HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 24, 2018

Wafanyakazi wa NMB wanavyosaidia Jamii kupitia Mishahara yao

 Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd, akichangia damu kwenye hafla ya uchangiaji damu iliyoandaliwa na benki hiyo kanda ya Dar es Salaam. Zaidi ya chupa 250 zilikusanywa kutoka kwa wafanyakazi wa NMB, pia walichangia vitanda vya hospitali vyenye thamani ya Sh. Mil. 8 kwa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Muhimbili tawi la Mloganzila. (Na Mpiga Picha Wetu).
 Prof Said Aboud kutoka Chuo Kikuu cha Muhimbili akipokea msaada wa vitanda vya kutolea damu kutoka kwa Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd, wakati wa makabidhiano yaliyofanyika makao makuu ya NMB jijini Dar es Salaam. Wafanyakazi wa NMB walichanga sehemu ya mishahara yao na kununua vitanda 10 vyenye thamani ya shilingi milioni 8 na pia kujitolea kuchangia damu chupa zaidi ya 250.
 Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd, akitoa maelezo mafupi kwa Prof Said Aboud kutoka Chuo Kikuu cha Muhimbili kuhusu mchango wa wafanyakazi wa benki uliofanikisha kununua vitanda 10 vya kutolea damu vyenye thamani ya shilingi milioni 8 na pia uamuzi wa wao wenyewe kuchangia Damu chupa zaidi ya 250. Wengine ni Ofisa Tawala wa Kanda ya Dar es Salaam, Katengesya John na Meneja wa Tawi la NMB Ohio, Subira Kapita

Na Mwandishi Wetu
 
BENKI ya NMB imekuwa mstari wa mbele katika kuchangia huduma  za kijamii kwa lengo la kurejesha sehemu ya faida yake kwa wananchi. Mwishoni mwa wiki iliyopita Benki ya NMB ilikabidhi vitanda vya kuchangia damu na pia wafanyakazi kuchangia damu chupa zaidi ya 250. 

Mbali na sera ya benki ya NMB kuchagia jamii inayojikita kwenye elimu na afya, wafanyakazi nao wameamua kuanzisha utaratibu wa kuchanga fedha kutoka kwenye mishahara yao na kuchagua eneo lenye mahitaji na kutoa msaada.

Benki ya NMB imetenga zaidi ya shilingi bilioni moja kwaajili ya kusaidia jamii kwenye afya na elimu kwa mwaka huu – 2018, Wafanyakazi pia wamechangia zaidi ya shilingi milioni 600 kwa miaka mitatu (2016, 2017 na 2018) kwaajili ya kusaidia jamii inayowazunguka kwa njia ya kurudisha fadhira kwa jamii iliyowalea na kuwasomesha.

Akiongea kwenye hafla ya kukabidhi vitanda vyenye thamani ya shilingi milioni 8 kwa uongozi wa hospitali ya chuo kikuu Muhimbili tawi la Mlogazila, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam – Badru Idd  anasema wafanyakazi wameamua kujitolea fedha zao na kusaidia vifaa vya kutolea damu na pia wao wenyewe kushiriki kuchangia damu  ili kunusuru wagonjwa ambao wanaamini ni sehemu ya wateja wao.

Bwana Badru ameongeza kuwa mbali na kujitolea kuchangia damu, wafanyakazi hao wamejitolea michango na kufanikisha kununua vitanda 10 maalum kwa ajili ya kuchangia damu vyenye thamani ya shilingi milioni 8.“Suala la kujitoa tumekuwa tukilifanya mara kwa mara, lakini safari hii tulifikiria nini tukitoe kwa wananchi ndipo tukaona kuna haja ya kujitoa na kuchangia damu kwa wagonjwa ili kusaidia  kuokoa maisha ya wahitaji.”

Anasema utaratibu wa kurejesha sehemu ya mapato kwa wateja wao umekuwa ukifanywa pia na Benki kwa kujipangia kutoa  asilimia moja ya faida baada ya kodi kila mwaka na kuirejesha kwa jamii kupitia misaada kwenye sekta ya elimu na afya. 

Anasema NMB itaendelea kujitolea kwa jamii pale inapobidi, jambo ambalo imekuwa ikilifanya maeneo mbalimbali ya mikoa, kulingana na ilivyojitanua katika utoaji huduma zake.
Meneja wa Kitengo cha Uwabikaji kwa Jamii (CSR) cha benki ya NMB, Lilian Kisamba anasema msaada huo ni sehemu ya utaratibu wa wafanyakazi wa benki hiyo ambao wamejiwekea kusaida jamii yenye uhitaji wakisaidina na kitengo cha CSR.

