May 03, 2018

MALALAMIKO YA YANGA DHIDI YA MBEYA CITY YATUPWA

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati ya Saa) katika kikao chake cha Mei 1, 2018 chini ya Mwenyekiti wake Bw. Clement Sanga ilipitia matukio mbalimbali ya Ligi Kuu ya Vodacom, na malalamiko ya klabu za Yanga na Arusha FC na kuyafanyia uamuzi.

 Kamati imekataa malalamiko ya Yanga kutaka ipatiwe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu dhidi ya Mbeya City kwa timu hiyo kuwa na mchezaji zaidi kwenye mechi, kwa vile hakuna Kanuni yoyote ya Ligi Kuu inayoweza kubadili matokeo ya uwanjani kwa mazingira hayo.

Hakuna namna yoyote ile mchezaji anayezidi (extra player) kubadili matokeo ya mchezo. Katika mazingira ya extra player likifungwa bao, Mwamuzi atalikataa bao hilo. Kutokana na kanuni za Ligi kutojitosheleza katika suala hilo la extra player, Kamati iliangalia Kanuni za FIFA na kufikia uamuzi huo.

Mchezaji Ramadhan Malima wa Mbeya City ambaye alitolewa nje kwa kadi nyekundu, lakini akatoka kwenye chumba cha kuvalia (dressing room) kwenda kushangilia bao la kusawazisha la timu yake amesimamishwa hadi suala lake litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu TFF. Uamuzi wa kumsimamisha umezingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu kuhusu Usimamizi wa Ligi.

Kwa upande wa waamuzi, kulikuwa na upungufu katika suala la kusimamia ubadilishaji wa wachezaji (substitution), hivyo Kamati ya Waamuzi ya TFF imeandikiwa barua ili ichukua hatua dhidi ya wahusika. 
 
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati ya Saa) katika kikao chake cha Mei 1, 2018 chini ya Mwenyekiti wake Bw. Clement Sanga ilipitia matukio mbalimbali ya Ligi Kuu ya Vodacom, na malalamiko ya klabu za Yanga na Arusha FC na kuyafanyia uamuzi.

Mechi namba 199 (Mbeya City 1 vs Yanga 1). Klabu ya Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na vurugu za washabiki wake ikiwemo kurusha mawe na chupa uwanjani katika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 22, 2018 kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu.

Kwa vile mchezaji Obrey Chirwa wa Yanga alionywa kwa kadi ya njano kwa kosa la kumsukuma mchezaji wa Mbeya City ingawa kwenye picha za televisheni inaonekana kama alipiga kiwiko, Kamati haikutoa adhabu nyingine kwa vile tayari ameadhibiwa.

Hata hivyo, klabu ya Yanga imeandikiwa barua kuhusu kumuonya mchezaji huyo kwa vile kumbukumbu zinaonyesha ameshafanya matukio ya utovu wa nidhamu mara kadhaa akiwa uwanjani.

Mechi namba 178 (Simba 1 vs Yanga 0). Mchezaji Kelvin Yondani wa Yanga amesimamishwa hadi suala lake la kumtemea mate Asante Kwasi wa Simba katika mechi hiyo iliyochezwa Aprili 29, 2018 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF.

Adhabu ya kusimamishwa imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu kuhusu Usimamizi wa Ligi.

Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Manara amepewa Onyo Kali kwa kuingia uwanjani kushangilia ushindi wa timu yake baada ya mchezo kumalizika. Kitendo chake ni ukiukwaji wa Kanuni ya 14(11) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo, na adhabu dhidi yake imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

MALALAMIKO YA ARUSHA FC
Kamati imeipa Arusha FC ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya African Sports kuchezesha wachezaji wawili waliotumia leseni za kughushi (non qualified) katika mechi ya Kundi B Ligi Daraja la Pili (SDL) kati ya timu hizo iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Uamuzi huo dhidi ya African Sports umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(17) na 42(23) za Ligi Daraja la Pili. Nayo Arusha FC imepewa ushindi kwa kuzingatia Kanuni ya 14(36) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Taratibu za Mchezo. 

Vilevile viongozi wa African Sports waliohusika kughushi leseni zilizotumiwa na wachezaji hao ambao hawakusajiliwa watafikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya TFF kwa ajili ya hatua zaidi.

IMETOLEWA NA BODI YA LIGI KUU TANZANIA

No comments:

Post a Comment

Pages