Na. WFM, Bali Indonesia
Nchi za Afrika ikiwemo
Tanzania zinatakiwa kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye maarifa na elimu ili
kuendana na soko la ushindani linaloendelea kwa kasi Duniani
Hayo yalibainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango ambaye pia ni mwakilishi wa Tanzania katika Bodi ya Magavana
wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Dkt. Philip Isdor Mpango, wakati wa mikutano
ya WB na IMF mjini Bali Indonesia.
Dkt. Mpango alisema kuwa,
katika mikutano hiyo ya Kimataifa yapo mambo ambayo Tanzania inatakiwa
kuyafanyia kazi wakati huu ambao inapiga hatua kuelekea katika uchumi wa kati
unaotegemea viwanda ambapo elimu inayotolewa inatakiwa kujikita katika kukuza
maarifa na ujuzi .
“Wakati suala la teknolojia
likiangaziwa katika bara la Afrika ni vema kuangalia pia namna ya kukabiliana
na changamoto zinazotokana na teknolojia hiyo kwa kuwa katika maeneo mengi
ajira za watu zimepungua kutokana
na mashine kuchukua nafasi za watu”,
alisema Dkt. Mpango.
Alisema mikutano ya Benki ya Dunia na Shirika la
Fedha la Kimataifa imekua na umuhimu
mkubwa kwa kuwa wadau wamebadilishana mawazo ambayo yamelenga kukabiliana na
changamoto za kiuchumi ambazo zimeendelea kutokea Duniani ikiwa ni pamoja na
baadhi ya nchi kuwa juu kiuchumi na nyingine kuendelea kuporomoka kwa kasi.
Katika mikutano hiyo
Tanzania imetajwa kuwa uchumi wake unaendelea kuimarika ambapo kwa sasa unakua
kwa takribani asilimia sita hivyo kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika
na Dunia kwa ujumla.
Wajumbe wa mikutano hiyo
wametakiwa pia kukabiliana na suala la mabadiliko ya tabia nchi katika nchi zao
kwa kuwa yanaathari kubwa katika uchumi hasa katika Sekta ya afya kutokana na
kuongezeka kwa magonjwa lakini pia mafuriko na ukame.
Naye Kamishna wa Fedha za
Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. John Rubuka, alisema kuwa suala la amani
duniani limejadiliwa kwa kina katika mikutano hiyo kwa kuwa ni chachu ya
maendeleo si tu ya kiuchumi lakini pia ya kijamii.
Mikutano ya Benki ya Dunia
na Shirika la Fedha la Kimataifa inaendelea Mjini Bali Indonesia, ambapo imewakutanisha
Mawaziri, Magavana na wadau wa masuala ya Fedha na Uchumi kutoka nchini
mbalimbali duniani.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini
Wizara
ya Fedha na Mipango
Mjini
Bali Indonesia
No comments:
Post a Comment