WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa njia ya kusafirisha
umeme wa kilovoti 220 kutoka Makambako hadi Songea na kuahidi kuwa Serikali
itaendelelea kuwasambazia umeme wananchi wote.
Ametoa ahadi
hiyo leo (Jumapili, Januari 7, 2018) wakati Akizungumza na wananchi wa eneo la
Unangwa nje kidogo ya mji wa Songea, mara bada ya kuweka jiwe la msingi kwenye
mradi wa ujenzi wa kituo cha kupozea umeme.
Waziri Mkuu
amesema ujenzi huo unaenda sambamba na ahadi ya Mheshimiwa Rais, Dk. John
Joseph Magufuli ya kuwataka Watanzania wapate umeme kwa urahisi. “Mheshimiwa Rais
ameshusha gharama za umeme kutoka sh. 380,000 hadi sh. 27,000. Zamani ulikuwa
unalipia fomu za kuomba umeme, sasa hivi nazo amesema zitolewe bure. Nguzo za
umeme zilikuwa zinatozwa sh. 150,000, sasa hivi amesema zitolewe bure,”
alisema.
Waziri Mkuu
amesema zamani mikoa ya Njombe, Iringa, Ruvuma, Songwe, Mtwara na Lindi ilikuwa
na matatizo sufu ya kupata umeme lakini hivi sasa mikoa ya Mbeya na Iringa
imepata suluhisho baada ya kukamilika kwa mradi wa umeme wa kilovoti 400 wa
kutoka Iringa hadi Shinyanga.
“Sasa hivi
tunaingia Njombe na Ruvuma na baadaye tutaenda Mtwara na Lindi,” alisema.
Alitumia fursa
hiyo kuwaomba wakazi wanaoishi jirani na mahali kituo hicho kinapojengwa, wawe
walinzi wakuu wa mali za mkandarasi ili mradi huo uweze kukamilika mapema. “Eneo
hili lina saruji, nyanya na nondo, si vema watu wachache wjiokeze na kuiba
vifaa vya ujenzi. Saidieni kulinda eneo hili, na mali za mkandarasi ili mradi
ukamilike kwa wakati,” alisisitiza.
Akitoa taarifa
ya ujenzi wa mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Titus Mwinuka
alisema mradi huo utakapokamilika utaunganisha vijiji 120 na wateja 22,700.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameweka jiwe la msingi
la ujenzi wa ofisi za TANESCO mjini Songea ambalo litagharimu sh. bilioni 2.27.
Ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Machi, 2018.
Akimkaribisha
kuzungumza na watumishi wa TANESCO na wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Waziri
wa Madini, Dk. Medard Kalemani alisema jengo hilo ni moja ya majengo makubwa saba
nchini ambayo yatakuwa makao makuu ya kimkoa ya TANESCO.
Majengo mengine
yatajengwa kwenye mikoa ya Singida, Kilimanjaro, Mtwara, Njombe, Pwani, Geita
na Kigoma. “Kukamilika kwa ofisi hizi haimaanishi wafanyakazi wakae ofisini na
kufaidi viyoyozi. Ni lazima waende nje kuwafuata wateja,” alisisitiza.
Dk. Kalemani alisema
chini ya mradi wa kusafirisha umeme wa kilovoti 220 kutoka Makambako hadi
Songea, Serikali imeamua kujenga vituo vya kupozea umeme huko Makambako, Madaba
na Songea ambavyo vitakamilika Agosti 30, 2018.
“Kukamilika kwa
mradi huo kutaiepusha TANESCO na mzigo mkubwa wa kutumia fedha nyingi kununua mafuta
mazito ambao pia utapunguza gharama za umeme kwa watumiaji. Kabla ya hapa,
TANESCO ilikuwa inatumia sh. milioni 900 kwa siku kugharimia mafuta hayo,”
alisema.
Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Kaimu MKurugenzi Mtendaji wa TANESCO,
Dk. Titus Mwinuka alisema ujenzi wa jengo hilo ambao umefikia asilimia 78, unatarajiwa
kukamilika ifikapo Machi 31, mwaka huu.
“Gharama za
ujenzi kwa jengo zima ni sh. bilioni 2.198 na gharama za mshauri ni sh. milioni
78 na gharama zote zinafikia sh. bilioni 2.276. Fedha hizi zimetolewa na
Serikali,” alisema.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI,
JANUARI 7, 2018.
No comments:
Post a Comment