May 10, 2018

SERIKALI YATOA SIKU TATU KWA WALIOFICHA MAFUTA NA SUKARI

*Yasisitiza kamwe haitokubali kuchezewa na wafanyabiashara wasiowaaminifu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku tatu kwa wafanyabiashara na wenye viwanda vya mafuta ya kupikia na sukari nchini kuhakikisha bidhaa hizo zinaendelea kupatikana katika maeneo yote na katika bei ya kawaida.

“Natoa siku tatu kuanzia kesho Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi mafuta yote yaliyoko bohari yaondolewe yaendelee kusambazwa kama kawaida nchini kote ili kuondoa uhaba uliojitokeza na kamwe Serikali haitokubali kuchezewa na wafanyabiashara wasiowaaminifu,”

Ametoa agizo hilo leo jioni (Jumatano, Mei 9, 2018) Bungeni Jijini Dodoma mara baada ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage kutoa kauli ya Serikali kuhusu uhaba wa mafuta ya kupikia nchini.

Amesema kama uhaba wa bidhaa hiyo utaendelea, ifikapo Jumapili Serikali itaanza kufanya msako kwenye viwanda na maghala na kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kuficha mafuta hayo.

Waziri Mkuu amesema takwimu zinathibitisha kwamba mafuta ya kupikia yaliyoingizwa nchini yanatosha, hivyo nchi haipaswi kuwa na uhaba. Amesema kwa mwezi mafuta yanayotumika nchini tani 28.9 na kila mwezi zinaingizwa tani 30,000. 

“Hatuwezi kukubaliana na jambo hili kwa sababu haliko kwa bahati mbaya ni mpango uliopangwa kwani imekuwa ni kawaida kila tunapoelekea kwenye Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kunakuwa na upungufu wa bidhaa hasa sukari, hivyo Serikali haitakubali wananchi wateseke bila sababu za msingi,” amesisitiza. 

Akiwasilisha kauli ya Serikali Bungeni, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Mwijage alisema vyanzo vinavyotumika kuzalishia mafuta nchini vinatosheleza mahitaji kwa asilimia 30, hivyo asilimia 70 ya mafuta huagizwa kutoka nje ya nchi.

“Miezi mitatu ya mwanzo kwa mwaka huu kuanzia Januari wastani wa mafuta yaliyoingizwa ni tani 30,210.71 kwa mwezi na jumla ya akiba ya mafuta yaliyopo nchini ni wastani wa tani 68, 902, hivyo hakuna upungufu,” alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMATANO, Mei 9, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages