa pungufu, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi
Daraja la Kwanza. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi
Daraja la Kwanza. Mechi hiyo ilifanyika Novemba 7, 2017 kwenye Uwanja wa
Uhuru jijini Dar es Salaam.
Mtunza
Vifaa wa timu ya JKT Mlale, Noel Murish amesimamishwa hadi suala lake
la kuwamwagia maji washabiki wa Polisi Tanzania litakaposikilizwa na
Kamati ya Nidhamu ya TFF. Uamuzi wa kumsimamisha ni kwa mujibu wa Kanuni
ya 9(5) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Usimamizi wa Ligi. Alifanya
kitendo hicho katika mechi hiyo iliyochezwa Novemba 4, 2017 kwenye
Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.
Klabu
ya Coastal Union imepewa Onyo Kali kutokana na timu yake kuhudhuria
kikao cha maandalizi ya mechi ikiwa na maofisa pungufu, kitendo ambacho
ni kinyume na Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza. Adhabu hiyo ni
kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza. Ilifanya hivyo
katika mechi dhidi ya JKT Mlale iliyofanyika Novemba 12, 2017 katika
Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Nayo
Klabu ya JKT Mlale imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa
kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi hiyo. Adhabu hiyo ni
kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza.
JKT
Mlale imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya KMC
kumchezesha nahodha wake Stephano Mwasika katika mechi namba 28
iliyofanyika Oktoba 30, 2017 kwenye Uwanja wa Azam Complex wakati akiwa
anatumikia adhabu ya kadi nyekundu.
Mwasika
alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kiwiko mpinzani
wake kwenye mechi namba 15 kati ya KMC na Mbeya kwanza iliyochezwa
Oktoba 5, 2017 katika Uwanja wa Azam Complex.
Baada
ya kupata kadi hiyo, Mwasika alitakiwa kukosa mechi tatu na kulipa
faini ya sh. 300,000 (laki tatu). Mechi alizotakiwa kukosa ni dhidi ya
Mufindi United (Oktoba 15), Polisi Tanzania (Oktoba 23) na JKT Mlale
(Oktoba 30). Alikosa mechi mbili tu za kwanza, lakini akacheza mechi ya
tatu dhidi ya JKT Mlale iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Klabu
ya Toto Africans imepewa Onyo Kali kutokana na timu yake kuchelewa
kikao cha maandalizi (pre match meeting) katika mechi dhidi ya Biashara
United Mara iliyofanyika Novemba 5, 2017 kwenye Uwanja wa Nyamagana
jijini Mwanza. Adhabu hiyo ni utekelezaji wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi
Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
Meneja
wa Toto Africans, Yusufu Jumaa amefungiwa miezi miwili na kupigwa faini
ya sh. 200,000 (laki mbili) baada ya kuondolewa na Mwamuzi kwenye
benchi la ufundi kwa kupinga maamuzi yake na kumshambulia kwa maneno.
Ofisa
Habari wa Toto Africans, Cuthbert Japhet amesimamishwa hadi suala lake
la kummwagia maji Mwamuzi na kumjeruhi kwa kitu chenye ncha kali wakati
wa mapumziko katika mechi hiyo litakaposilikizwa na Kamati ya Nidhamu ya
TFF.
Waamuzi
Wasaidizi Jumanne Njige wa Mwanza na Bam Bilasho wa Dodoma wamepewa
Onyo Kali kwa kuchezesha chini ya kiwango mechi namba 36 ya Kundi C kati
ya Transit Camp na Rhino Rangers iliyofanyika Novemba 11, 2017 katika
Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya
38 (5) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.
No comments:
Post a Comment