Anaongeza kuwa wafanyakazi wa benki hiyo wamekuwa na utaratibu wa kusaidia jamii kupitia programu yao ya "staff initiative" ambao ni mpango uliokwa na kitengo cha uwajibikaji ili kusaida matatizo mbalimbali ambayo yanaikabili jamii. 

Hivyo wafanyakazi wa Kanda ya Mashariki wakisaidina na kitengo cha CSR walifanikiwa kuchanga shilingi milioni 13, ambazo zilikabidhiwa kwa uongozi wa Hospitali ya CCBRT ili kufanikisha upasuaji wa akina mama wenye fistula.

"Wafanyakazi wa NMB ndio wametoa pesa hizo kutoka mifukoni mwao lakini pia wanapata mchango kutoka kitengo cha uwajibikaji kuwaongezea pale walipotoa ili kufanikisha upasuaji kwa wanawake waliopo CCBRT." Anasema kiongozi huyo.

Kwa mwaka huu pekee benki ya NMB Tanzania kupitia Kitengo cha Masuala ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) ilichangia msaada wa vifaa vya hospitali, vifaa vya ujenzi wa madarasa pamoja na madawati katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Songwe pamoja na Mkoa wa Mara.

Mkoani Mwanza, benki hiyo ilitoa msaada wa madawati 60 kwa Shule ya Msingi Mwenge yenye thamani ya shilingi milioni tano ili kusaidia kupunguza uhaba wa madawati katika shule hiyo.

Huku mkoa wa Shinyanga, ukinufaika kwa msaada wa vifaa vya ujenzi ambavyo vilitumika kumalizia ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi Nyasubi iliyopo wilayani Kahama ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali ya Rais John Pombe Magufuli.

Kama hiyo haitoshi NMB ikajitolea pia msaada kwa Mkoa wa Songwe kwa kutoa vifaa vya hospitali vyenye thamani ya shilingi milioni tano ambavyo vilitumika katika Hospitali ya Wilaya ya Songwe Mwambani, vikiwa na lengo la kupunguza uhaba wa vifaa uliopo katika hospitali hiyo.

Hata hivyo juhudia za kushiriki uchangiaji wa huduma za jamii, umeisukuma NMB kutoa vifaa vya kisasa vya hospitali vikiwepo vitanda vya kujifungulia katika kituo cha Afya cha Mgango kilichopo wilayani Musoma, Mkoa wa Mara vyote vikifikia takribani shilingi milioni 15 za kitanzania.
“NMB tulikabidhi madawati 50 katika Shule ya Msingi Mwisenge, shule ambayo alisoma Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, yote yakiwa na thamani ya Shilingi milioni 5, pia tukatoa msaada Musoma Vijijini ambapo tulikabidhi vitanda vya kujifungulia na vitanda vya kulalia wagonjwa, jumla ya vitanda nane pamoja na mashine za Shinikizo la Damu (BP) katika Kituo cha Afya cha Mugango  zenye thamani ya Sh. 5 milioni,” anasema kiongozi huyo.

Hivi karibuni Benki ya NMB katika hafla ya uzinduzi wa Tawi jipya la NMB Pamba mkoani Mwanza ilitoa msaada wa vitanda 11 vikiwa na magodoro na mashuka yake katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana (Butimba) vyote vikiwa na thamani ya Shilingi Milioni 10 kwa ajili ya akinamama wajawazito na hivyo kupunguza adha ya kukosa malazi.

Kwa mkoa wa Dar es Salaam shule zilizonufaika hivi karibuni ni pamoja na Shule ya Sekondari Mikocheni iliyopo Manispaa ya Kinondoni iliyopokea msaada wa madawati na viti 50 vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 5, na Shule ya Msingi Karume iliyonufaika kwa kusaidiwa vifaa vya ujenzi kukaamilisha madarasa mawili ikiwa ni kuunga mkono changamoto za elimu bure kuongeza vyumba vya madarasa katika shule hiyo.

Pamoja na hayo sekta ya afya inaendelea imeendelea kunufaika katika misaada ya NMB, baada ya Wafanyakazi wa Benki ya NMB Tanzania Kanda ya Mashariki kutoa msaada wa Shilingi milioni 13 kwa Hospitali ya CCBRT ili kufanikisha upasuaji kwa wakinamama saba wenye ugonjwa wa Fistula.

No comments:

Post a Comment

Pages