Kamati
ya Maadili ya Uchaguzi Ngazi ya Taifa, imekitaka Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kiendelee kutekeleza maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya
Jimbo la Ukonga yaliyokitaka chama hicho kusahihisha makosa yaliyotendeka na kuomba
msamaha hadharani kwa kosa la kimaadili walilotenda.
Uamuzi
huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Jaji Mst. Mary Longway baada ya kikao
cha kamati hiyo kupitia na kujadili rufaa dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Maadili
Jimbo la Uchaguzi Ukonga, iliyowasilisha na Chadema Septemba 5, 2018 ikiitaka
kamati hiyo itengue uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Jimbo.
Alisema
kwa mujibu wa vielelezo vilivyoambatishwa katika Rufaa hiyo, Kamati ya rufaa
imefikia maamuzi ya kuwa rufaa hiyo imewasilishwa nje ya muda wa saa 48 kinyume
na maelekezo ya kipengele cha 5.7 (b)
cha Maadili tajwa.
“Rufaa
iliyowasilishwa yenye Kumb. Na. CDM/ILALA/MAADILI/2018/28 ya tarehe 5 Septemba,
2018 iliyopokelewa Tume tarehe 7 Septemba..Imewasilishwa nje ya muda wa saa 48
kinyume na maelekezo ya kipengele cha
5.7 (b) cha Maadili tajwa. Hivyo, Kamati inaelekeza kuwa mrufani aendelee
kutekeleza maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo.”, alisema Jaji Mst.
Longway.
Kwa
mujibu wa uamuzi wa Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo la Ukonga, Chadema kimeonywa
kuhakikisha kuwa kinafuata Kanuni na Taratibu za Maadili ya Uchaguzi wa Rais,
Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 na kutekeleza maamuzi hayo ndani ya saa 48
tangu kutolewa na adhabu hiyo.
Msimamizi
wa Uchaguzi Jimbo la Ukonga Jumanne Shauri mnamo Agosti 27, 2018 alipokea
malalamiko na kupitia utetezi wa Chadema na kujiridhisha kuwa Chadema kilitumia
kiongozi wa dini kumpigia kampeni mgombea wa chama hicho kinyume na kifungu cha
2.2 (k) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015.
Msimamizi
huyo wa Uchaguzi aliongeza kuwa “Dr. Makongora Mahanga akiwa kiongozi wa
Chadema, siku ya kampeni tarehe 25/8/2018 alitumia lugha ya matusi, kashfa,
kejeli na udhalilishaji dhidi ya mgombea wa CCM, ikiwa pia ni kinyume na
kifungu cha 2.2 (k) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya
mwaka 2015” aliongeza taarifa ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ukonga ambaye
ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Jimbo hilo”
Mbali
na uamuzi juu ya rufaa hiyo, Kamati hiyo pia imepitia barua ya tarehe 5
Septemba, 2018 iliyowasilishwa Tume tarehe 7 Septemba, 2018 kupinga maelekezo
ya Kamati ya Maadili Jimbo la Ukonga yaliyokiagiza Chadema kuwasilisha ndani ya
Saa 48 kuanzia tarehe 4 Septemba, 2018 vielelezo vilivyothibitishwa na Mamlaka
ya Mawasiliano na wataalamu wa lugha ya Kikurya ili kutoa maamuzi ya shauri
husika.
Akizungumzia
barua hiyo, Jaji Mst. Longway alisema baada ya kupitia vielelezo na kujadili
barua husika, imeamuliwa kuwa rufaa hiyo imekosa sifa kwa kuwa hakuna maamuzi
yaliyofanywa na Kamati ya Maadili Jimbo la Ukonga.
Kutokana
na jambo hilo, Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ya Taifa imekielekeza Chadema
kuwasilisha vielelezo Kamati ya Maadili ya Jimbo la Ukonga kwa uamuzi kama
ilivyoelekezwa na Kamati husika.
No comments:
Post a Comment