June 05, 2018

WAZIRI MKUU AMPONGEZA STEVEN MASELE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika Mheshimiwa Stephen Masele na kumuahidi kwamba Serikali itampa ushirikiano ili aweze kutimiza majukumu yake.

Ametoa ahadi hiyo leo (Jumanne, Juni 5, 2018) wakati akizungumza na Mheshimiwa Masele ofisini kwake Bungeni, Dodoma. Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza kwa kuchaguliwa kushika wadhifa huo.

Amesema ushindi wake katika nafasi hiyo umelipa heshima kubwa Bunge na Serikali na kwamba wana matarajio makubwa kwa sababu uwepo wake, utaliongezea Taifa ushirikiano na nchi nyingine za Afrika.

"Matarajio kwa Bunge ni makubwa kwani kuna mambo ambayo tunataka ushirikiano na nchi nyingine za Afrika, hivyo uwepo wako ni muhimu katika kufanikisha utekelezaji wake."

Vilevile, Waziri Mkuu amewapongeza wabunge wengine wawili, Waheshimiwa David Silinde na Asha Abdullah Juma kwa ushirikiano wao uliochangia ushindi wa Mheshimiwa Masele.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Masele ambaye ni Mbunge wa Shinyanga Mjini, ameishukuru Serikali kwa ushirikiano iliyompa na hatimaye kuibuka na ushindi huo.

Amesema ushindani ulikuwa mkali kutokana na uwepo wa mataifa mengi yaliyokuwa yakiwania nafasi hiyo. Aliahidi kutetea maslahi ya Taifa kwa muda wote atakaotumikia nafasi hiyo. “Nakuhakikishia Waziri Mkuu kwamba nitayalinda na kuyatetea maslahi ya Tanzania kwa muda wote ambao nitakuwa katika wadhifa huu,” alisema Mhe. Masele.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMANNE, JUNI 5, 2018.

No comments:

Post a Comment

Pages