May 26, 2018

TUJIEPUSHE NA VITENDO VYA CHUKI – WAZIRI MKUU

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir wakati alipowasili kwenye ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius  Nyerere jijini Dar es salaam kuwa mgeni rasmi katika Mashindano ya Kitaifa ya Kuhifadhi Quraan Tukufu yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Kiislam ya Istiquaama Tanzania, Mei 26, 2018. (Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir akizungumza katika Mashindano ya Kitaifa ya kuhifadhi Qur-aan Tukufu  yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Kiislam ya Istiquaama Tanzania.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Mashindano ya Kitaifa ya kuhifadhi Qur-aan Tukufu.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Kombo Faki Hamadi kutoka Pemba zawadi ya Shilingi milioni 4 baada ya kuibuka  kuwa mshindi wa kwanza wa Juzuu 30 katika Mashindano ya Kitaifa ya Kuhifadhi Qur-aan Tukufu  yaliyofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius  Nyerere jijini Dar es salaam, Mei 26, 2018. Katikati ni Mwenyekiti wa  Jumuiya ya Kiislam ya Istiquaama  Tanzania (Istiqaama Muslim Community of Tanzania), Seif Ali Seif. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mwenyekiti  wa  Jumuiya ya Kiislam ya Istiquaama  Tanzania ( Istiqaama Muslim Community of Tanzania), Seif Ali Seif.
 Baadhi ya washiriki wa Mashindano ya Kitaifa ya kuhifadhi Qur-aan Tukufu.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana  na baadhi ya viongozi wa  Taasisi na Jumuiya za Kiislam waliohudhuria katika Mashindano ya Kitaifa ya kuhifadhi Qur-aan Tukufu.

Dar es Salaam, Tanzania-WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka waumini wa dini ya Kiislamu wajiepushe na vitendo vinavyoweza kupandikiza chuki dhidi yao au kwa waumini wa dini nyingine.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Mei 26, 2018) wakati akizungumza na viongozi na mamia ya waumini wa dini ya Kiislamu walioshiriki mashindano ya kitaifa ya kuhifadhi Quran tukufu kwenye ukumbi wa Mwl. J. K. Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Kiislamu ya Istiqaama Tanzania (Istiqaama Muslim Community of Tanzania), yalijumuisha washiriki 29 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani.

“Serikali inatambua na inathamini sana, mchango wa dini katika kuwalea waumini kiimani na kutunza amani ya nchi. Hivyo, tujiepushe na kauli au vitendo ambavyo vinaweza kupandikiza chuki na uhasama dhidi yetu au dhidi ya waumini wa imani nyingine,” amesema.

“Nitoe rai kwenu viongozi wangu na waumini wenzangu, tujenge misingi ya kuvumiliana na kustahamiliana. Hilo pekee ndilo linaloisimamisha nchi yetu kuwa ni mfano wa kuigwa na kimbilio la wale waliovurugikiwa na amani katika nchi zao. Kadhalika, amani inajenga na kutoa fursa ya kuweza kutekeleza majukumu yetu ya kiibada, kiuchumi na kijamii bila hofu,” amesema.

Waziri Mkuu amesema kwa mujibu wa Surah Al-Imraan Ayah 103, Allah Mtukufu alihimiza umuhimu wa umoja miongoni mwa Waislamu. “Katika umoja huo, Allah amesisitiza Waislamu kuwa wamoja na kutofarakana. Mafundisho na wasia wa Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam ni kuwa tupendane na tushikamane. Wakati wote Mtume wetu aliheshimu na kuwathamini watu wote hata ambao hawakuwa Waislamu,” ameongeza.

“Kwa msingi huo, kama Waislamu nasi ni vema tukajipamba na tabia njema za Mtume wetu Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam. Katika hili, mtakubaliana nami kuwa tabia njema ni miongoni mwa makusudio muhimu sana ya kuletwa Mtume Muhammad kwetu,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuwapa elimu watoto kama ambavyo imesisitizwa kwenye Quran tukufu na kama ambavyo imesisitizwa na mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW) kwamba suala la kutafuta elimu ni la lazima kwa muislamu, awe mwanaume au mwanamke.

