May 11, 2018

MAJALIWA:TUPO TAYARI KWA FAINALI ZA AFCON 2019

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ipo tayari kwa maandaalizi  ya fainali za michuano ya Afrika ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 mwaka 2019.

Mashindano ya mpira wa miguu kwa Vijana wenye umri wa chini ya  miaka 17 AFCON yanayotarajiwa kufanyika mwakani nchini Tanzania.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Mei  10, 2018) wakati akijibu swali la Mbungewa Sumve Bw. Richard Ndassa katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni Jijini Dodoma.

Katika swali lake Bw. Ndassa alitaka kujua Serikali imejipangaje kufanikisha mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) kuipa Tanzania uenyeji wa fainali hizo.

“Maandalizi ya fainali hizo yanaendelea vizuri, hivyo nawaomba Watanzania wenzangu tuendelee kuziunga mkono timu zote zinazofikia mashindano ya kimataifa ili ziweze kufanya vizuri”.

Waziri Mkuu amesisitiza kwamba “ni jukumu letu kuziandaa timu zote ambazo zinashiriki mashindano ya kimataifa ili ziweze kuibuka na ushindi.”

Hata hivyo amesema analishukuru Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na maandalizi yanaendelea ikiwa ni pamoja na kuipeleka timu nchini Sweden.

Pia Waziri Mkuu amesemaWizara ya Maliasili na Utalii itatumia mashindano hayo kwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.“Tutawapeleka Kilwa wakaone majengo ya zamani yaliyokaliwa na Waarabu na maeneo mengine.”

Waziri Mkuu amewasihi Watanzania kutumia fursa ya mashindano hayo yanayotarajia kufanyika nchini kwa kufanya shughuli mbalimbali zitakazowaongezea kipato.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI, Mei 10, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages