HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 25, 2017

Wahandisi watakiwa kuwa waadilifu, wawajibikaji

MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amewataka wahandisi na watu wote ambao wanasimamia sekta hiyo kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na uaminifu katika kazi zao ili kuchochea Tanzania ya uchumi wa kati.

Mbarawa aliyasema hayo jana wakati wa hafla ya kukabidhiwa Tuzo ya Heshima ya Rais wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA), iliyotolewa kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS),Mhandisi Patrick Mfugale.

Alisema wahandisi wengi hasa wanajihusisha na ujenzi wa miundombinu wanakosa uaminifu, uadilifu na uwajibikaji hali ambayo inachangia ubovu katika miradi wanayosimamia.

Waziri alisema uamuzi wa JICA kumpa tuzo ya heshima Mfugale ni jambo la kupongezwa na la kuigwa na wataalam mbalimbali hasa katika sekta ya ujenzi.

“Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba wahandisi wenzako waige mfano wako katika kazi ili nao siku moja waweze kupata tuzo hii ya heshima ya JICA ambayo umeipata kutokana na jitihada zao katika kusimamia majukumu yako,” alisema.

Waziri Mbarawa alisema tangu aingie katika wizara hiyo amekuwa akijifunza mambo mengi kupitia kwa Mfugale hivyo anaamini tuzo hiyo imetolewa kwa mtu sahihi.

Akizungumza katika hafla hiyo Mwakilishi Mkazi wa JICA, Toshio Nagase alisema shirika hilo limetoa tuzo hiyo kwa Mfugale kutokana na uwajibikaji wake kwenye sekta ambayo anaisimamia.

“Hii ni tuzo ya 13 ya Rais wa JICA ambayo ni ya utambuzi wa heshima kwa watu binafsi wataalam, wataalam washauri, wafanyakazi wa kujitolea na miradi kwa mchango wao wa kufanikisha katika Nyanja za rasilimali watu na Mfugale amefanya hilo,” alisema.

Alisema katika tuzo hiyo ya heshima ya Rais wa JAICA ya mwaka huu watu binafsi 26 kote duniani wamepata mmoja wapo akiwa Mfugale kutoka Tanzania, vikundi sita miradi tisa na wafanyakazi wakujitolea watatu.

Nagase alisema mchango wa Mfugale katika miundombinu umeanza tangu mwaka 1977 wakati alipoajiriwa wizara ya ujenzi kama mtaalam msaidizi huku akisimamia miradi ya JAICA tangu mwaka 2007.

Kwa upande wake Balozi wa Japani nchini Masaharu Yoshida alisema uamuzi wa JAICA kutoka tuzo hiyo kwa Mfugale ni ishara tosha kuwa Tanzania inaushirikiano mzuri na Japani.

Yoshida alisema nchi yake itaendelea kusaidia Tanzania katika sekta mbalimbali huku akiwata wasimamizi wa miradi mingine ambayo inapata msaada wa JIICA kuuiga mfano wa Mfugale.

Akizungumzia tuzo hiyo Mhandisi Mfugale alisema ameipokea kwa heshima kunbwa huku akiweka bayana kuwa tuzo hiyo inatokana na mchango mkubwa wa wizara, wafanyakazi wenzake na JAICA kwa ujumla.

Mtendaji mkuu huyo wa TANROADS aliwataka wafanyakazi wenzake kuongeza jitihada kazini ili siku nyingine tuzo hiyo ya heshima ya Rais wa JAICA wapewe wao.

“Siamini kuwa nina kitu cha ajabu ila naamini kuwa ushirikiano baina yetu ndio mafanikio yangu hivyo ni wakati muafaka kwa kila mmoja kusimamia eneo lake kwa faida ya nchi na wananchi,” alisema. Mfugale alisema iwapo kila mmoja atasimamia nafasi yake kikamilifu upo uwezekano wa Tanzania ya viwanda kufikiwa ifikapo 2025 kama lilivyolengo la Serikali na Rais John Magufuli.

No comments:

Post a Comment

Pages