Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Kaimu
Mtendaji Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali ya Reli (RAHCO), Masanja Kadogosa
(kushoto), kuhusu kusimamia kwa karibu mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa
(Standard Gauge), wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo katika
kijiji cha Soga Mkoani Pwani na Ngerengere mkoani Morogoro.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto), akimsikiliza Kaimu
Mtendaji Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali ya Reli (RAHCO), Masanja Kadogosa
(kulia), alipomweleza hatua za ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa (Standard
Gauge), wakati Waziri huyo alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo Mkoani
Pwani.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akichanganya zege katika moja
ya Makalvati yanayojengwa katika mradi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge),
katika eneo la Kisarawe alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo Mkoani
Pwani.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati), akibonyeza kitufe
cha kuruhusu zege kwenda kwenye kalvati linalojengwa kwenye Reli ya Kisasa
(Standard Gauge), wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo Mkoani
Pwani.
Tingatinga likiendelea na kazi ya kuchenjua tabaka
la chini la Reli ya Kisasa (Standard Gauge), katika eneo la Soga, Mkoani Pwani. Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
xxxxxxxxxxxxxxxxx
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa wito kwa
mkandarasi Yapi Merkezi na Motaengil Africa wanaojenga reli ya kisasa (Standard
Gauge Railway), kufanya kazi kwa uadilifu, kulingana na vipimo vilivyo kwenye
mkataba ili kuwezesha mradi huo kukamilika kwa wakati.
Aidha,
ameitaka Kampuni Hodhi ya Rasilimali za reli (RAHCO), kuhakikisha kuwa
inafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo kwani wananchi wamekuwa wakisubiri
kukamilika kwake na kuanza kupata huduma za usafiri wa treni zitakazorahisisha
shughuli zao za kibiashara na kijamii.
Akizungumza
leo mara baada ya kukagua mradi huo katika kijiji cha Soga mkoani Pwani, Waziri
Mbarawa amesema kuwa ameridhishwa na kasi ya wakandarasi hao na kuagiza
kuongeza spidi zaidi ili ifikapo mwaka 2020 mradi huo uwe umekamilika.
"Kasi
mnayoenda nayo sio mbaya, ila naomba RAHCO mhakikishe mnasimamia kwa karibu
kuhakikisha spidi inaongezwa ili kazi ikamilishwe haraka na kwa viwango",
amesema Profesa Mbarawa.
Akiwa
katika kijiji hicho, Waziri Mbarawa amemwagiza Kaimu Mtendaji Mkuu wa RAHCO,
Masanja Kadogosa, kukutana na uongozi wa kampuni hizo kujadili na kuangalia
fursa za upatikanaji wa ajira kwa watanzania hususan wakazi wa eneo inapopita
reli hiyo.
Kwa
upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa RAHCO, Masanja Kadogosa, amesema mpaka sasa
mradi huo upo ndani ya muda na kumhakikishia Waziri Mbarawa kuwa mradi
utakamilka kwa wakati kwani kazi inayofanyika sasa ni kuweka zege kwa ajili ya
ujenzi wa boksi kalvati ambapo kazi hiyo inaendelea vizuri.
Ameongeza
kuwa katika kipindi hiki mradi ulisuasua kutokana na changamoto za mvua za
vuli, hivyo amefafanua kuwa wana mpango wa kuongeza kambi nyengine nane upande
wa Soga na nane upande wa Ngerengere ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa
wakati.
Mradi
wa SGR unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza unahusisha ujenzi wa
reli kutoka Dar es salaam - Morogoro na ya pili itahusisha sehemu ya Morogoro
hadi Makutupora mkoani Dodoma pamoja na njia za kupishana ambapo kwa pamoja
itakuwa na urefu wa kilometa 722 na itajengwa kwa gharama ya shilingi Trilioni
7.1.
No comments:
Post a Comment