OFISI
ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema kuwa mkoa wa Njombe unaongoza kuwa na
idadi kubwa ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi ambapo ni asilimia
11.4 ya watu hao huku Zanzibar wanaoishi na virusi hivyo ni chini ya
asilimia 1.
Takwimu
hizo zimetolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa katika
maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika viwanja
vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Dk
Chuwa amesema mkoa wa Lindi umekuwa wa mwisho kwa watu wenye virusi
vya ukimwi na idadi ya asilimia 0.1 huku maambukizo kwa Jiji la Dar es
Salaam yamepungua hadi kufikia asilimia 4.7 ikiwa na maana watu 133,971
wanaishi na ugonjwa huo.
Mkurugenzi
huyo amesema kwa ujumla watu 1.4 milioni nchini Tanzania wanaishi na
virusi vya Ukimwi na takwimu hizo ndiyo rasmi hivyo asitokee mtu au
kikundi cha watu kupotosha.
"Nasema
kwa sababu kuna watu wanakurupuka na kuja na takwimu zao. Naomba
watambue takwimu ni fani kama fani nyingine na zina miiko yake," amesema
Dk Chuwa
Hata
hivyo, Dk Chuwa amesema Serikali haimzuii mtu au kikundi kufanya
utafiti ila ni lazima awasiliane na ofisi ya takwimu wapitie dodoso zake
kabla ya kuruhusiwa kufanya.
Amesema
atakayekiuka na kupotosha takwimu adhabu yake iliyowekwa kisheria ni
kifungo cha miaka mitatu au faini Sh10 milioni au vyote kwa pamoja.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Watu wanaoishi na virusi vya
Ukimwi, Justin Mwinuka ameiomba Serikali kutengeneza Sheria
zitakazoratibu upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya ukimwi (ARV).
Mwinuka
amesema uwepo wa sheria hiyo utasaidia kuwabana watu wanaofanya
biashara kupitia dawa hizo.Amesema wagonjwa wengi hawapati dawa kutokana
na kushindwa kumudu gharama.
"Tuna changamoto ya uhaba wa dawa na zinazopatikana zinauzwa sasa wagonjwa wanashindwa kupata fedha za kununua,"
Mwinuka
pia ameomba watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kuingizwa kwenye mpango
wa kaya maskini Tasaf ili waweze kutatua changamoto ya uhakika wa
lishe.
No comments:
Post a Comment