June 14, 2018

TAMUFO YAMTUNUKU DK.MREMA TUZO YA HESHIMA

 Rais wa Umoja wa Muziki Tanzania (TAMUFO), Dk. Donald Kisanga (kushoto),akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kumkabidhi Tuzo ya Amani, Heshima na Utumishi uliotukuka, Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole na Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Augustino Mrema (katikati) iliyotolewa na umoja huo katika hafla iliyofanyika nyumbani kwa Mrema Sinza jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Katibu wa TAMUFO, Stellah Joel.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole na Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Augustino Mrema (katikati), akimkabidhi sh.milioni 1.5 Katibu wa umoja, Stellah Joel alizizitoa kwa ajili ya kusaidia TAMUFO.
 Katibu wa umoja, Stellah Joel , akizungumza kwenye mkutano huo.
Rais wa Umoja wa Muziki Tanzania (TAMUFO), Dk. Donald Kisanga (kushoto), akimkabidhi Tuzo ya Amani, Heshima na Utumishi uliotukuka, Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole na Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Augustino Mrema iliyotolewa na umoja huo katika hafla iliyofanyika nyumbani kwa Mrema Sinza jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Katibu wa TAMUFO, Stellah Joel.

Na Dotto Mwaibale 

UMOJA wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) umemtunuku Tuzo ya Amani, Heshima na Utumishi Uliotukuka, Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya PAROLE, Dk. Augostine Lyatonga Mrema, kutokana na jitihada zake za kuhimiza umoja, utulivu na mshikamano. 

Dk. Mrema ambaye pia ni Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Naibu Waziri Mkuu katika kipindi cha awamu ya pili chini ya uongozi wa Mzee Alhaj  Ally Hassan Mwinyi, (Mzee Ruksa) alikabidhiwa tuzo hiyo na Rais wa TAMUFO Dk. Donald Kisanga. 

Akizungumza Dar es Salaam jana, mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Dk. Mrema aliwashukuru TAMOFO kwa kutambua mchango wake kwa Taifa katika kipindi ambacho alikuwa akiwajibika serikalini na kwenye jamii. 

Alisema ni muhimu kwa Taifa kutambua watu mbalimbali na hasa wazee waliofanya mambo mengi mema na mazuri kwa Taifa, badala ya kusubiri kutoa pongezi na shukrani wakati wa mazishi. 

Pia Dk. Mrema alitoa pongezi za kipekee kwa TAMUFO kutokana na uamuzi wao wa kuanzisha maombi maalum ya kuliombea Tiafa, akisema kazi hiyo ni muhimu na haipaswi kufanywa kwenye maeneo machache. 

“TAMUFO wameanzisha maombi maalum ya kuliombea Taifa kwa kushirikiana na wanamuziki wa Nyimbo za Injili nchini, lakini walianza kazi hiyo kule Ubungo Anglikana,” alisema Dk. Mrema. 

Aliongeza kusema kwamba, aliwaambia waandaaji wa matamasha hayo ya kuliombea amani Taifa, kutambua kazi kubwa inayofanywa na Dk. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo ni kubwa na muhimu. 

“Hivyo, nimewaomba wao TAMUFO na wadau wengine wakiwamo wafanyabishara, viongozi wa kada mbalimbali nchini, kuona umuhimu wa kuiunga mkono taasisi hiyo ili matamasha kama haya yaweze kufanyika nchini kote,” alisema Dk. Mrema. 

Alisema ikiwa TAMUFO itawezeshwa kuyafikia maeneo mengi nchini, itakuwa imesaidia kutuliza sintofahamu ya sasa ambapo baadhi ya watu bado hawajatambua nia njema ya Rais Dk. Magufuli, katika kuifanya nchi kuwa ya viwanda na yenye amani na utulivu kiuchumi.  

“Nitamfimkishia Mheshimiwa Rais Magufuli tuzo hii ya amani na ujumbe wake kwa Taifa,  ambayo nimepewa mimi binafsi kutambua mchango wangu kwenye nchi hii, lakini pia nashukuru kwa TAMUFO kutambua umuhimu huu,” alsema Mzee Mrema. 

Kwa upande wake Dk. Kisanga, alisema wazo la kumpatia tuzo hiyo Mzee Mrema, ilitokana na tamasha lililofanyika Jumapili katika kanisa la Anglikana Ubungo Jijini Dar es Salaam. 

Dk. Kisanga, alisema TAMUFO iliona kwa hatua za awali na katika kipindi  hiki ambacho Rais Magufuli na serikali yote ya awamu ya tano, amekuwa akisisitiza amani na mshikamano, wao waliamua kuanza mchakato wa kufanya matamasha ya aina hiyo kwa kuwashirikisha waimbaji wa nyimbo za injili. 

“Hivyo, tumempatia tuzo hii mzee Mrema, ambaye alifanyakazi kubwa kuanzisha vituo vingi vya polisi nchini, polisi jamii pamoja na ulinzi shirikishi nchini kote,” alisema Kisanga, na kuongeza kwamba mke wake mzee Mrema alitunikiwa cheti cha Shukran. 

Alisema katika kipindi hicho Mzee Mrema alikuwa tayari kukabiliana na mtu ama kikundi cha aina yeyote kinachohatarisha usalama wa nchi kwa kuwaita wahusika na kuzungumza nao ndani ya siku saba na matukio hayo kusimama mara moja,” alisema Dk. Kisanga. 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TAMUFO, Stella Joel, alisema na kumshuikuru Mzee Mrema kwa mchango mkubwa alioutoa kwa Taofa kipindi cha utumishi wake. 

Lakini pia Stella, alisema kwenye tamasha hilo la kuombea amani ya nchi, Mzee Mrema aliahidi kuchangia kiasi cha Sh. Milioni 1.5 kwa TAMUFO kuendelea na matamasha ya kuombea amani nchini pamoja na kumtakia afya njema Rais. 

“Tumekabidhiwa tayari kiasi hicho cha fedha na Mzee Mrema, hivyo tunawaomba na kutoa wito kwa wadau wa maendeleo, haki na amani ya nchi kuungana naye mzee Mrema kufikia malengo ya kuwaunganisha wananchi kwenye matamasha ya aina hii.

No comments:

Post a Comment

Pages