June 05, 2018

CMSA YATOA MAFUNZO KWA WATENDAJI KATIKA MASOKO YA MITAJI

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji ya Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama, akizungumza katika mafunzo ya  watendaji  katika masoko ya mitaji ikiwa ni utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kisera, kisheria na kiutendaji unaofanywa na CMSA.
Meneja Mahusiano wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji ya Dhamana (CMSA), Charles Shirima, akizungumza katika mafunzo ya  watendaji katika masoko ya mitaji ikiwa ni utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kisera, kisheria na kiutendaji unaofanywa na CMSA.
Washiriki wa mafunzo hayo.
  Washiriki wa mafunzo.
Meneja Mahusiano wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji ya Dhamana (CMSA), Charles Shirima, akizungumza katika mafunzo ya  watendaji katika masoko ya mitaji ikiwa ni utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kisera, kisheria na kiutendaji unaofanywa na CMSA.
Picha ya pamoja.

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Masoko na Mitaji ya Dhamana (CMSA) imewaasa watendaji katika masoko ya  Mitaji kuhudhuria mafunzo yanayotambulika katika viwango vya kimaitafa ili kupata ujuzi na kuwa wabobezi katika masoko ya kimaitafa.

Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji ya Dhamana (CMSA) Nicodemus Mkama, katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya Watendaji katika Masoko ya Mitaji (SICC) iliyoendeshwa kati ya CMSA na Taasisi ya Uwekezaji na Dhamana (CISI) ya nchini Uingereza.

Alisema chini ya kifungu namba 32 cha Sheria ya Masoko ya Mitaji ya 1994 kama ilivyorekebishwa mwaka 2010, mtu yeyote anayetaka kutoa huduma katika masoko ya mitaji kama Dalali wa Soko la Hisa, Mwakilishi wa Dalali wa Soko la Hisa, Mshauri wa Uwekezaji, Mwakilishi wa Mshauri wa Uwekezaji, Mshauri Mteule, Mwakilishi wa Mshauri Mteule au mtendaji yeyote katika masoko ya mitaji ni lazima apitie mafunzo yanayotolewa na CMSA na kufaulu.

Mkama alisema lengo la sharti hilo ni kuhakikisha kuwa watendaji na wataalamu katika masoko ya mitaji wanakuwa na ujuzi stahiki katika utoaji wa huduma za masoko ya mitaji ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri katika uuzwaji wa dhamana kwa umma na uorodheshwaji wake kwenye masoko ya hisa.

"Tangu kuanzishwa kwake, CMSA imekuwa ikitoa mafunzo hayo na mpaka sasa zaidi ya watalamu 560 wamefuzu," alisema. 

Alisema katika utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki, (East African Common Market Protocol), Taasisi za Usimamizi wa Masoko ya Mitaji za Afrika (EASRA) zilipitisha na kukubaliana kuwa watendaji wanaotaka kutoa huduma katika masoko ya mitaji ya Afrika Mashariki ni lazima wapitie mafunzo na kufaulu mtihani unaotambulika kimataifa.

"Hivyo utaona kuwa hii ni moja ya utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kisera, kisheria na kiutendaji unaofanywa na CMSA ili kuwezesha masoko ya mitaji kuwa na watendaji wengi wenye ujuzi na weledi wa kukuza uwekezaji kupitia masoko ya mitaji na hivyo kuchochea ukuaji wa sekta ya fedha, hususani masoko ya mitaji na uchumi hapa nchini," alisema

Alisema ukanda wa wa Afrika Mashariki unaendesha mafunzo hayo kwa kufuata mitaala inayoshabiana ikiwemo kushirikiana na CISI.

Mkama alisema lengo la kozi hiyo ni kuandaa watendaji na watalamu wa masoko ya mitaji wenye utaalamu na ujuzi wa viwango vinavyoendana na kasi ya maendeleo na mabadiliko yanayotokea katika huduma za masoko ya mitaji kimataifa, hivyo kuleta weledi na ubobezi katika masoko.

"Mafunzo haya yanajumuisha washiriki 64 ikiwa ni washiriki 24 zaidi ya lengo la washiriki 40. Mwitikio huu unatokana na ongezeko la uelewa na uhitaji wa wataalamu wa masuala ya masoko ya mitaji hapa nchini," alisema Mkama.

Aidha alisema kwamba wahitimu watapata fursa ya kuomba leseni ya kutoa huduma katika sekta ya masoko ya mitaji kwa ngazi za kimataifa.

Hatahivyo alisema kwamba CMSA itaendelea kushirikiana na wadau kujenga mazingira bora, wezeshi na endelevu yenye lengo la kuendeleza na kukuza masoko ya mitaji nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages