Na WFM Mjini Bali Indonesia
Marekebisho ya Sheria ya
Takwimu ya Mwaka 2018, hayawazuii wadau
wa takwimu kutoa takwimu kwa ajili ya
matumizi yao bali marekebisho hayo yanaweka misingi ya kuzingatiwa wakati wa utoaji wa takwimu hizo.
Hayo yameelezwa na Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor
Mpango, alipofanya mkutano na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha (IMF) anayewakilisha
Tanzania na nchi nyingine (Africa Group 1 Constituency), Bw. Maxwell Mkwezalamba,
katika Mikutano ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)
mjini Bali Indoneshia.
Dkt. Mpango amesema kuwa
lengo la marekebisho ya sheria hiyo ni kurahisisha ufanyaji
wa tafiti na utoaji wa
matokeo ya tafiti
na sio kuwabana wadau katika ukusanyaji wa taarifa za kitakwimu au
kuzuia mijadala ya uchambuzi wa kisera wa matokeo ya takwimu
rasmi.
“Tumekubaliana kutumia
fursa ya kuboresha Kanuni za Takwimu kwa ajili ya kuweka mazingira ya utekelezaji mzuri wa
vipengele
vya sheria vilivyorekebishwa kwa kuwashirikisha
wadau mbalimbali ili kuelewa lengo la marekebisho hayo”, alieleza Dkt. Mpango.
Marekebisho hayo ya kanuni
za takwimu yatawezesha utekelezaji mzuri wa vifungu vya sheria
vilivyorekebishwa ambapo ametoa wito kwa wadau kushiriki katika mchakato wa marekebisho hayo.
Aidha, Waziri alieleza kuwa mwezi Novemba mwaka huu
Serikali itakutana na wadau wa maendeleo, ili kutoa fursa kwa wadau hao kuelewa kwa
kina dhumuni la Serikali kufanya
marekebisho yaliyofanyika na kupitishwa na Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwezi Septemba 2018.
Vilevile,
Waziri Mpango,
alimueleza Mkurugenzi Mtendaji wa IMF kuwa marekebisho makubwa ya
kiuchumi ambayo yamefanywa na
Serikali ya Awamu ya Tano yameambatana na mabadiliko ya sheria
mbalimbali hususan sheria za za madini kwa lengo la kuhakikisha
rasilimali za nchi zinawanufaisha wananchi lakini pia wawekezaji
wanaowekeza
fedha zao nchini.
Aidha, alisema kuwa Bw.
Kwezilamba, ni mwakilishi wa Tanzania kwenye Bodi ya Magavana wa IMF, hivyo ni
muhimu aelewe maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanayofanyika nchini Tanzania ili
aweze kueleza uhalisia kwenye mikutano ya Bodi hiyo.
Naye Gavana wa Benki Kuu
ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga, alisema kuwa BoT imeendelea kuboresha
Sera ya Fedha ya Mwaka 2017 ili kutatua changamoto za Sekta ya Fedha zinazoibuka
zikiwemo za uhaba wa mikopo hasa katika Sekta binafsi.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Fedha (IMF) anaeiwakilisha Tanzania, Bw. Maxwell Mkwezelamba,
aliipongeza Tanzania kwa hatua mbalimbali za maendeleo ya uchumi kwa kuwa imeendelea kuwa nchi inayopiga hatua kubwa ya maendeleo na kuwa
mfano katika nchi za Afrika.
Ameishauri Tanzania
kutumia ofisi yake ili Washirika wa Maendeleo waelewe dhumuni la marekebisho ya
kiuchumi yanayoenda sambamba na maboresho ya sheria mbalimbali ili maendeleo
hayo yawe endelevu.
Vilevile Dkt. Mpango, alifanya
mkutano na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia (WB) anayewakilisha Tanzania
na nchi nyingine (Africa Group 1 Constituency), Bw. Andrew Bvumbe, wakati wa mikutano ya mwaka
ya WB na IMF inayofanyika mjini Bali
Indonesia na kupongeza ushirikiano wa kimaendeleo na taasisi hizo.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano Serikali
Wizara
ya Fedha na Mipango
Mjini
Bali, Indonesia
No comments:
Post a Comment