WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanasiasa
wakiwemo mawaziri na wabunge wawahamishe Watanzania kuendeleza utamaduni wao.
Ametoa wito huo leo (Jumatano, Julai 18, 2018)
wakati akizungumza na wazee na wananchi wa Makunduchi mara baada ya kushuhudia
maadhimisho ya sikukuu ya Mwaka-Kogwa yaliyofanyika Makunduchi, wilaya ya Kusini,
mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
“Mawaziri wote, tuna dhamana ya kuwahamasisha
Watanzania waendeleze utamaduni ili uwe ni jambo hai. Wabunge na wawakilishi
tukiwa kwenye majukwaa, tusisitize Watanzania waendeleze utamaduni,” amesema.
Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania (SMT) pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zinasimamia uwepo
wa utamaduni na zenyewe zinaongozwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo imelenga
kuihamasisha jamii kuuenzi, kuulinda na kuudumisha
utamaduni wa Mzanzibari na kushiriki katika uandaaji wa matamasha 50 ya utamaduni.
“Lazima utamaduni uendelezwe ndani na nje ya
nchi na ni lazima tufanye jitihada tuwarithishe watoto utamaduni wetu. Kwa
mfano, hapa Zanzibar mnalo tamasha la ZIFF, lile ni la kimataifa, vyombo vya
muziki ni vya kisasa. Ni vema sasa, tukaangalia uwezekano wa kuwa na tamasha la
huku chini ambalo litatumia ala za muziki za asili,” alisema.
Akizungumzia sherehe za Mwaka Kogwa, Waziri Mkuu
alisema hii ni mara yake ya kwanza tangu azaliwe kuona watu wakichapana viboko si
kwa ugomvi wala chuki, bali wakiwa na furaha.
“Mwaka Kogwa ni utamaduni wetu, pande zote za
visiwani na zimekuwa zikifanyika kila mwaka lakini hivi sasa ni Makunduchi peke
yake ambao mmeweza kuendeleza utamaduni huu, wengine wameacha kuadhimisha sherehe
hizi,” amesema.
“Tanzania tuna makabila zaidi ya 120 wenye tamaduni
na mila tofauti lakini si wote ambao wanaenzi mila na tamaduni zao. Utamaduni
ni jambo muhimu nchini, utamaduni ni fursa ya kiuchumi kwa sababu watalii
wanatoka kwao kuja Zanzibar kuangalia tukio kama hili, ni lazima tuuenzi,”
alisisitiza.
Wakati huohuo,
Waziri Mkuu amewapongeza wakazi wa Makunduchi kwa kutunza na kuhifadhi
mazingira na amewataka waendeleze bidii ya kuyatunza.
“Kati ya mambo ambayo nimeyapenda sana, ni
tabia yenu ya uhifadhi mazingira. Lazima niwapongeze wana-Makunduchi kwa
kutunza na kuhifadhi mazingira. Kama msingekuwa watu wazuri mgeshafyeka misitu
yote, na kusingekuwa na mvuto kama nilivyoona. Endeleeni kuhifadhi mazingira yetu
ili yaweze kututunza,” alisema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Kusini, Bw. Hassan Khatib Hassan alisema wanafanya maadhimisho hayo ikiwa ni
sehemu ya kuendeleza utamaduni na kuonyesha urithi kutoka kwa wazazi wao. “Tunaendeleza
utamaduni huu sababu ni urithi kutoka kwa wazazi wetu. Ni upendo, amani na mshikamano,”
alisema.
Mapema, Mkuu
wa Wilaya ya Kusini, Bw. Idrissa Kitwana Mustafa alisema wamewaalika mabalozi
wa Uturuki na Iran kwenye maadhimisho hayo kwa sababu utamaduni huo pia
unafanyika kwenye nchi zao.
Akitoa shukrani
kwa niaba ya wananchi wa Makunduchi, Mwakilishi wa jimbo la Makunduchi, Bw.
Haroun Ali Suleiman alisema anaipongeza serikali ya awamu y atano kwa mambo
ambayo imeyafanya kwa kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
“Hakuna asiyeona, na kama mtu hataki kuona,
basi hataona kabisa. TUnaomba utufikishie salamu zetu kwa Mhshimiwa Rais
Magufuli,” alisema.
Alisema anaomba kuwe na ushirikiano wa karibu
baina ya watendaji wa wilaya ya Kusini na ile ya Ruangwa ambako Waziri Mkuu
anatoka ili watumishi wake waweze kubadilishana uzoefu na kuimarisha muungano.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, JULAI 18, 2018.
No comments:
Post a Comment