Serikali imesema inajiandaa
kuja na mbinu za kisasa zaidi za ukaguzi na ulinzi katika ukuta unaozunguka
migodi ya Tanzanite, Mirerani ili
kudhibiti utoroshaji wa madini hayo yanayopatikana Wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Madini Angellah
Kairuki tarehe 2 Agosti, 2018 wakati wa
mkutano wa hadhara ulishirikisha wamiliki wa migodi, wachimbaji, wauzaji na
wote wanaofanya shughuli zao za ndani ya ukuta huo.
Alisema, mabadiliko ya ujenzi
wa ukuta huo ni chanya ambayo yamelenga kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta ya
madini ili kuongeza mchango wa sekta husika katika pato la taifa.
Waziri Kairuki alieleza ili shughuli za uuzaji na ununuzi ziweze
kufanyika ndani ya eneo hilo, tayari Serikali imejenga sehemu maalum kwa ajili
ya shughuli hizo na kuongeza, “ baada ya
kukamilika jengo hilo kutakuwa na sehemu kwa ajili ya Broker kufanyia shughuli zao hapo hapo ndani ya ukuta.”
Aliongeza, tayari Mkataba wa
ujenzi wa Kituo cha kufanyia shughuli zote zinazohusu biashara ya madini ya
tanzanite kwa ujumla (One Stop Center) umekwishakabidhiwa na ndani ya muda
mfupi ujao, ujenzi wa jengo husika utaanza.
Akitoa ufafanuzi kuhusu
taratibu za kuingia na kufanya shughuli za uchimbaji ndani ya ukuta, Waziri
Kairuki alisema taratibu za ukaguzi zinalenga katika kudhibiti utoroshaji
madini na hivyo kuwataka wadau wote kutoa ushirikiano wakati wa zoezi la
ukaguzi katika ukuta huo na kuongeza kuwa, aina ya ukaguzi unaofanywa kwa sasa
ni wa muda mpaka hapo taratibu maalum za ukaguzi zitakapokuwa tayari.
Akitoa ufafanuzi kuhusu
wazawa wenye leseni za uuzaji kulipa ada kwa
kutumia Dola za Marekani, Waziri Kairuki alieleza kuwa, kwa kuwa Kanuni
za eneo la Mirerani zimeandaliwa na Waziri mwenye dhamana na sekta, suala hilo
litafanyiwa kazi ili kipengele husika kiweze kufanyiwa marekebisho na hivyo
kuwawezesha kulipia kwa fedha za Tanzania. Pia, aliongeza kuwa, katika kipindi
hiki ambacho mabadiliko hayo hayajafanyika, wahusika watalazimika kuendelea na
utaratibu uliopo.
Ili kuongeza kasi ya shughuli
ya uthamini wa madini hayo, waziri Kairuki alisema wizara yake itaongeza idadi
ya wataalam kutoka mmoja hadi wanne ili kuongeza kasi ya kufanya shughuli
husika.
Pia, Waziri Kairuki aliwataka
wamiliki wa migodi kuhakikisha wanakuwa na mikataba ya wafanyakazi katika
migodi yao na kuongeza kuwa, suala la maslahi ya watumishi ni jambo ambalo
linapaswa kupewa kipaumbele na wadau wote katika sekta husika.
“Maslahi ya wafanyakazi
yanatakiwa kuwa namba moja. Mimi ni Mbunge niliyechaguliwa kupitia umoja wa
vyama vya wafanyakazi hivyo suala la maslahi ya wafanyakazi lazima nilisimamie
kikamilifu,” alisisitiza Kairuki.
Akizungumzia suala la usafiri
ndani ya ukuta, alisema zoezi husika litaendelea kama ilivyo sasa na kutumia
fursa hiyo kukaribisha wawekezaji zaidi katika huduma ya kutoa huduma ya usafiri ndani ya ukuta huo.
Pia, alitumia fursa hiyo
kuwataka wadau wote katika eneo hilo kuwa waaminifu na kushirikiana na serikali
na hususan ofisi ya Madini katika kutoa taarifa za utoroshaji madini hayo.
Mwisho aliwataka Maafisa
Madini kuendelea kutoa elimu ya Sheria
ya Madini pamoja na taratibu zake pia, Mbunge wa eneo husika aendelee
kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa ukuta huo ili kuwawezesha
wadau wote kuwa na uelewa wa pamoja.
Kwa upande wake, Mbunge wa
Simanjiro James Ole Milya, alisema alimweleza Waziri Kairuki kuwa kero kubwa
katika eneo husika ni baina ya wamiliki wa migodi na wafanyakazi na hivyo
kumtaka Waziri kuona namna ya kushughulikia suala hilo.
Pia, alipendekeza kuundwa kwa
kamati mbili moja ikiwa ya wamiliki na wafanyakazi kwa lengo la kuondoa mvutano
uliopo sasa kati ya pande mbili.
Waziri
wa Madini Angellah Kairuki (katikati) akimsikiliza mmoja wa kina mama ambaye
anafanya shughuli zake ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite, Mirerani
wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika nje ya geti la ukuta huo.
Wanaofuatilia ni Mbunge wa Jimbo la Simanjiro James Ole Milya (kulia), Kamishna
wa Madini Mhandisi David Mlabwa
(kushoto) na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara wa kwanza kulia.
Waziri wa Madini
Angellah Kairuki akisisitiza jambo wakati akizungumza na katika mkutano wa hadhara na wananchi
wanaofanya shughuli zao ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite,
mirerani. Wanaofuatilia mbele ni Mbunge
wa Simanjiro James Ole Milya (kulia) na kushoto ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya
Simanjiro, Tumain Magesa.
Sehemu
ya wananchi waliofika katika mkutano wa hadhara ambao ulijumuisha wamiliki wa
migodi, wachimbaji, wauzaji, wanunuzi na wanaofanya shughuli mmbalimbali ndani
ya ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite, Mireran wakimsikiliza Waziri wa
Madini Angellah Kairuki, hayupo pichani.
Mkurugenzi
wa kampuni ya TanzaniteOne Faisal Juma
(kushoto) akiongozana na mmoja wa wafanyakazi ambaye aliwasilisha malalamiko
yake kuhusu kampuni hiyo kwa kwa Waziri wa Madini Angellah Kairuki wakati wa
mkutano wa hadhara. Anayefuatilia ni mmoja wa viongozi katika kampuni hiyo Hussein Gonga.
Mkurugenzi
wa kampuni ya TanzaniteOne Faisal Juma (kulia) na mmoja wa viongozi katika
kampuni hiyo Hussen Gonga (katikati) wakimsikiliza mmoja wa watumishi katika
kampuni hiyo wakati akiwasilisha malalamiko yake kwa Waziri wa Madini Angellah
Kairuki (hayupo pichani) wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika nje ya geti
la kuingilia katika ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite, mirerani.
Mbunge
wa Simanjiro, James Ole Milya akisititiza jambo wakati wa mkutano wa hadhara
uliofanyika kati ya Waziri wa Madini na wadau wa madini ya tanzanite wanaofanya
shughuli zao ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya Tanzanite, Mirerani.
Kaimu
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Tumain
Magesa akieleza jambo wakati wa mkutano wa hadhara kati ya Waziri wa Madini
Angellah Kairuki (hayupo pichani) na wadau wa madini ya tanzanite wanaofanya
shughuli zao ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite, mirerani.
Wanaofuatilia ni wawakilishi wa makundi mbalimbali ya wadau wanaofanya shughuli
zao ndani ya ukuta wakitaka kusilisha malalamiko yao kwa Waziri Kairuki.








No comments:
Post a Comment