May 26, 2018

MSIKIMBILIE KUUZA UFUTA - WAZIRI MKUU

*Aonya wakulima wasiwauzie chomachoma, ataka wasubiri minada
 *Akabidhi mikopo kwa akina mamalishe na babalishe

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa (pichani) amewaonya wakulima wa ufuta wasikimbilie kuuza zao hilo kwa wanunuzi wasio rasmi maarufu kwa jina la chomachoma bali wasubiri minada itangazwe mwezi ujao.

“Ninawasihi msikubali kuuza kwa akina chomachoma bali tumieni Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani, tumeona mfumo huu ulivyosaidia kwenye korosho,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo (Ijumaa, Mei 25, 2018) wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua uwanja mpya wa michezo unaojengwa katika kijiji cha Dodoma, kata ya Nachingwea, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.

“Kuna wawakilishi wa Kampuni ya Hyseas International Investment (T) Limited ya kutoka China ambao wamekuja hapa kuonana na uongozi wa Halmashauri. Wamesema watanunua ufuta wote uliolimwa Ruangwa na Nachingwea, ndiyo maana ninawasihi msubiri, msikimbiile kuuza ufuta kwa sasa,” alisisitiza.

Alisema kampuni hiyo imeahidi kuweka vituo vya ununuzi kwenye kata za Mandawa, Nanjaru, Nangurugai, Machang’anja hadi Mbangala ili wakulima wasihangaike kusafirisha ufuta wao. “Tunataka mwaka huu, wakulima wa ufuta nao wapate hela nzuri,” alisema.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amekabidhi mikopo kwa wajasiriamali 42 wanaofanya kazi zao wilayani Ruangwa ambapo kati yao akinamama lishe ni 39 na akinababa lishe ni watatu.

Mkurugenzi wa kampuni ya Ruangwa Distributors ambayo imetoa mikopo hiyo, Bw. Abdallah Mang’onyola alisema wajasiriamali 30 kati ya 42, wamepokea mikopo ya sh. 200,000 na 12 waliobakia wamepokea mikopo ya sh. 250,000.

Alisema wajasiriamali hao wanatoka kwenye kata saba za Matambalale, Narung’ombe, Mbekenyera, Chibula, Namichiga, Mandawa na Nambilanje.

Akizungumza na wajasiamali hao pamoja na wnanchi waliofika kwenye hafla hiyo fupi, Waziri Mkuu alimshukuru Mkurugenzi wa Ruangwa Distributors kwa kutoa mikopo hiyo yenye masharti nafuu na isiyo na riba.

Waziri Mkuu alisema hii ni mara ya pili kwa wajasiriamali wa Wilaya hiyo kupatiwa mikopo. Alitumia fursa hiyo kumshukuru Bw. Mpaluka Hashim Mtopela wa kampuni ya Sasalema ambaye awali alitoa mikopo ya sh. milioni 25 kwa wajasiriamali 89.

 IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, MEI 25, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages