HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 12, 2018

300 WAMILIKI VIWANJA KUPITIA AMANA BENKI, PIL

NA SULEIMAN MSUYA

BENKI ya Amana  na Kampuni ya Property International (PIL), zinewezesha wateja zaidi ya 300 wa benki hiyo kumiliki viwanja venye hati miliki kwa kipindi cha miaka mitatu.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya Amana Munir Rajab wakati akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kuwakabidhi hati wateja na kutangaza kuendelea na biashara ya umilikishaji viwanja na PIL.

Rajab alisema benki hiyo iliingia mkataba na PIL ambao uliwezesha wateja wa benki hiyo kukopeshwa viwanja na kulipa kwa kipindi cha miaka mitatu ambapo mafanikio yameonekana.

Mkuu huyo wa Idara alisema  utaratibu huo wa kuwawezesha wateja wao kumiliki viwanja umekuwa na manufaa makubwa hivyo wamekubali kuongeza muda wa mkataba.

"Amana benki imedhamiria kubadilisha maisha ya Watanzania na moja ya njia ya kufikia malengo hayo ni wananchi kumiliki viwanja vyao venye hati ili waweze kupata mikopo itakayowasidia kuwekeza," alisema.

Rajab alisema kuanzia sasa mteja wa benki hiyo ambaye atapata mkopo wa kiwanja atatakiwa kurejesha baada ya miaka mitatu kutoka mmoja na nusu wa awali.

Aidha, alisema wamewapunguzia faida  kutoka asilimia 14 hadi 12 kwa mwaka ili waweze kurejesha kwa wakati.

"Mteja anatakiwa kutanguliza asilimia 20 ya thamani ya kiwanja kama malipo ya awali na kulipa kiasi kilichobaki kwa muda usiozidi miaka mitatu na kila mita ya mraba moja atapata punguzo la shilingi 1,000, " alisema.

Mkuu huyo wa Idara alisema  watatumia wiki ya huduma kwa wateja inayoanza Novemba 19/2018 hadi Novemba 24/2018 kuuza viwanja kwa bei ya punguzo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Undeshaji wa PIL, George Obado alisema ubia huo walioingia na Amana benki umekuwa mkombozi wa watanzania wengi.

Alisema viwanja ambavyo vinauzwa na PIL vina ukubwa wa kuanzia mita za mraba 300 hadi 1,000 na kwamba miundombinu inazingatiwa katika kuvigawa.

Obado alitoa wito kwa wateja wa benki hiyo kutumia fursa hiyo ili waweze kujipatia viwanja vya bei rahisi na vyenye hati miliki.

Wanufaika Nora Laizer, Aisha Spana na Stephen Mathias ambao ni wateja wa benki hiyo walisema mkopo huo wa viwanja umewahakikishia maisha bora na kuahidi kutumia hati hizo kukopa fedha iki wajikite katika ujasiriliamali.

No comments:

Post a Comment

Pages