*Akerwa na tabia ya kupokea fedha na kutopeleka vifaa, dawa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema hataki kuona tabia ya kupokea fedha na kuchelewa kupeleka vifaa inayofanywa
na Bohari ya Madawa (MSD) ikiendelea.
“MSD ninawatahadharisha
wasirudie kosa la kupokea fedha na kutopeleka dawa na vifaa tiba. Ofisi zao
ziko hapo Dodoma mjini, ni kwa nini mnachelewa kuleta vifaa hivyo,” amehoji.
Ametoa onyo hilo leo
mchana (Alhamisi, Septemba 20, 2018) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya
Mauno, wilayani Kondoa ambako alienda kukagua ujenzi wa kituo cha afya na
kuelezwa kuwa MSD imekuwa ikichelewa kuleta dawa. Waziri Mkuu leo ameanza ziara
ya kikazi ya siku saba katika mkoa wa Dodoma.
Amesema Serikali ilitoa
sh. milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya na kwamba baada ya
ukaguzi ameridhika na kazi inayofanyika. Hata hivyo, amemtaka Mwenyekiti wa
Halmashauri hiyo pamoja na madiwani wahakikishe wanatenga fedha kwa ajili ya
ujenzi wa wodi mbili za wagonjwa wa kawaida wa kike na wa kiume.
“Hapa mna kituo cha afya,
hospitali ya wilaya iko Kondoa mjini ambako ni km.62 kutoka hapa. Tengeni fedha
za kujenga hizo wodi ili watu walazwe hapahapa. Halmashauri mnao uwezo wa
kujenga hizo wodi mbili. Nataka nione mnaanza na nipate taarifa kuwa mmeanza
ujenzi huo,” amesisitiza.
“Mwenyekiti wa
Halmashauri na madiwani kaeni na mfanye hiyo kazi. Nikisema muanze maana yake
ni kuanza. Tunataka wana-Mauno watibiwe hukuhuku na hakuna haja ya kuwasumbua wananchi
kwenda hadi Kondoa mjini. Mkimaliza ujenzi, mtuambie, tutaleta sh. milioni 250
za kununua vifaa vya ndani.”
Amesema Serikali
inaimarisha huduma za afya kwa kujenga zahanati na kuimarisha vituo vya afya
ambapo hadi kufikia Agosti mwaka huu, jumla ya vituo vya afya 209 vilikuwa
vimekwishajengwa hapa nchini.
Amesema kila mwezi,
Serikali inapeleka wilayani humo sh. milioni 25 kwa ajili ya ununuzi wa dawa
kuanzia hospitali ya wilaya, vituo vya afya na zahanati na akawaonya waganga na
wauguzi wasiziguse dawa hizo kwa sababu zimelenga kuwasaidia wananchi.
Mapema, akizungumza na wananchi hao, Naibu Waziri wa
Fedha, Dk. Ashatu Kijaji ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kondoa, aliishukuru Serikali
ya awamu ya tano kwa kuimarisha huduma za afya wilayani humo ambapo katika
kipindi cha miaka mitatu, wameweza kuwa na vituop vya afya vitano.
“Katika kipindi cha miaka
40, tulikuwa na vituo vya afya vitatu tu lakini ndani ya miaka mitatu,
tumefikisha vituo vya afya vitano. Alivitaja vituo hivyo kuwa ni Mauno, Busi,
Bereko, Kalamba na Thawi.
Waziri Mkuu anaendelea na
ziara yake wilayani Kondoa ambako atazungumza na wananchi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI, SEPTEMBA 20, 2018.
No comments:
Post a Comment