HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 03, 2018

JOKATE MWEGELO AAPISHWA KUWA MKUU WA WILAYA YA KISARAWE

Mkuu Mpya wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, ameapishwa leo huku akipewa onyo kuepuka wapotoshaji.


Pamoja na Jokate, Zainab Kawawa naye ameapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo.

Jokate, ambaye aliwahi kuwa mlimbwende wa mashindano ya Miss Tanzania mwaka 2006, aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Julai 28 mwaka huu.

Jokate ameapishwa leo Agosti 3 huku ndugu, jamaa, marafiki na viongozi wa CCM wakihudhuria hafla hiyo.

Akizungumza mara baada ya wakuu hao wawili wa wilaya kuapishwa, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani, Ramadhani Maneno amewataka wateule hao waepuke wanaofika ofisini kutaka kuwapotosha katika utendaji wao.

Amewataka wakakae na makatibu tawala ili wakusanye mapato kwani mkoa wa Pwani una viwanda. “Kwa nafasi mlizopata hakikisheni mnakua karibu na viongozi wa chama hilo ni jambo kubwa. Wakati sasa mnaenda kuripoti kwenye wilaya mkaanzie kwenye ofisi za chama,”amesema.

Ameongeza: “Huko mnapoenda mtafute desturi na mila za maeneo yenu msizipuuzie, lakini mtafute yale yanayoendana na nyaraka zilizopo.”

Amesema anawakabidhi vitu vitatu, macho, masikio na mdomo ambavyo vitawasaidia kwenye utendaji wao wa kazi.

Pamoja na kuwepo kwa idadi ndogo ya waliohudhuria sherehe hizo za uapisho, hakuna msanii hata mmoja aliyeonekana.

Wengi walitarajia kuona wasanii wakijitokeza kwa wingi katika sherehe hizo kwa kuwa Jokate ni msanii wa filamu, muziki na ni mwanamitindo. 
 Mkuu Mpya wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, ameapishwa akila kiapo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Kibaha, Mhandisi Evarist Ndikiro.

Kiapo.

Mkuu Mpya wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, akisaini baada ya kula kiapo. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kibaha, Mhandisi Evarist Ndikiro.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, akipokea saluti mara baada ya kuapishwa kuwa mkuu wa wilaya hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, akipongezwa baada ya kuapishwa.

No comments:

Post a Comment

Pages