Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji
cha Kangeme kwenye Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga, Julai 16,
2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
*Ni kwa upotevu wa dola za Marekani 21,000
*Ni kwa upotevu wa dola za Marekani 21,000
*Wakimbia mkutano baada ya wananchi kuzomea
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule awakamate viongozi wa Chama cha Msingi
cha Mkombozi kwa upotevu wa dola za marekani 21,000 za chama hicho.
"Wabebe hawa watu, wahoji waseme hiyo fedha iko
wapi na jambo la kwanza wailete hiyo fedha ya wakulima. Wakishindwa kurejesha
fedha, wawekwe ndani," amesema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Julai
16, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa kijiji cha Kangeme, kata
ya Ulowa katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama ambao alienda kuzindua
mpango wa Ushirika Afya na NHIF.
Waziri Mkuu amefikia uamuzi huo baada ya
kuwaita viongozi wa chama cha Mkombozi watoke hadharani na kubaini kuwa
hakuwepo hata mmoja. Inadaiwa kwamba walitoroka baada ya wananchi kuanza
kuzomea.
Kamanda Haule amewataja watuhumiwa hao kuwa ni
Mwenyekiti, Bw. Shilinde Abdallah na mhasibu wa AMCOS hiyo, Bw. Kulwa Shinzi
pamoja na wajumbe saba wa bodi ya chama hicho.
Akiwa katika tukio hilo, Mwenyekiti wa Chama Kikuu
cha Ushirika cha Kahama (KACU), Bw. Emmanuel Cherehani alisoma taarifa ya Chama
na alipotaja bei ya tumbaku kuwa ni nzuri, wananchi walimzomea kupinga kile
alichokisema. Bw. Cherehani alikuwa akitoa mafanikio ya chama hicho, na kusema
kuwa bei ya tumbaku ni nzuri.
Akitoa ufafanuzi kuhusu kadhia hiyo, Waziri wa
Kilimo, Dk. Charles Tizeba alisema kuna tatizo katika uteuzi (grading) wa
tumbaku kwani wakulima wanalima tumbaku nzuri lakini katika upangaji bei,
wanalipwa bei ndogo. “Kuna wakulima wanakidai chama cha Mkombozi kiasi cha dola
za Marekani ambayo ni madai ya tumbaku waliyoiuza tangu mwaka 2014.”
Akizungumza na wananchi hao, Waziri Mkuu alisema
Serikali imeamua kufufua ushirika kwa sababu ndiyo mkombozi wa wakulima.
"Tumeamua kurudisha ushirika aminifu kwa wakulima, na nirudie kutoa onyo
kwa viongozi waliopata dhamana ya kuongoza ushirika wasidhani kule wameenda
kupata ulaji.”
“Tunataka ushirika unaosimamiwa na viongozi
waaminifu. Kwenye ushirika kuna fedha na kuna mali za chama, kwa hiyo ni lazima
tupate viongozi ambao ni waaminifu,” amesema.
“Kwa mfano, hapa Ulowa wakulima wamekuwa
wakilalamikia kupewa bei ya chini wakati wakati wao viongozi wanabeba kile cha
juu na kuwaumiza wakulima. Kiongozi wa KACU kasoma taarifa hapa mkaanza
kuzomea, hiyo ni dalili tosha kwamba kuna tatizo la msingi,” amesema.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaasa
wakulima waachane na tabia ya kukopa pembejeo na kufunga mikataba na makampuni
ya ununuzi wa tumbaku na badala yake wajiwekee akiba ili msimu wa kilimo
ukianza wasirudie tena kukopa.
“Gharama za kulima ekari moja, kuweka dawa,
palizi na kuchoma haizidi sh. 150,000. Wewe amua unataka kulima ekari ngapi,
weka fedha zako kwenye akaunti usubiri msimu ujao. Kwenye hii biashara ya
tumbaku, ukitafuta mikopo utabakia kuwa maskini kwa sababu huna nguvu ya
kubishania bei. Wenzenu wanaolima korosho, wameacha kukopa na bei mnazisikia
kila mwaka zinapanda,” amesema.
“Ukiwa na mazao yako utaweza kubishana na
mnunuzi. Tanzania bei ya tumbaku iko chini sababu wakulima mmetufikisha hapo
kwa kupitia mikopo na mikataba na makampuni ya ununuzi. Kuanzia sasa
badilikeni, ili muweze kuinua bei ya zao hili muhimu, alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, JULAI 16, 2018.
No comments:
Post a Comment