“Kama mnavyofahamu, Uislamu umeweka mkazo mkubwa sambamba na kusisitiza umuhimu wa elimu. Hili linathibitishwa na aya ya kwanza kabisa ya Quran kuteremshwa kwa Bwana Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam (SAW) ambayo ilimuamrisha kusoma (Surah Al-’Alaq ayah 1).”

“Kwa msingi huo, kama ambavyo mnatoa msukumo kwa vijana wetu kusomeshwa Quran, msukumo huo huo muutoe pia katika kuhakikisha kuwa vijana hawa wanapatiwa mafunzo sahihi kuhusu tabia njema, utii na kuheshimu mamlaka za utawala zilizopo. Kwa kufanya hivyo, tutawasaidia vijana hawa kuwa raia wema na wazalendo kwa nchi yao,” amesema.

Amesema Quran licha ya kuwa ni kitabu cha dini lakini kimebeba masuala yote muhimu katika maisha ya muislamu ya kila siku. “Hivyo, ukitaka kuleta maendeleo ya uchumi ulio imara, ukitaka kujenga jamii inayoheshimu na kufuata misingi ya uadilifu, ukitaka kujenga Taifa lenye amani na utulivu, huna budi kuwekeza zaidi katika elimu. Kwa hiyo, uwekezaji katika elimu haumaanishi tu kuhakikisha watoto wetu wanasoma na kuhifadhi Quran pekee, bali pia wanapaswa kupewa fursa ya kujifunza elimu ya mazingira ili waweze kufikia hatua bora za kimaisha duniani na akhera,” amesema.

Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubei alisema mashindano hayo yamefana na imeshangaza kuona mtoto anatajiwa namba tu ya aya na anaweza kuielezea kuwa iko kwenye sura fulani.

Kama ambavyo nabii Yahya aliamriwa kushika kitabu, nasi pia tushike kitabu na tuyashike yaliyo ndani yake, tusije kuishi katika ardhi yenye rutuba na yenye rasilmali madini halafu na sisi tushindwe kuvuna kile kilichomo,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiaya ya Istiqaama Tanzania, Sheikh Seif Ally Seif alisema jumuiya hiyo yenye matawi 20 Tanzania Bara na Visiwani, ilianzishwa mwaka 1993 kwa lengo la kutoa mafunzo ya kiroho na kuwajengea vijana maadili mema ili Taifa liwe na watu wenye kujali amani, wanaoheshimiana na kupendana kidugu.

Alisema jumuiya hiyo imejenga shule 14 za msingi na sekondari kwenye maeneo mbalimbali nchini na inatarajia kujenga shule kubwa ya kimataifa jijini Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na kufungua shule ya ufundi.

Katika mashindano hayo, kijana Kombo Fakhi Hamad (19) kutoka Istiqaama Pemba aliibuka mshindi wa jumla kwa kuweza kuhifadhi juzuu 30 na kupewa zawadi ya sh. milioni nne. Kombo pia aliibuka mshindi wa kwanza kwenye kundi la kuhifadhi juzuu 30 (tahfidh) akifuatiwa na Ally Said Mohamad (18) aliyepata sh. milioni mbili. Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Mariam Nassor Said (14) aliyepata sh. milioni 1.5.

Katika kundi la kuhifadhi juzuu 30 (tashdia), Masoud Bakari Ally (18) alikuwa mshindi wa kwanza na alipewa zawadi ya sh. milioni moja akifuatiwa na Mustafa Abdallah Hamad (17) aliyepata sh. 700,000 na wa tatu alikuwa Jumaa Ally Othman (16) aliyepata sh. 500,000.

Katika kundi la kuhifadhi juzuu 20, mshindi wa kwanza alikuwa Hilal Khamis Hamad (14) aliyepata sh. milioni 2.5 akifuatiwa na Ally Suleiman Ally (15) aliyepata sh. milioni 1.3 na mshindi wa tatu alikuwa Salim Khamiis Juma (15) aliyepata sh. milioni moja.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, MEI 26, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages