January 04, 2018

Lions Club kuendelea kuwasaidia wanamichezo walemavu

NA MWANDISHI WETU

KLABU ya Lions Kimataifa imetoa wito kwa Olipiki Maalum Tanzania (SOT)  na kueleza kwamba wamegundua  eneo la michezo ya walemavu wa akili ni sehemu kusaidiwa kwa hali na mali na kuahidi kuendelea kuisaidia katika maendeleo yao.

Akizungumza jana katika ufunguzi wa michezo hiyo, hafla iliyofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mwakilishi wa klabu ya Lions, Bakari Omari alisema baada ya kutafakari kwa kina wamegundua kwamba ni jukumu lao la moja kwa moja kuwasaidia walemavu wa akili katika michezo ili kuwasaidia kuondokana na unyanyapaa.

Omari alisema awali kabla ya kujitosa kusaidia walemavu hao  waliketi na kupitia historia ya michezo yao na kugundua kwamba inahitaji msaada zaidi kwa sababu ni eneo ambalo changamoto zake zinahitaji wadau ambao ndio kimbilio lao.

Mkurugenzi wa mipango na Maendeleo wa Olimpiki Maalum Afrika, Joe Mutue alitumia fursa hiyo kuishukuru Klabu ya Lions Kimataifa kwa kusaidia kuwashirikisha walemavu wa akili kutoka kambi ya wakimbizi wa Nyarugusu mkoani Kigoma ambao awali walitakiwa kushiriki michezo ya Taifa iliyofanyika Zanzibar kuanzia Desemba 7-10 kwenye  uwanja wa Amaan, ambao hawakushiriki kwa sababu ya kukosa ruhusa ya ushiriki wa michezo hiyo.

Mutue alisema Lions Club kabla ya kufanikisha safari ya wanamichezo hao 60 kutoka Nyarugusu  ambao watashiriki michezo na wengine 60 wa Wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni ambao watachuana katika michezo ya soka na riadha.

Mutue alisema kupitia michezo hiyo anawaomba wanamichezo kucheza kiungwana ili kupatikana wanamichezo ambao watashiriki michezo ya dunia  mwakani Abu Dhabi Falme za Kiarabu.

Kaimu Mwenyekiti  wa Olimpiki Maalum, Lightness Mbilla alisema mwaka 2018 umeanza vizuri kwa sababu ya ujio wa viongozi wakubwa wa Kamati hiyo na kueleza kwamba anaona Baraka za Mungu katika siku za usoni katika michezo ya walemavu wa akili.    

Mbilla alitumia fursa hiyo kuwashukuru Lions Club kwa mchango wao wa kuwasaidia wakimbizi kushiriki katika michezo hiyo ambako pia wasaidie maandalizi ya michezo ya dunia ambayo Tanzania inatarajia kuwakilishwa na wanamichezo 40.

Mbilla alisema pamoja na mchango wa Lions Club lakini wadau wengine wamejificha na kutoipa kipaumbele michezo hiyo  ambayo wanamichezo wake huleta medali nyingi tofauti na michezo mingine.

Aidha Mbilla alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kuwa na jicho la tatu kusaidia michezo ya walemavu wa akili ambao wanatakiwa kuwa na michezo mbalimbali ambayo itawasaidia wanamichezo hayo.

Kabla ya michezo hiyo kuanza, yalifanyika matukio kama kuwasha na kukimbiza mwenge wa Kamati hiyo pamoja na kupandisha bendera yake ambayo ni kiashiria cha ufunguzi wa michezo hiyo inayotarajia kuendelea kesho uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Pages