HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 13, 2018

Ndugu wakiri hakuna wizi JNIA

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (wa pili kushoto) leo akiongea na waandishi wa habari kuhusiana na shutuma za wizi wa pochi kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Pili la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBII).
  Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari leo wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (katikati mbele) alipokuwa akiongea nao kuhusiana na shutuma za wizi wa pochi ndogo ya abiria (jina limehifadhiwa) aliyesafiri Septemba 8, 2018 kuelekea Dubai. 
Bw. Wael Hassan (kulia) akiushukuru uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kwa kuonesha picha zilizopigwa na kamera za Usalama za tukio la kulalamikiwa kwa wizi wa pochi ya dada yake (jina limehifadhiwa), aliyesafiri tarehe 8 Septemba, 2018 akielekea Dubai. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela.

  Na Mwandishi Wetu

NDUGU wa abiria mmoja (jina limehifadhiwa) wamekiri baada ya kuoneshwa picha za kamera za usalama (CCTV) baada ya  ndugu yao aliyelalamika kwenye mitandao ya Kijamii kuibiwa pochi eneo la mwisho la ukaguzi la abiria wanaosafiri kwenda nje ya nchi,  iliyokuwa na fedha na vitambulisho mbalimbali, wakati akisafiri kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), akielekea Dubai.

Bw. Wael Hassan (mdogo wa mlalamikaji), ambaye ni Raia wa Tanzania mwenye asili ya Kiarabu, ametoa kauli hiyo leo kwenye Ukumbi wa mikutano wa Jengo la Pili la abiria la JNIA-TB2 katika Mkutano wa Waandishi wa Habari ulioitishwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuhusiana na taarifa hizo za shutuma za wizi.

Bw. Hassan anasema ameridhika na picha zote za kuanzia hatua ya kwanza ya ukaguzi na baadaye ukaguzi wa pili, na ameshukuru kwa Mamlaka kutumia fursa hiyo kupiga simu ambayo iliachwa na dada yake, kama moja ya njia ya mawasiliano endapo pochi yake ingepatikana afahamishwe kwenda kuichukua.

“Nimeona matukio yote ile jana nilivyoitwa na hata leo, na hakuna sehemu yeyote nimeona dada yangu ameibiwa pochi ndogo iliyokuwa ndani ya pochi kubwa alilokuwa amelitundika begani muda wote wa safari, maana mimi ndiye nilimsindikiza, lakini yeye (dada) ndio aliyesema ameibiwa sasa sijui ni wapi alipoibiwa ingawa pale checking point ya mwisho ameonekana hata hiyo pochi hajaitoa, ninashukuru sana,” amesema Bw. Wael.

Hatahivyo, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela amesema hawezi kukataa au kukubali juu ya wizi JNIA unaoripotiwa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari kwa kuwa kuna wafanyakazi ambao sio waaminifu, lakini wakibainika wanaondolewa mara moja kulingana na sheria, taratibu na kanuni za kazi na nchi.

“Sisi hatuwezi kukataa juu ya wizi na ndio maana tukasema bado uchunguzi unafanyika na tukaanza kwa kuangalia picha za CCTV na tukaona hakuna wizi wowote pale katika eneo aliposema ameibiwa, lakini bado vyombo vya kiusalama vilivyopo hapa kiwanjani vinaendelea na uchunguzi wa tukio hili, ambalo limeripotiwa kwenye mitandao ya kijamii na kusambaa kwa kasi duniani kote, ,” amesema Bw. Mayongela.

Pia Bw. Mayongela ameshukuru ndugu wa mlalamikaji kutoa ushirikiano kwa kuja na kutoa ushirikiano kwa kukubaliana na picha walizoziona juu ya ujumbe unaodaiwa kusambazwa na dada yao, kwenye mitandao ya kijamii, wakati akisafiri kurudi nyumbani kwake Falme za Kiarabu, baada ya mapumziko mafupi. Kwa mujibu wa Bw. Wael wanaishi maeneo ya Chang’ombe jijini Dar es Salaam.

Hatahivyo, Bw. Mayongela amesema sasa TAA inamkakati kamambe wa kuongeza kamera za Usalama kwenye viwanja vyote, ili kubaini matukio mbalimbali yasiyo ya kiusalama na wizi, na pia wafanyakazi wa Mamlaka na wa taasisi nyingine wanaofanya kazi kwenye viwanja vya ndege wameanza kufanyiwa uchunguzi ili kuwabaini wale wote wasio waaminifu na kuwaondoa mara moja kulingana na sheria, taratibu na kanuni za nchi na ajira. 

Bw. Mayongela ametoa wito kwa wananchi na watumia wa viwanja vyote vya ndege nchini, kuhakikisha wanafuata taratibu za kutoa taarifa kwa Afisa Usalama atakayekuwepo kwenye kiwanja husika na kutoa taarifa polisi endapo atakuwa anatatizo linalotakiwa kupatiwa ufumbuzi kabla ya kusafiri, na pia kujikagua kabla ya kufika eneo la kiwanja endapo atakuwa anakitu alichokisahau aidha nyumbani au kwenye gari iliyomleta.

Hatahivyo, kutokana na kadhia hiyo ya kuichafua taswira ya taasisi na nchi kwa ujumla, Bw. Mayongela amesema mlalamikaji anatakiwa kuomba radhi kwa njia ya maandishi na akishindwa kufanya hivyo, hatua zaidi za kisheria zitachukua mkondo wake, ikiwemo ya adhabu ya makosa ya kimtandao.

Kwa upande wa Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Afande Matanga Mbushi amesema kwa mwaka huu, imeripotiwa matukio mawili ya uwizi, na baada ya uchunguzi imebainika hakukuwa na uwizi wowote na baada ya abiria kulalamika amepoteza komputa mpakato na Ipad, na vilipatikana na amepatiwa.

“Huyu abiria wa pili alisema ameacha komputa mpakato eneo la Uhamiaji, lakini baada ya uchunguzi waligundua hakuwa nayo,” amesema Afande RPC Mbushi.

No comments:

Post a Comment

Pages